Mkulazi yaanza kwa kishindo
Sukari ni bidhaa muhimu nchini ambayo inatumiwa na watanzania walio wengi. Bidhaa hii nchini inatengenezwa kwa kutumia miwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Sukari, mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka 2023/24 ni wastani wa tani 807,000 ambapo sukari kwa matumizi ya kawaida ni tani 552,000 na kwa mahitaji ya viwandani ni tani 255,000. Mahitaji ya sukari nchini yanaongezeka kulingana na ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya tabia.
Kwa kuzingatia umuhimu wa bidhaa hii, Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya sukari na kuwezesha kuanzishwa kwa viwanda vipya vya sukari nchini, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha sukari Mkulazi.
Ukuaji wa Sekta ya sukari umekuwa na mchango mkubwa kiuchumi kwani umeongeza wigo wa kodi nchini, ajira kwa watanzania, kutoa fursa za kilimo cha miwa kibiashara na fursa za kibiashara kwa wauzaji na wasambazaji wa sukari.
Wakati uwezo wa ndani ya nchi wa kuzalisha sukari ya kawaida (Brown Sugar) ukiongezeka kila mwaka. Serikali imeendelea na juhudi mbalimbali za kuandaa mazingira bora ya viwanda vya ndani kuanza kuzalisha sukari ya viwandani “Industrial Sugar), ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani.
Jitihada hizo ni pamoja ujenzi wa kiwanda kipya cha sukari Mkulazi. Kiwanda hiki kinamilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza (SHIMA).
Kiwanda hiki kimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya sukari nchini kwani kina uwezo wa kuzalisha tani 50,000 za sukari ya kawaida na sukari ya viwandani kwa mwaka.
Katika mahojiano maalamu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hodhi ya Mkulazi, Dkt. Hildelitha Msita alisema kwamba wakati walipokabidhiwa kusimamia mradi huu walihakikisha kila kitu kinafanyika kwa utaalamu, kuanzia kilimo , umwagiliaji na kuajiri wataalamu. Tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kufikia malengo tuliyojiwekea.
Dkt Msita alimshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kuzindua kiwanda cha sukari Mkulazi kwani yalikuwa matamanio yao kiwanda hiki kizinduliwe na Mhe. Dkt.Samia.
Pia Dkt Msita alisema kwamba, kiwanda cha sukari Mkulazi kimekuwa na hamasa kubwa kwa wadau mbalimbali kwani kitaondoa tatizo la uhaba wa sukari nchini.
Vilevile Dkt Msita amemhakikishia Rais Mhe. Dkt. Samia watatekeleza maagizo yote ambayo aliyoyatoa siku ya uzinduzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi Agosti 7, 2024.
“Lazima tusimamie kiwanda hiki kiweze kuzalisha, kilete faida, kiwe endelevu lakini kiweze kuhudumia wananchi kwa maana bidhaa zinazotoka kiwandani hapa zitawasaidia wananchi katika maisha yao ya kila siku na Serikali itapata ahueni ya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi.” Alisema Dkt Msita.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hodhi ya Mkulazi Selestine Some alisema tulikamilisha ujenzi wa kiwanda mwezi Novemba 2023 na majaribio yakaanza Novemba 2023 ambayo yalienda mpaka Machi 2024 mara baada ya hapo msimu wa mvua ulianza hivyo, kiwanda kikasimama tayari kwa kuanza uzalishaji msimu wa 2024/25. Mnamo tarehe 1 Julai 2024 msimu wetu wa kwanza wa mwaka 2024/25 ulianza rasmi kwa kuzalisha na kuuza sukari sokoni.
Pia Some alisema anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua kiwanda cha sukari Mkulazi mnamo tarehe 7, Agosti 2024.
Some aliongezea kuwa wafanyakazi wa Kampuni tulifarijika sana, kwani tunatambua kwamba Mhe.Rais Samia ana majukumu mengi sana ya Kitaifa lakini alitenga muda kwa ajili yetu, kuja kukagua na kuzindua kiwanda.
“Sisi tumeanza kutekeleza agizo la Mh. Rais Samia wa kujipanga kuzalisha sukari ya viwandani, kwani kampuni yetu na kiwanda chetu kinauwezo wa kuzalisha sukari ya Viwandani (Industrial Sugar) na hivyo, msimu wa 2025/26 kiwanda kitaanza rasmi kuzalisha sukari hii ya viwandani.
