MSF inavyopunguza vifo vya wajawazito na watoto katika kambi ya wakimbizi Nduta
Kigoma. “Nina furaha kuona akina mama wajawazito wakija hospitalini kwa ajili ya kujifungua wenyewe na wakiondoka makwao na nyuso zenye furaha, wakiwa wamekumbatia vichanga vyao,” anasema Kiongozi wa Timu ya Matabibu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), Kibondo, Elda Kyando.
Kauli ya Elda imebeba hisia za furaha na matumaini kwa maisha ya wakimbizi wanawake katika kambi ya Nduta hata kama tusingesikia wala kuona nyuso zao. Ni ushindi wa kuipambania furaha ya kuwa na familia bora wakiwa mbali na ardhi yao ya asili.
Lakini kwa upande wa Sabina Kwezi, ambaye ni msimamizi wa huduma za ukunga, ni hadithi nzuri isiyokwisha utamu wake akiwa kama kiongozi wa mapambano dhidi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Akielezea uzoefu wa usimamizi wa huduma hizo katika kambi ya Nduta, Sabina anasema, “Nikiwa kama msimamizi wa huduma za ukunga katika kambi ya Nduta, nasimamia timu ya watoa huduma za uzazi za kina kwa wanawake, vichanga na mama wajawazito.
Huduma zetu zilijumuisha huduma za uzazi (chumba cha kujifungulia na uzalishaji), huduma za dharura kwa watoto na akina mama na huduma za uangalizi kwa wajawazito na baada ya uzazi.”
Kwa kuongezea, anasema; “Pia, tunahudumia wajawazito walio katika hatari na changamoto zitokanazo na uchungu kwa wajawazito kwa kuwapa rufaa ya kupatiwa huduma mbadala za dharura za uzazi kwenye vituo vya afya vibobezi haraka iwezekanavyo.”
Anasema kuwa upo utaratibu mzuri wa utoaji rufaa kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo ambayo ni sehemu ya mkakati wao wa utoaji huduma bora za uzazi za afya ili kufikia matokeo lengwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nduta na jamii wenyeji.
Akizungumzia lengo la upunguzaji wa vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama na watoto, anasema kupitia uboreshaji utoaji huduma za afya kwa mama na mtoto ikijumuisha mahudhurio wakati wa uzalishaji (ukunga) na utoaji rufaa kwa wakati kwa wajawazito walio katika hatari zaidi, matarajio ni kuona vifo hivyo vinaendelea kupungua zaidi kambini hapo.
Sabina anasema miongoni mwa changamoto za kiafya ambazo zinatajwa kuongoza kusababisha vifo hivyo ni pamoja na utokaji mwingi wa damu baada ya kujifungua, shinikizo la damu na wingi wa protini kwa mama wajawazito, mwitikio mkali wa kinga ya mwili dhidi ya maambukizi unaoweza kuathiri viungo na matatizo ya uchungu.
Anasema kuwa programu za afya za jamii zimeongeza uelewa na imani juu ya huduma za afya za mama na mtoto, ikichangia mwamko wa wanawake wengi kutaka kupatiwa huduma hizo mapema.
Ushirikiano na taasisi za afya za kimataifa kama vile Medical Teams International, International Rescue Committee na Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, umehakikisha kuwa visa hatarishi zaidi vinapewa kipaumbele.
“Licha ya changamoto, hatua hizi zinatengeneza mazingira mazuri zaidi katika utoaji wa huduma za afya za dharura, na kuchagiza matokeo makubwa ya huduma za afya za wanawake wajawazito na watoto wachanga.”
“Kwa wastani, tunatoa rufaa zipatazo 40 kila mwezi, hususan katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo. Kwa hakika, tumejifunza mambo kadhaa muhimu katika shughuli zetu,” anasema Sabina na kuongeza kuwa: “Kwanza, umuhimu wa kukabiliana na mazingira yaliyopo na upatikanaji wa rasilimali zote katika kutoa huduma bora za afya.
Pia tumeona faida kubwa ya kuwa na programu za uimarishaji afya ya jamii katika kuwawezesha watu kujali afya zao, na kuleta matokeo bora ya huduma za afya.”
Akizungumzia miundombinu, Sabina anasema hospitali ya Nduta ina vitanda 15 kwa ajili ya huduma za afya ya uzazi kati ya 74. Pia ina dawa, vifaatiba na rasilimali watu wenye weledi wa kutosha. Hospitali pia inatoa huduma kwa kufuata miongozo iliyofafanuliwa vizuri, yenye msingi wa tafiti mbalimbali kutoka kwa Wizara ya Afya (MOH) na MSF.
Hospitali ina mfumo mzuri utoaji rufavibobezi haraka iwezekanavyo, hususan kwa wajawazito walio hatarini. Anabainisha uwepo wa benki ya damu, ambayo imekuwa muhimu katika kuokoa maisha, hususan wale walio katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na upotezaji wa damu nyingi wakati au baada ya kujifungua.
