Mwisho wa hadaa; Kwa nini COP27 iwe kweli COP ya Afrika?

Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Dk Omar Shajak, akifungua kongamano la kitaifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya nishati lililofanyika Oktoba 20, jijini Dar es Salaam. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaojulikana zaidi kama Mkutano wa Nchi Wanachama (COP 27) utafanyika kuanzia tarehe 6 hadi 18 Novemba 2022 mjini Sharm El Sheikh, Misri. Mkutano wa mwaka huu umetambulishwa kama COP ya Afrika’ kwa kuwa utafanyika Afrika.

Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaojulikana zaidi kama Mkutano wa Nchi Wanachama (COP 27) utafanyika kuanzia tarehe 6 hadi 18 Novemba 2022 mjini Sharm El Sheikh, Misri. Mkutano wa mwaka huu umetambulishwa kama COP ya Afrika’ kwa kuwa utafanyika Afrika.

Kinachofurahisha zaidi ni kwamba hii si mara ya kwanza kwa mkutano wa aina hiyo kufanyika katika bara la Afrika (Afrika imekuwa mwenyeji wa mikutano mingine ya COP hapo kabla ambayo ilifanyika Morocco, Durban na Nairobi) na kama tukirejelea COP zilizopita, ahadi na malengo ya mabadiliko ya tabianchi hayajawahi kuheshimiwa, hasa na nchi zinazoongoza duniani katika suala la utoaji wa hewa ukaa hata baada ya Mkataba wa Paris.

Mwaka 2009, katika COP15 mataifa yaliyoendelea yaliahidi mchango wa kila mwaka wa Dola za Marekani 100 bilioni ifikapo 2020. Katika COP15 na COP16 mataifa yaliyoendelea yaliahidi mchango wa kila mwaka wa Dola za Marekani 100 bilioni ifikapo 2020. Fedha hizi hazikuonekana. Na muda huo uliotengwa kwa ajili ya kuchangisha kiasi hicho cha fedha ulisogezwa mpaka katika COP26 mwaka 2025.

Katika mazingira mbalimbali, uongozi wa kisiasa barani Afrika mara nyingi haukufungamana katika msimamo wa pamoja uliojielekeza juu ya hali halisi ya watu wa bara hili, maisha na uchumi wao kama wachangiaji wa mwisho wa athari za mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, sauti na malalamiko ya watu mara nyingi hayajumuishwi katika majadiliano na taratibu zinazofuatia.

Matokeo halisi yamekuwa mchakato wa kitaalamu na kidiplomasia ambao umesababisha kulegalega kwa harakati za mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kusahauliwa huku Afrika ikibeba mzigo mkubwa wa athari zake.

Nikiwa mwanafunzi wa diplomasia ya uchumi, tulijifunza kuwa moja ya mikakati ya kufanikiwa katika majadiliano ni kuchagua eneo na wakati. Katika kubuni mkakati wa majadiliano wenye mafanikio, tunafundishwa au kushauriwa kuchagua mahali na wakati ambao ni rafiki kwako na ambao unaweza kuwa mgumu au si rafiki kwa mwenzio au upande wa pili unaojadili nao.

Acha ajenda igawanywe katika maeneo mengi na mikutano muhimu ifanyike katika sehemu mbalimbali na uhakikishe ujumbe wa mwenzako unapata wakati mgumu kuhudhuria kikamilifu. Inaonekana huu ndio mkakati ambao tayari unatumika katika COP27.

Gharama za kufanyia mkutano Sharm El Sheikh ni kubwa mno kwa wajumbe wengi wa Afrika. Aidha, idadi ya wajumbe walioteuliwa kuwakilisha ni ndogo mno, na beji za kuteuliwa na ruksa (registration and accreditation) ya kufika Sham El Sheik kama mwakilishi ziliadimika, jambo ambalo limepunguza zaidi idadi ya wajumbe kutoka bara la Afrika.

Kwa kuzingatia haya, sauti ya Afrika na wengi ambao hawawezi kumudu gharama katika COP27 ambao pia ndiyo waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi, huenda zisisikike tena au kwa sauti kubwa.

