Mkakati wa SUA kuwa kitovu cha utafiti, uvumbuzi

Jukwaa kuu walipokuwa wamekaa viongozi wa chuo hicho na wageni wengine waalikwa. Katikati ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Jaji mstaafu, Joseph Warioba

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu, changamoto kuu ya vyuo vikuu nchini imekuwa uhaba wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na madarasa, maabara kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, hosteli na upungufu wa watumishi.Kwa muda mrefu, changamoto kuu ya vyuo vikuu nchini imekuwa uhaba wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na madarasa, maabara kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, hosteli na upungufu wa watumishi.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo kwenye milima ya Uluguru mkoani Morogoro, sawa na vingine vingi, kimekuwa kikikumbwa na uhaba huo, licha ya kwamba kinaendelea kuwa miongoni mwa taasisi bora za elimu ya juu nchini.

Taasisi hiyo imekuwa bora zaidi linapokuja suala la utafiti wa kilimo, ambayo matokeo yake yamekuwa yakileta mapinduzi katika sekta ya kilimo kutoka ngazi ya jamii hadi taifa.

“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, pia kuna changamoto mbalimbali ambazo tumeendelea kukabiliana nazo. Kubwa zaidi ni ukosefu wa miundombinu ya kutosha na uhaba wa wafanyakazi,”anafichua Profesa Raphael Chibunda, Makamu Mkuu wa chuo hicho, alipokuwa akihutubia kwenye sherehe za mahafali ya 40 ya chuo hicho wiki iliyopita.

Lakini ujio wa mradi mkubwa wenye lengo la kuleta mageuzi katika maeneo mbalimbali ya elimu ya juu ikiwamo fedha, upanuzi wa miundombinu na kujenga uwezo, umeanza kubadili taswira nzima ya taasisi za elimu ya juu za hapa nchini ikiwemo SUA.

Sehemu ya wahitimu wa chuo hicho katika mahafali ya 40 yaliyofanyika chuoni hapo.

Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mapinduzi ya Kiuchumi (HEET) ni mradi wa miaka mitano wenye thamani ya dola milioni 425 (Sh972 bilioni) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia na unalenga kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuibua nguvu ya elimu ya juu ili kusukuma maendeleo ya uchumi wa nchi.

Kutokana na mradi huo, Profesa Chibunda anabainisha kuwa SUA ina mpango maalum wa ujenzi wa miundombinu mipya katika kampasi za Edward Moringe, Solomon Mahlangu na Mizengo Pinda kupitia mradi huo.

Katika mradi huo, kituo cha fikra za kilimo kimetengewa kiasi cha Sh73.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu, uboreshaji wa mitalaa, ununuzi wa vifaa na kuwezesha mafunzo ya watumishi.

Kadhalika, Profesa Chibunda anabainisha kuwa chuo kitajenga majengo 11 kwa ajili ya kujifunzia na kufundishia. Majengo sita yatajengwa katika kampasi ya Edward Moringe, majengo mawili katika kampasi ya Solomon Mahlangu na majengo matatu katika kampasi ya Mizengo Pinda.

“Majengo haya ni pamoja na hosteli tatu, majengo matatu ya kitaaluma, bweni moja na maabara tatu na jengo moja kwa ajili ya kukuza utafiti na ubunifu katika fani za uhandisi na Tehama,” anafafanua Profesa Chibunda.

Pia, anasema wanaishukuru Serikali kwa kutoa kibali kwa chuo hicho kuajiri watumishi wapya 140 (wanataaluma 93 na watendaji 47) kwani hadi sasa watumishi 77 wameajiriwa na kuripoti kazini.

“Mchakato wa ajira kwa watumishi waliobaki upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, watumishi hawa watasaidia sana kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi,” anafafanua zaidi.

SUA yapeperusha bendera ya utafiti

Katika nyanja ya taaluma na utafiti, chuo hicho cha kilimo kimeendelea kufanya vizuri, kama vile matokeo yaliyotolewa na Google Scholar citation index ya Julai, 2022, SUA ilishika nafasi ya kwanza kitaifa katika nyanja ya utafiti, na ya 42 barani Afrika.

Aidha, katika orodha ya watafiti bora 1000 nchini Tanzania iliyotolewa na shirika la ad science index SUA imeendelea kutoa watafiti bora nchini yenye jumla ya watafiti 222 katika orodha hiyo.

“Kati ya watafiti bora 100 nchini Tanzania, SUA ilitoa watafiti bora 33 na mtafiti namba moja nchini anatoka SUA,” anathibitisha Profesa Chibunda katika mahojiano.

