Mkwawa Tobacco Processors Limited kuleta mapinduzi, kuongeza tija katika sekta ya tumbaku
Tumbaku ni mojawapo ya mazao ya biashara yanayoongoza nchini, ikiwa na nafasi muhimu katika ajira, mapato ya kigeni na maendeleo ya kijamii. Sekta hii ina historia ndefu, iliyoanza rasmi katika kipindi cha ukoloni na kuendelea kukua baada ya Uhuru.
Kilimo cha tumbaku kinafanyika zaidi katika maeneo ya Magharibi na kati mwa Tanzania, ikiwemo mikoa ya Tabora, Iringa, Kigoma, Mbeya na Singida. Wakulima wadogo ndiyo wazalishaji wakuu wa tumbaku, wakilima chini ya mfumo wa ushirika au kupitia mikataba na kampuni za ununuzi.
Sekta ya tumbaku ina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu, tumbaku ni miongoni mwa mazao yanayochangia kwa kiasi kikubwa mapato ya kigeni. Pia, sekta hii inachangia ajira kwa mamilioni ya watu, ikiwa ni pamoja na wakulima, wafanyakazi wa viwanda vya usindikaji, na wale wanaohusika na usafirishaji.
Pamoja na mchango wake mkubwa, sekta ya tumbaku inakabiliwa na changamoto kadhaa. Moja ya changamoto hizo inatajwa kuwa ni bei ya tumbaku kwenye soko la dunia kuyumba, jambo ambalo linawaathiri wakulima.
Serikali na wadau wa sekta hii wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizi. Moja ya mikakati ni kuhimiza matumizi ya teknolojia bora katika kilimo cha tumbaku ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo.
Moja ya wadau wakubwa wa sekta ya tumbaku nchini ambao wamefanya na wanaendelea kufanya juhudi kubwa katika kuleta mapeinduzi ya sekta hiyo ni Kiwanda cha Mkwawa Leaf Tobacco.
Mkwawa Leaf Tobacco kimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya tumbaku nchini kwa kutoa fursa mpya za ajira.Kiwanda hiki kimekuwa na athari kubwa katika uchumi hasa kwa wakulima wa tumbaku.
Kwa kuanzisha miundombinu bora na teknolojia za kisasa za usindikaji, kampuni hii imeboresha ubora wa bidhaa na kuongeza thamani ya tumbaku inayozalishwa nchini.
Katika kuhakikisha kinaendelea kuongeza thamani katika zao la tumbaku na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo, MTPL kimeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Sigara cha Serengeti (SCC) kilichopo Morogoro.
Ili kuleta mapinduzi na kuongeza aina za sigara zinazozalishwa ndani katika soko la kimataifa kwa malengo endelevu, Mkwawa Leaf Tobacco imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha Sigara cha Serengeti (SCC) kinachojengwa mkoani Morogoro.
Kupitia njia 10 za uzalishaji, kiwanda cha SCC kinatarajiwa kuongeza ajira hadi na kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa chanzo kikuu cha mapato kutoka nje na ndani.
Uzinduzi wa kiwanda hicho ulifanyika Agosti 6, 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda hicho, Rais Samia amesema kiwanda hicho kina umuhimu mkubwa sana kwa Taifa na Serikali kwa sababu ya kuzalisha ajira kwa vijana.
“Mkwawa Leaf Tobacco kupitia kampuni dada ya Mkwawa Tobacco Processors Limited (MTPL) imesaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha ajira sasa ikiwa na wafanyakazi 5,000 huku ikiongeza uwezo wa kusindika tumbaku kutoka tani 70,000 mpaka kufikia tani 180,000” alisema Rais Samia.
Alisema kiwanda hicho pia kinakwenda kuongeza mauzo ya tumbaku nje ya nchi jambo linalosaidia kuongeza mapato kwa wakulima wa tumbaku kutokana na kupanda kwa bei ya tumbaku kutoka Dola 1.4 mpaka 2.4 kwa kilo.
Rais Samia alisema uwekezaji uliofanyika umesaidia kuwapa wakulima wa tumbaku nguvu na ari ya kulima zao hilo. “Uwekezaji huu unamuwezesha mkulima wa tumbaku kuuza kila kitu kuanzia jani lenyewe, mizizi ya jani, viungio vya majani nk ambavyo vinachakatwa hapa nchini kupitia MTPL.”
Rais Samia pia alitoa rai kwa kiwanda hicho kusimamia mkakati wa kuwapa nguvu wakulima na kuwasihi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusimamia utunzaji wa mazingira hususani kwenye shughuli za uzalishaji.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema uwekezaji uliofanyika katika kiwanda hicho wenye thamani ya Dola milioni 300 unakwenda kuongeza ajira zinazozalishwa katika sekta ya tumbaku katika Mkoa wa Morogoro kutoka ajira 7,000 mpaka 12,000, uzalishaji wa tumbaku utaongezeka kufikia tani laki tatu kwa mwaka na thamani ya kusafirisha tumbaku kwenda nje ya nchi itafikia Dola 700 milioni.
“Kupitia kiwanda cha sigara cha Serengeti tumekubaliana na kampuni kubwa nne duniani kuja kufanya “blending” (uchanganyaji wa malighafi ya sigara) kwa ajili ya kuziisafirisha kwenda katika nchi zao, hivyo tunakushukuru kwa maelekezo yako na juhudi zako za kuboresha sekta ya tumbaku nchini,” amesema Bashe.
Kwa upande wake mmiliki na Mkurugenzi Mkuu wa MTPL na SCC, Ahmed Huwel alisema uwekezaji unaofanyika katika viwanda hivyo ni mkubwa. Aidha aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini.
“Uwekezaji huu mkubwa tunaofanya wa upanuzi wa MTPL na ujenzi wa SCC ni matunda ya mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali hivyo tunakushuru na pia tuna imani kubwa na uongozi wako wewe binafsi pamoja na mawaziri wote,” alisema Huwel.
Huwel amesema kiwanda hicho ni cha mtanzania ambapo tumbaku inayochakatwa inalimwa na Watanzania jambo linalochangia katika kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuboresha maisha ya wakulima wa tumbaku nchini.
Ujenzi wa Kiwanda cha Sigara cha Serengeti unaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili barani Afrika kuwa na kiwanda cha aina hiyo ambacho kinamilikiwa na wazawa na kutumia malighafi zinazozalishwa nchini.