Kwa kuangalia uzoefu na kadhia hii, azaki sita za Afrika Mashariki na Kusini (CSOs) yaani Taasisi ya Utawala wa Maliasili-NRGI, Publish What you Pay, Tax Justice Network Africa, Oxfam, Powershift Africa na Eco-News Africa zilihamasisha kuwepo kwa mfululizo wa majadiliano ya kimtandao ili kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya changamoto zinazofanana za mabadiliko ya tabianchi na mapinduzi ya nishati kwa kuwa yanalihusu moja kwa moja bara la Afrika na watu wake. Matarajio makubwa ni kwamba COP ya mwaka huu lazima iwe kweli kwa ajili ya bara la Afrika!


Mabadiliko ya tabianchi yamefika, mafanikio haiwezekani bila kusikiliza sauti ya watu

Licha ya kuwa mchafuzi wa kiwango cha chini zaidi wa mazingira, Afrika bado inakabiliwa na hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi na hatari za mapinduzi ya nishati. Ripoti za awali za IPCC zinaonyesha kuwa Afrika inakabiliwa na ongezeko kubwa la joto na kupanda kwa kiwango cha maji baharini kuliko mahali pengine popote duniani.

Katika muongo ujao, Afrika itakabiliwa na mawimbi ya joto kali ya hadi mara 5 zaidi kuwahi kutokea, mvua isiyo na uhakika zaidi, ukame n.k. Afrika inakabiliwa na uharibifu mkubwa na hivyo njia za kupunguza athari zake na kukabiliana na janga hilo zinahitajika ili kupunguza hatari za jumla za mabadiliko ya tabianchi.

Hivi sasa, Mashariki na Pembe ya Afrika inakabiliwa na ukame kwa zaidi ya miaka 40, huku kati ya watu milioni 22 hadi milioni 50 wakikabiliwa na njaa na zaidi ya watoto milioni 3.4 tayari wana utapiamlo. Mvua za Machi hadi Mei zilikuwa za kiwango cha chini zaidi katika miaka 70 ambayo imesababisha kutokufanya vizuri kwa mazao na kupoteza mamilioni ya mifugo, vitu ambavyo ni muhimu kwa maisha.

Kwetu sisi, hatari kubwa zaidi ya ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi yapo kila mahali na kila siku tunakabiliana nayo. Ikiwa na eneo la msitu lenye jumla ya kilomita za mraba 7,13,789 ambalo ni asilimia 21.71-24.6 ya eneo la kijiografia la nchi, Tanzania ni mojawapo ya maeneo makubwa yaliyobaki yanayonyonya hewa ya ukaa.

Misitu ya Tanzania inazuia zaidi ya tani milioni 2,019 za kaboni kwa ujumla wake. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba kati ya 1990 na 2010, Tanzania ilipoteza asilimia 19.4 ya eneo la misitu yake, au takriban hekta 8,067,000. Kwa kiwango hiki, tunaweza kupoteza nusu ya misitu yetu ifikapo 2030.

Kupanda kwa ghafla kwa kina cha bahari kwa futi 3 kunatosha kuitosa Zanzibar yote majini. Wanasayansi wa taasisi ya National Geographic wanakadiria kuwa visiwa vya Zanzibar na Mafia huenda vikatoweka chini ya maji ifikapo mwaka 2100 kutokana na kupanda kwa kina cha bahari kunakochochewa na ongezeko la joto duniani.

Duniani kote, kiwango cha bahari kimepanda takriban inchi nane tangu mwanzo wa karne ya 20 na zaidi ya inchi mbili katika miaka 20 iliyopita pekee. Kila mwaka, kina cha bahari hupanda inchi nyingine 13 (milimita 3.2). Utafiti mpya uliochapishwa Februari 15, 2022, unaonyesha kuwa kiwango cha maji baharini kinaongezeka kwa kasi na kinatarajiwa kupanda kwa futi moja kufikia 2050.

COP27 ya mwaka huu kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Mapinduzi ya nishati kutoka nishati chafu kwenda nishati safi inapaswa kuwahusu watu. Mabadiliko hayawezi kufikiwa ikiwa watu wengi tayari wameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na uwezekano wa kuathiriwa na mapinduzi ya nishati ni mkubwa, na kama hatua za kukabiliana na hali hazisikiki kwenye meza ya mazungumzo.