Pamoja na yote chuo kinaendelea kujitanua kwa lengo la kuwafikia Watanzania wengi. Kwa maana hiyo, upanuzi wa kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi unaendelea kwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanajamii na watumishi.

Hadi kufikia Oktoba, 2022 chuo kimetumia Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu na ununuzi wa vifaa na huduma.

Katika mwezi wa Novemba, chuo kimepokea miradi mipya 25 ya utafiti yenye thamani ya Sh8.07 bilioni. Miradi hiyo inafadhiliwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

“Chuo kimeendelea kuwezesha tafiti mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo watafiti vijana kufanya tafiti na kupata majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii yetu,” anasema Profesa Chibunda.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, utafiti na ushauri wa kitaalamu) Profesa Maulid Mwatawala (katiakti), akiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, utawala na Fedha) Profesa Amandus Muhairwa (kushoto) na Profesa Yonika Ngaga (kulia)

Chuo kilitumia zaidi ya Sh458 milioni kufadhili shughuli za utafiti, machapisho na ubunifu kwa wasomi 34 vijana.

Kadhalika, chuo kilinunua mashine na vifaa mbalimbali kwa ajili ya warsha za uhandisi wa kilimo. Vifaa vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine ya CNC lathe, mashine ya kusaga wima na meza za kuchora (30) zenye thamani ya Sh450 milioni.

Katika kukifanya chuo hicho kuishi ndoto yake ya kuwa kituo cha watafiti na wahitimu bora, kumekuwepo na uboreshaji wa mashamba ya mafunzo kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa uanzishwaji wa kiwanda cha kuzalisha vifaranga vya samaki aina ya kambare.

Kiwanda hicho kinadaiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha vifaranga milioni mbili kwa mwezi. “Hivyo nitumie fursa hii kuwaalika wafugaji wa samaki kuja kununua vifaranga bora vya samaki kutoka hapa.”

Chuo kimekamilisha ujenzi wa jengo la Cross Learning lenye vyumba vya madarasa nane na maabara nane. Jengo hilo limejengwa kwa gharama ya Sh11.7 bilioni na lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,205 kwa wakati mmoja.

Mchango kwa Taifa

Licha ya kuwa chuo hicho kuendelea kutoa wahitimu wengi waliojiajiri katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo cha kisasa, ufugaji wa samaki, kuku, ng’ombe na nyinginezo zilizokijikita katika ubunifu wa utunzaji wa mazingira, wapo watumishi wengi ambao wako serikalini na wengine sekta binafsi wanaoendelea kukiwakilisha chuo vizuri.

Anasema watumishi wake wameteuliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi, wizara na uenyekiti na ujumbe wa bodi na kamati katika mashirika mbalimbali nchini.

“Katika kipindi hiki cha taarifa, watumishi wanane waliteuliwa na mamlaka za uteuzi kushika nyadhifa mbalimbali,” anasema.

Mmoja wa watumishi wa umma ambao wameendelea kupeperusha bendera ya chuo hicho ni Suleiman Jafo, Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Jafo aliyewahi kusoma hapo, alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuitisha (convocation) chuo hicho mnamo Novemba 24, 2022.

Jafo anaeleza kuwa alipokuwa akisoma chuoni hapo miaka 20 iliyopita, kulikuwa na wanafunzi chini ya 5,000 lakini sasa idadi ya wanafunzi imeongezeka na kufikia zaidi ya 15,000.

“Sio ongezeko la wanafunzi pekee, bali pia mmeongeza wigo mpana katika fani ya utaalamu. Wale ambao hawajui chuo hiki kilitoka wapi hawawezi kueleza mabadiliko makubwa yanayoendelea,” anaeleza Jafo.

“Nilikuja kusoma hapa na mpaka sasa hivi naamini, wanafunzi wa SUA wanapomaliza wanajulikana kwa jina la ‘trainable’, wanafunzi wakitoka hapa na kuajiriwa popote, wana uwezo wa kufanya kazi/kufundishika na kukiwakilisha chuo hiki vyema,” anaongeza.

Alibainisha kuwa SUA imemjenga sana katika kazi zake na kumfanya aendelee na juhudi hizo kila anapopewa nafasi ya kuongoza au kufanya kazi sehemu yoyote ikiwemo wizara mbalimbali alizowahi kuzishika.

Kuhusu sherehe ya mahafali ya 40

Dira ya SUA ya kuwa chuo kikuu kinachoongoza katika utoaji wa maarifa bora, ujuzi na ubunifu katika kilimo na sayansi shirikishi ilitimizwa tena katika Kampasi Kuu (Edward Moringe) iliyoko kilomita tatu Kusini mwa Manispaa ya Morogoro.