Some amesema sukari ya Mkulazi imeingia sokoni tangu Julai 2024, sukari hii, ina ubora mzuri sana. Pia, ametoa rai kwa wananchi walipo Jirani na kiwanda hiki, kutumia fursa hii kubwa kulima miwa kibiashara kwani kampuni imejipanga kununua miwa mingi kutoka kwa wakulima.
Aliongeza pia, kampuni ina idara inayotoa huduma za kitaalamu kwa wakulima wa miwa na tuko tayari kuwafundisha namna nzuri ya kulima miwa kibiashara. Kampuni pia, imejipanga kutoa mbegu za kisasa kwa wakulima ili waweze kuzalisha miwa yenye ubora.
Akizungumzia kuhusu ajira Some alisema kiwanda kwa sasa kimetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 2,176 .Aidha, ajira ambazo sio za moja kwa moja (indirect employment) ambazo zinatokana na kiwanda hiki zinakadiriwa kufika zaidi ya Watanzania 8000, hivyo kufanya jumla ya ajira 10,176.
Kwa Upande wa Afisa Mwandamizi wa Masoko na Mauzo wa Mkulazi Milkasia Joseph alisema sukari ya Mkulazi imepokelewa vizuri sokoni kutokana na ubora wa sukari tunayozalisha. Hii imesaidia kuongeza wateja wa sukari yetu. Tumeshauza kwenye mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro ambapo kiwanda kipo, Dar es Salaam, Tanga, Iringa, Dodoma na mikoa ya kusini mikoa yaani Lindi na Mtwara.
“Tunatoa fursa kwa wafanyabiashara wote nchini kuweza kufanyabiasha na sisi hii kampuni yetu ni Kampuni ya Umma na haibagui wafanyabiashara. Alisema Milkasia.
Kampuni inatoa, fursa kwa wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo. Mkakati wetu ni kufanya biashara na wafanyabishara wote kusambaza sukari yetu. Bei ya sukari yetu ni nafuu.
Naye Mtaalamu wa Afya ya Udongo wa Mkulazi, Halima Mbaga alisema, kazi za kilimo katika shamba la miwa zinafanyika kwa kutumia mitambo ya kisasa kulima na kupanda miwa. Na pia tunahakikikisha tunafuata kanuni za ulimaji wa miwa ili kuweza kupata tija katika mashamba ya miwa.
Meneja wa kiwanda cha sukari Mkulazi Mhandisi Aron Mwaigaga alisema kiwanda kimeanza kuzalisha sukari na wafanyakazi wanafanya kazi kwenye mazingira salama. Aidha, aliongeza kwamba, “kiwanda cha sukari Mkulazi ni kiwanda cha mfano kwa maana kinasimamiwa na wazawa na kinaendelea kufanya vizuri.” Alisema Mwaigaga
Wakulima wazungumza
Rehema Joseph ni mkulima wa Makiwami AMCOS amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuweza kuzindua kiwanda cha sukari Mkulazi ambapo wakulima wa miwa wamepata fursa ya kuuza miwa.
Meneja wa Chama cha msingi Makiwami AMCOS Karimu Saif ameishukuru Kampuni Hodhi ya Mkulazi kwa ushirikano wanaotoa kwa wakulima wa miwa na pia ameiomba Serikali kusaidia wakulima wawezeshwe mikopo.
Hamis Idd Barisi ni mkulima wa Msowero AMCOS ameiomba Serikali mitambo mfano trekta za kulima kwa njia ya mkopo au kwa kupunguziwa bei ili waweze kulima kilimo cha kisasa.
Hadija Masud ni mkulima kutoka Mbigiri AMCOS alisema anamshukuru sana Mhe. Rais. Dkt. Samia kwani kwa sasa tunauza miwa yetu kwenye kiwanda cha sukari Mkulazi. Kilimo cha miwa kimekuwa faraja kubwa sana kwetu na tumeona faida ya kulima miwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mradi wa pamoja MAGOLE Kikwete Salum Mluba ameishukuru Mkulazi kwa kutoa ushirikiano kwa wakulima katika hatua za uvunaji na usafirishaji wa miwa kwenda kiwandani na kuhakikisha barabara za mashambani zinaweza kupitika kwa ajili ya kupeleka miwa kiwandani.
Pia ametoa wito kwa wananchi kukimbilia fursa za kilimo cha miwa kwa ajili ya kuuza kwenye kiwanda cha sukari Mkulazi. Chama hiki kinasimamia AMCOS tano zikiwemo Makiwami, Masowero, Mbigiri, Dumila na Malangali AMCOS.