Upatikanaji wa teknolojia

Kuhakikisha teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zipatikana na kwa unafuu katika bara la Afrika. Gharama ya teknolojia kadhaa zinazozalisha kiwango kidogo cha hewa ya ukaa imeshuka tangu 2010 na sera za kuweka pamoja za uvumbuzi zimewezesha gharama hizo kushuka.

Mifumo yote ya uvumbuzi na sera za kuweka pamoja vimesaidia kukabili athari tawanyizi, za kimazingira, na kijamii zinazoweza kuhusishwa na usambazaji wa teknolojia za gharama nafuu duniani. Kwa bahati mbaya, uwekezaji huu na maendeleo ya kiteknolojia haujagawanywa ipasavyo. Teknolojia hizo ni chache katika nchi zinazoendelea na Afrika kwa ujumla.

Wakati mabadiliko hayo yanafanyika, Afrika inaachwa nyuma, lakini inaharakisha na inatarajiwa kufikia kasi sawa na nchi zile zilizoendelea. Hivyo, mabadiliko ya haki katika maana halisi yanahitajika ambayo yanaruhusu au kuwezesha Afrika kufaidika katika maendeleo ya teknolojia ya mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea.

Afrika haipaswi kuwa soko pekee, bali pia mzalishaji wa teknolojia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kama jambo la msingi na la haki, tuache uzalishaji wa teknolojia hizi ufanyike pia katika bara la Afrika ili kutumia rasilimali zilizopo barani, kuongeza thamani, na kuzalisha nafasi za kazi.


Mafuta na gesi ya Afrika

Inatakiwa kuisaidia Afrika kutumia rasilimali zake asilia katika muda mfupi kwa kadiri inavyopitia mabadiliko. Afrika ina hazina kubwa ya makaa ya mawe na kwa sasa ndiye mzalishaji anayekua kwa kasi kwa upatikanaji wa mafuta na gesi. Gesi nyingi imepatikana Tanzania, Musumbiji, Namibia na Senegal. Ni dhahiri kuwa Afrika itaendelea kutegemea katika rasilimali asilia kama vile mafuta na gesi kama chanzo cha nishati kwa mustakabali wa muda mrefu unaotarajiwa zaidi na nchi zilizoendelea kulingana na hali yake ya umaskini wa nishati na ongezeko la idadi ya watu.

Afrika ni mzalishaji mdogo wa mafuta lakini mafuta ni tegemeo ya kiuchumi. N Swali ni iwapo wazalishaji wapya kama vile Uganda wanapaswa kusonga mbele. Jibu lake labda liko katika kusawazisha uchumi wa gharama za fursa, masoko ya baadaye na kutumia vyema biashara ya kikanda kwa masoko ya Afrika ambayo pengine yanaweza kuendelea kutegemea mafuta kwa muda mrefu katika siku za usoni.

Kuna maoni tofauti juu ya bara hili juu ya mustakabali wa gesi kama chanzo cha nishati. Swali linaloulizwa mara nyingi ni ikiwa gesi inaweza kurejelewa kama nishati asilia ‘safi’. Gesi inachukuliwa kuwa nishati asilia safi ya kimabadiliko zaidi, kwani inatoa hewa ya ukaa chini ya asilimia 50 kuliko mafuta na makaa ya mawe. Hivyo ni chaguo bora, kwani nishati jadidifu ziko thabiti kiteknolojia na kiuchumi kukabili kutokupatikana kwa nishati katika vipindi tofauti.

Makubaliano yaliyopo ya viongozi wa kisiasa barani Afrika yanaonekana kuunga mkono kuendelea kwa uwekezaji na matumizi ya gesi kama chanzo cha kimabadiliko cha nishati ili kuimarisha mipango yao ya mchanganyiko wa nishati ili kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza Afrika katika siku zijazo. Hoja yangu ni usawa unaoruhusu Afrika kutumia gesi yake kwa maendeleo kwa sasa wakati mipango ya upatikanaji wa nishati safi ikiendelea lakini pia Africa inatakiwa iwe makini wakati huo huo kutokujifunga kwa kutumia nishati ambayo si endelevu kwa siku za usoni.