Maelfu ya watu wakiwemo wazazi na wahitimu zaidi ya 3000, marafiki na walezi walijaa mbele ya chuo hicho siku ya Ijumaa Novemba 25 wakisubiri kutunukiwa vyeti vyao na kusherehekea umahiri walioupata chuoni hapo.

Kikiwa na dhamira ya kufanya mafunzo, utafiti wa kilimo na sayansi shirikishi na kutoa matokeo yenye ushindani mkubwa ambayo yanachangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya kitaifa, kikanda na kimataifa, mwaka huu wanafunzi 3,744 walitunukiwa vyeti na digrii mbalimbali.

Katika mahafali ya mwaka huu, kulikuwa na jumla ya programu za masomo 59 zenye jumla ya wahitimu 3,744 (wanaume 2,223 na wanawake 1,479).

Wahitimu wa Shahada ya Kwanza waliostahili kutunukiwa ni 3,425 (wanaume 2,083 na wanawake 1,342), Shahada za Uzamili ni 41 (wanaume 23 na wanawake 18).

Diploma mbili za Elimu ya Juu, mwanamume na mwanamke. Kulikuwa na wahitimu tisa wa PhD (wanaume 8 na mwanamke mmoja).

Kadhalika, wahitimu wa Diploma walikuwa 220 (wanaume 121 na wanawake 99) na wahitimu 48 wa Cheti (wanaume 29 na wanawake 19). Miongoni mwa waliotunukiwa, jumla ya wanawake waliotunukiwa katika mahafali hayo ni 1,479 sawa na asilimia 39.5 ya wahitimu wote.

“Idadi ya wahitimu kwa mwaka wa masomo 2021/2022 imepungua kidogo kutoka 4,078 mwaka 2021 hadi 3,744 kwani baadhi walihitimu katika mahafali ya katikati ya mwaka yaliyofanyika Mei,” Profesa Chibunda alieleza wakati wa hotuba yake.

Aidha, alisema baada ya kuhitimu ni wakati wa wahitimu kutafakari sura mpya ya maisha yao; ambapo wataingia duniani na mazingira ya kazi na ujenzi wa taifa.

“Bidii mliyoonyesha wakati wa masomo, uaminifu, na ari ya kusoma, muendelee kuwa nayo katika maeneo yenu ya kazi ili muweze kufaulu huko,” alishauri.

“Ni matarajio yetu kuwa mafanikio haya yatakuwa chachu ya ufanisi, tija na ubunifu katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa, ikiwemo kuzalisha mali na kutoa huduma bora kwa jamii na taifa kwa ujumla,” aliongeza.

Aidha, alisema wanatarajia wahitimu wao kuwa mabalozi wazuri wa kukitangaza chuo vizuri kwa tabia zao nzuri na maadili ya kazi. “Ni matarajio ya chuo kuwa watatumia elimu waliyoipata kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu na kwa maendeleo ya nchi yetu.”

Wakati huo huo, ilifichuka kuwa katika mwaka wa masomo 2022/2023, chuo kimesajili wanafunzi 5,025 wa shahada ya kwanza na uzamili. Aidha, chuo kimesajili jumla ya wanafunzi 187 kwa masomo ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu.

Hivi sasa chuo kina jumla ya wanafunzi 16,556. Miongoni mwao, wanafunzi 15,522 ni wa shahada za kwanza na 1,034 ni wa shahada za juu.

“Kuna wanafunzi wa kigeni 112 chuoni (shahada 27 na shahada za juu 85) kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika na nje ya Bara la Afrika,” alisema Prof Chibunda.

SUA inajulikana zaidi kwa kutoa kozi na programu nyingi katika fani ya Kilimo, Sayansi ya Mifugo, Misitu, Sayansi ya Wanyama, Usimamizi wa Wanyamapori, Usimamizi wa Utalii, Sayansi ya Mazingira, Sayansi ya Chakula, Maliasili, Lishe, Maendeleo Vijijini, tangu kuanzishwa kwake.

Kampasi

Kampasi Kuu (Edward Moringe) ambayo iko kilomita tatu Kusini mwa Manispaa ya Morogoro, Kampasi ya Solomon Mahlangu (ambayo ilikuwa hadi 1992 Chuo cha Uhuru cha Solomon Mahlangu cha African National Congress ya Afrika Kusini) kilichoko kilomita 11 Kaskazini-Magharibi mwa Manispaa ya Morogoro.

Nyingine ni Kampasi ya Olmotonyi iliyopo Arusha, ambayo pia ni kituo cha mafunzo ya vitendo vya Misitu, Hifadhi ya Misitu ya Mazumbai iliyopo Lushoto (huu ni msitu wa asili unaotmika kwa mafunzo na utafiti), Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo Mkoani Katavi.