Mkutano wa Rais Samia na viongozi wa Serikali ishara njema kukubalika AICC

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar Mhandisi Zena Said, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella pamoja na mawaziri mara baada ya kufungua mkutano wa faragha wa viongozi hao uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Machi 2, 2023. PICHA NA IKULU.

Hivi karibuni Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kilikuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa faragha wa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wengine wa Serikali katika tukio linaloashiria uwezo wa kituo hicho kutoa huduma bora kwa kiwango cha juu.

Rais Samia Suluhu Hassan aliwaongoza viongozi wa juu Serekalini katika mkutano muhimu wa siku tatu, maarufu kama “semina elekezi,” uliolenga kujenga ufungamanifu kwa viongozi hao wenye majukumu nyeti.

Lilikuwa tukio na wakati muhimu kwa AICC pale kituo hicho kilipochaguliwa tena kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu wa Serikali, na kwa hakika umethibitisha kwa kiasi kikubwa nia ya kituo hicho kukuza viwango vya huduma za mikutano kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mtendaji Mkuu wa AICC aliyeteuliwa hivi karibuni, Ephraim Mafuru, ana furaha kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo mzito wa Serikali ulioendeshwa na Uongozi Institute, taasisi ya uongozi inayojihusisha kujenga na kuimarisha uwezo wa viongozi barani Afrika. Mafuru anaamini AICC ina mengi zaidi ya kutoa.

“Tumepata heshima ya kuwa mwenyeji na kuhudumia Mheshimiwa Rais na timu yake yote katika siku hizi tatu. Huku kulikuwa ni kukubalika kwa wazi kwa AICC na Rais Samia, na kwetu ni mwito wa kutaka tushindane kwa viwango vya juu zaidi.           

“Ninamshukuru Rais kwa imani aliyoonesha kwa AICC, na sisi kwa pamoja, tuna furaha kwamba wateja wetu walifurahi na kuridhika na kiwango cha huduma tulizowapa,” amesema Mafuru.

Mafuru amezikaribisha taasisi nyingine za umma na binafsi kukitumia kituo hicho ili wawe mashahidi wa uwezo wa ushindani wa AICC katika kuhudumia vikao mbalimbali na mikutano yao mikubwa.

“Tuko tayari na tunaahidi kutoa huduma bora kwa wateja wetu huku tukilenga kukuza hadhi ya AICC kama chaguo la kwanza la kitaifa na kikanda kwa huduma za mikutano na tafrija.

AICC pia inaendesha Kituo cha Mikutano cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) cha Dar es Salaam, ambacho umaarufu wake unazidi kukua siku hadi siku. Wiki iliyopita kituo hicho kilikuwa mwenyeji wa wajumbe 800 wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Kituo hicho pia ndiye mwekezaji mkubwa wa majengo ya biashara na makazi jijini Arusha, kikipangisha ofisi za kisasa na nyumba za makazi, hususan kwa wafanyakazi wa taasisi za kiamataifa. AICC pekee ina eneo la ukubwa wa mita za mraba 23,000 katikati ya Jiji la Arusha ama “Geneva ya Afrika,” kama wengine wanavyopenda kuliita.

Kwa sasa, vituo vya AICC na JNICC vimechukua nafasi ya pekee kujenga taswira ya Tanzania kama kituo kikuu cha mikutano na utalii na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi. Hili ni jambo ambalo Mkurugenzi Mkuu mpya ameahidi kulipambania ili Tanzania iwe juu na ijivunie uwezo wake miongoni mwa nchi zinazoitazama.

Kwa mujibu wa Mafuru, utajiri wa miaka 45 ya historia ya AICC pamoja na wito wake; We Bring the World to Tanzania (Tunaileta Dunia Tanzania) ichukuliwe kama chachu ya kuirudisha AICC katika hadhi stahiki na kuchukua nafasi ya pekee katika sekta ya utalii inayoanza kurudia hali yake ya awali baada ya kupungua kwa safari za watalii kulikosababishwa na mlipuko wa Uviko 19.

 “Tutatumia majaliwa yote ya fursa na maeneo tunayoyaweza zaidi kuvutia utalii wa mikutano. Ahadi yangu ni kwamba tutaongeza mara mbili juhudi kuhakikisha AICC, JNICC na vyombo vyake vingine vinatoa huduma za kisasa, shindani na kwa kutumia teknolojia mpya kwa wateja na washirika wetu,” anasema Mafuru.

Alisema biashara ya vituo vya mikutano ni moja ya shughuli zenye muunganiko mkubwa kati ya wazalishaji, watoa huduma na wateja, huku akiongeza kuwa mchango wa mafanikio ya AICC kwa sekta nyingine za uchumi zitasaidia kukuza ubora wa maisha kwa watanzania wengi.

Mafuru ambaye ni mtaalamu wa masoko aliteuliwa hivi karibuni na Rais Samia kuongoza AICC na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa saba wa kituo hicho tangu kianzishwe mwaka 1978.