Makaa ya mawe ya Afrika na mustakabali wa mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya nishati

Afrika ina hazina kubwa ya makaa ya mawe. Vita vya hivi karibuni vinavyoendelea vya Urusi dhidi ya Ukraine vinaonyesha kuwa licha ya utabiri wa hapo awali, matumizi ya makaa ya joto kama chanzo cha nishati sasa yanaweza kuwa ya muda mrefu kuliko ilivyodhaniwa, kwani nchi za Ulaya kama Ujerumani zinapanga kuwasha tena mitambo yao ya makaa ya joto kama njia ya kujitenga mbali na utegemezi wa gesi ya Urusi, kukidhi mahitaji ya sasa ya nishati na kuhakikisha usalama wao wa nishati wa siku zijazo.

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika mkutano wa 27 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Tabianchi (COP 27).

Duniani kote, kumekuwa na ongezeko la mahitaji na bei ya makaa ya joto iliyofikia zaidi ya dola 400 kwa tani kutoka dola 176 kwa tani mwaka jana na takriban dola 75 mwaka 2020. Ulaya iko tayari kulipa zaidi ya mara mbili ya bei ya makaa ya mawe mwaka jana. Kwa hivyo hii inaipa Afrika fursa ya kutumia na kufaidika katika mahitaji ya muda mfupi, na au bila kupoteza kabisa na kujifungia katika mustakabali wa matumizi ya hewa ya ukaa.

Kwa nchi za Afrika zenye utajiri wa makaa ya mawe kama vile Tanzania, miezi michache iliyopita imeshuhudia kuimarika kwa mauzo ya makaa ya mawe nje ya nchi. Kwa mujibu wa Tume ya Madini na ripoti za Reuters, Tanzania inatarajia kuongeza maradufu mauzo yake ya makaa ya mawe mwaka huu hadi takriban tani 696,773, huku uzalishaji ukitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 50 hadi takriban tani 1,364,707. Huu unaweza kuwa ubashiri wenye gharama zaidi kuwahi kuufanya, lakini mustakabali wake wa muda mrefu hauwezi kuwekewa dhamana.

Vita vya Ukraine vinaweza kuongeza kasi ya mabadiliko barani Ulaya. Kwa hiyo, ningeshauri nchi kama Tanzania kutumia mapato yatokanayo na makaa ya mawe kuwekeza katika mifumo safi ya nishati. Fungamanisha mfumo wa kisheria na sera hadi mwisho wa mradi. Nchi zilizoendelea zinapaswa kutoa ufadhili kwa awamu kuelekea mwishoni mwa mradi.


Madini ya nishati safi (Green or transition minerals) ya Afrika na mustakabali tunaoutaka

Madini ya technolojia ya nishati safi au Green, Critical or transition Minerals kwa kingereza, ya Afrika yanapaswa kuchagiza ustawi wa kiuchumi na mabadiliko ya ndani ya nchi. Afrika imejaliwa kuwa na hazina kubwa ya madini ambayo ni muhimu kwa teknolojia ya nishati safi inayohitajika kusaidia mapinduzi ya nishati na kuelekea katika lengo la kufikia uchafuzi wa mazingira sifuri.

Afrika inazalisha mafuta kidogo lakini madini mengi. Kulingana na takwimu, kati ya asilimia 48 hadi 70 ya kobalti (ambayo hutumiwa katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme na simu) na asilimia 4 ya shaba na asilimia 1 ya lithiamu inapatikana nchini DRC. Tanzania na Msumbiji zinachukua asilimia 45 ya madini ya grafiti duniani, huku Tanzania pekee ikishika nafasi ya 5 ya hifadhi kubwa ya madini duniani. Utatifiti uliofanyika na NRGI mwaka jana ulionyesha kwamba Tanzania ina aina 24 ya madini adimu muhimu katika technolojia ya nishati safi. Hu ni utajiri mkubwa

Afrika imekuwa chanzo cha rasilimali za maendeleo ya dunia. Madini barani Afrika kwa kiasi kikubwa yamekuwa chanzo cha umaskini na vifo. Mabadiliko ya haki hayawezi kufikiwa ikiwa madini ya Afrika yatatumiwa kwa ajili ya maendeleo ya kiteknolojia na usalama wa nishati mahali pengine. Nchi tajiri za rasilimali za Afrika hazipaswi kuwa watazamaji katika mabadiliko haya ya nishati. Wakati huu lazima tufikirie jinsi ya kujipanga, ili tusijikute katika kitendawili cha laana ya rasilimali ambayo itatufanya kuwa wanyonge kwa muda mrefu.