Sabina anakumbuka, “Siku moja usiku nilipigiwa simu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kuhusu mgonjwa tuliyempa rufaa ambaye alikuwa anavuja damu nyingi sana. Hospitali haikuwa na damu inayolingana na mahitaji yake na hivyo ilikuwa vigumu kumpata mtu wa kumtolea damu.
Nilifanikiwa kupata idhini ya kutumia benki yetu ya damu na chupa tatu za damu zilitumika kuokoa maisha ya mwanamke yule.” Anabainisha kuwa mwaka huu hospitali hiyo imetoa rufaa ya visa 191 vya akina mama katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo na kufanya idadi ya rufaa kwenda katika hospitali kufikia 624 tangu Januari.
Kumbukumbu zisizosahaulika
Mkaazi wa Kijiji cha Malolongwa, Kata ya Kumgondo, Wilaya ya Kibondo, Lilian Fabian ni mmoja wa wanawake wanufaika wa huduma za afya ya uzazi zinazotolewa katika Hospitali ya Nduta kutokana na huduma hizo kutolewa bila ya malipo na kwa ubora wa hali ya juu.
“Nina watoto watatu ambao wote nimejifungulia kwenye hospitali ya Nduta. Tulipokuwa tunakuja kambini tulipewa kibali maalumu cha kuingia kambini. Huduma zao kwa kweli ni nzuri na wahudumu wao ni wakarimu.
Utasilikizwa na kuhudumiwa vizuri. Tunaishukuru Serikali na wadau wengine walio nyuma ya kambi hii kwa kuwa jitihada zao zimeendelea kutusaidia,” anaeleza Lilian.
Moja ya kumbukumbu za kuvutia ni upatikanaji wa mapacha waliokuwa na changamoto kwa mafanikio chini ya timu ya wataalamu wa huduma za uzazi za dharura, zoezi lililochangia usalama wa mama na watoto baada ya kuzaliwa kwao.
Kumbukumbu nyingine kubwa ni ile ya uzazi kwa njia ya upasuaji wa mafanikio kwa mama mjamzito aliyekuwa na historia ya kujifungua watoto wanne kwa upasuaji huko nyuma na aliweza kupata mtoto wake salama.
Ajenda ya upunguzaji vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi
Licha ya nia ya dhati ya Serikali ya kuendelea kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano, lakini afya ni ya jamii nzima na hivyo sekta binafsi nazo zina dhima katika ajenda hii.
Kule Kigoma, ipo Taasisi ya Médecins Sans Frontières (MSF) – Madaktari Wasio na Mipaka – ambayo imekuwa ikitoa huduma za afya za dharura kwa wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokarasia ya Congo, Burundi na Rwanda na jamii wenyeji wanaozunguka kambi ya wakimbizi ya Nduta.
Ikiendesha huduma hizo tangu mwaka 1993, kati ya mwaka 1995 mpaka 2001, MSF ilisaidia kuendesha kliniki za huduma za udhibiti wa Malaria, kutoa huduma za upatikanaji wa majisafi na salama na kutoa huduma za afya za awali kwa maeneo ya Kasulu, Mtwara na Kigoma.
Pia, MS ilitekeleza mradi wa wa maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu kwa mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Dodoma, Mtwara, Arusha, Tanga na kisiwa cha Pemba. Kati ya mwaka 2001 na 2004, juhudi za kukabiliana na Malaria na UKIMWI zilielekezwa katika visiwa vya Pemba na Unguja (Zanzibar) na Makete na Njombe.
Mwaka 2015, Shirika lilianza kutoa chanjo na matibabu ya Kipindupindu pamoja na huduma za matibabu ya awali ya ugonjwa wa Malaria katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, mkoani Kigoma.
Kati ya mwaka 2016 hadi 2018, hospitali iliyokuwa na vitanda vipatavyo 175 iliyokuwa ikitoa huduma za awali za afya ilianzishwa katika kambi ya wakimbizi ya Nduta. Katika kipindi cha 2017- 2018, msaada wa kitaalamu ulitolewa kwa Wizara ya Afya Zanzibar dhidi ya Kipindupindu.
Miaka iliyofuata ilishuhudia mipango mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa huduma za upasuaji wa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo (2018), kukabiliana na ugonjwa wa Ebola na Kipindupindu (2019), na mradi mpya katika Wilaya ya Liwale wa afya ya mama na mtoto (2022).
MSF iliendelea kukabiliana na milipuko ya kipindupindu na dharura nyingine za kiafya, ikiwa ni pamoja na homa ya Marburg, mpango wa kudhibiti malaria na ule wa chanjo ya watu wengi mwaka 2023, kipindupindu huko Mara, Kalya- Uvinza.
Hata hivyo, mwaka 2024, MSF ilikabiliana na mlipuko wa kipindupindu huko Nanjilinji, Lindi. Kwa upande wa Kusini mwa Tanzania, Mkoa wa Lindi, hospitali ya Wilaya ya Liwale MSF inaendesha programu ya jamii za wilaya hiyo kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya za awali na uzazi kwa wajawazito na watoto.
Ni mpango jumuishi unaotekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ili kuhakikisha uendelevu na mwendelezo wa huduma za afya zinazopendekezwa.