Tupange maendeleo ya Afrika kwa kufata Ajenda ya Afrika 2063

Kupunguza ongezeko la joto duniani kufikia sentigredi 1.5 kunahitaji hatua muhimu ya kushuka kwa karibu nusu ya matumizi kutoka kwenye nishati asilia hadi nishati safi ifikapo 2030 na kwamba uzalishaji wa hewa chafu duniani kufikia sifuri kamili ifikapo 2050. Hii ni miaka minane tu kutoka sasa na nchi nyingi za Afrika hazitamudu kuuvuka muda huo uliowekwa. Afrika haipaswi kuonewa katika mapinduzi ya nishati.

Ili kuwa na mabadiliko ya haki barani Afrika, Serikali na ushiriki wa Waafrika ni muhimu katika kuweka ajenda ya majadiliano ya COP27 na kutafuta shabaha zinazowezekana. Kusikiliza maoni ya watu na kuyapa kipaumbele.

Afrika inahitaji kuendeleza au kuifafanua upya dira na dhamira yake juu ya mabadiliko ya tabianchi na mapinduzi ya nishati. Kuifafanua upya dira inaweza kuwa tofauti kidogo na maono ya dunia, lakini ikafungamana na dira ya Afrika, mahitaji na vipengele vinavyotambulisha maendeleo au vichochezi vya maendeleo. Kwa mfano, kuweka malengo ya mapinduzi ya nishati barani Afrika ili kufungamana na Ajenda 2063 ni wazo linalokubalika.

Katika ngazi ya Serikali, utekelezaji wa mpango waUamuzi wa Kitaifa wa kila nchi wa mchango wake kwenye Mabadiliko ya tabia nchi (Nationally Determined Contributions-NDCs) na Mipango ya Taifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ni muhimu. Kuwa na uwezo wa kushawishi ufadhili wa NDCs utakuwa chachu ya mabadiliko muhimu katika kukabili mabadiliko ya tabianchi.


Utumiaji wa nishati jadidifu kwa mustakabali wa Afrika

Uwezo wa Afrika wa nishati jadidifu hauna kikomo, hata iwe kwa kutumia teknolojia ya kawaida na uwekezaji uliopo. Uwezo wake wa nishati ya photovoltaic, kwa mfano, unaweza kuzalisha umeme wa takriban kilowati 660,000 kwa saa, ambayo ni kiasi kikubwa cha nishati kwa eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Ramani za jua na upepo na atlasi zipo. Hii ni pamoja na ramani za uchumi wa buluu, ambazo zimetengenezwa katika nchi kama vile Kenya, Afrika Kusini na Zanzibar, miongoni mwa nyingine. Hivyo, uwezekano wa kuzalisha fursa ya ajira katika sekta hii ni mkubwa sana.

Tanzania in uwezo mkubwa sana kuliko nchi za jirani. Licha ya uwezo huu, Afrika bado iko nyuma katika uzalishaji na matumizi ya nishati ya jua na upepo ikilinganishwa na nchi nyingine zilizoendelea na uzalishaji wa umeme wa jua na upepo wa bara uko chini zaidi ikilinganishwa na Jimbo la California nchini Marekani pekee.

Kwa takwimu hizi za sasa, Afrika inaweza kubaki mtazamaji wa kudumu katika teknolojia ya nishati jadidifu. Kama ilivyoelezwa hapo awali, teknolojia ya nishati safi haipo katika bara hili, huku Afrika ikiwa bado nchi inayoagiza vifaa vya nishati safi kama vile paneli za jua na mitambo ya upepo. Ili Afrika kufaidika, uwekezaji katika teknolojia na utengenezaji wa vifaa lazima ufanywe ndani ya bara la Afrika.


Hadi sasa hakuna nchi yoyote ya Kiafrika iliyo na kiwanda hata kimoja cha kutengeneza paneli za jua au mitambo ya upepo. Afrika ni bara la watumiaji wengi wa vifaa vya umeme wa jua, licha ya kujaliwa kuwa na fursa kubwa ya kuweza kuzalisha umeme wa jua kwa kuwa kando ya ikweta. Afrika haiwezi kuwa muagizaji wa paneli za jua iwe ni kizazi cha 1, kizazi cha 2 au kizazi cha 3 milele. Kwa tani za uranium zinazochimbwa Afrika Magharibi, hakuna mtambo wa uranium au nyuklia uliopo Afrika Magharibi. Ubaguzi huu na ukosefu wa usawa wa kiuchumi, hata ndani ya mazingira ya mabadiliko ya tabianchi, lazima ushughulikiwe kwa haraka.


Ufadhili kukabili mabadiliko ya tabianchi na mapinduzi ya nishati Afrika

Mabadiliko ya haki ya nishati kwa Afrika hayawezi kufikiwa bila uwezeshaji wa kifedha. Kuna ukwasi wa kutosha na mtaji wa kuwezesha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Mwaka 2010 nchi zilizoendelea zilijitolea kutoa Dola za Marekani 100 bilioni kila mwaka kwa ajili ya kuwezesha mikakati ya kukabili mabadiliko ya tabianchi. Kwa bahati mbaya, ahadi hii haijatekelezwa na bara la Afrika limekosa mambo mengi.

Kwa mujibu wa jarida la Africa Renewal la Umoja wa Mataifa la Septemba 2022, hadi sasa, ni Dola za Marekani bilioni 80 tu kati ya ahadi ya dola bilioni 100 kwa mwaka ya nchi zilizoendelea kwa nchi zinazoendelea ifikapo 2020 ndiyo zimetolewa. Kati ya hizo, ni takriban dola bilioni 20 pekee zilizotolewa kwa Afrika kuanzia 2016-2019.

Afrika ina uhitaji na inakabiliwa na uhaba mkubwa wa upatikanaji wa nishati. Takriban watu milioni 759 barani Afrika bado hawana umeme. Kulingana na UN Road Map to 2030, inahitajika 35bln tu kila mwaka kufikisha umeme kwa watu milioni 759 ambao hawana umeme kwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa hakika, kwa kiwango cha chini cha Dola za Marekani bilioni 25 zinazotumika kila mwaka, zinaweza kusaidia watu wote bilioni 2.6 ambao hawana umeme, lakini hakuna dalili ya kuzipata fedha hizi. COP27 inapaswa kuondoa aibu hii ambayo imejidhihirisha katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kufadhili mipango dhidi ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika na njia za mapinduzi ya nishati kuna faida kwa Afrika na nchi zilizoendelea, kwani kwa sababu ya eneo lake na viwango vya chini vya utoaji hewa chafu, Afrika hadi sasa ndiyo nchi yenye uwezo wa kunyonya hewa ya ukaa na kuisaidia dunia.

Afrika haiko tayari kuwezesha mabadiliko ya haki kwa sababu Seŕikali zake zina bajeti ndogo za fedha ya kuwezesha mipango hiyo kutokana na shinikizo la kushughulikia madeni na kushindana kwa vipaumbele kwa matumizi ya huduma za kijamii.

Nchi zilizoendelea lazima zitoe fungu la kuwezesha mikakati hiyo kama ilivyokuwa katika mikutano iliyopita na kuziba mianya ya mitaji haramu mtaji haramu na mtiririko wa fedha kutoka Afrika ili kuwezesha bara hilo kutumia fedha hizo kuwezesha mabadiliko hayo.

Ili Afrika iwe tayari kwa mabadiliko ya tabianchi na mapinduzi ya nishati, kuna haja ya kuziba mianya iliyopo ya uwezeshaji fedha ambayo inawezesha Mtiririko Haramu wa Kifedha hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 89 kila mwaka (kulingana na ripoti ya Biashara na Maendeleo ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa 2020). Hii hata hivyo inaonyesha kuwa Afrika inaweza kufikia na kuzidi deni lake la uwezeshaji fedha la Dola za Marekani 70 bilioni kwa nishati jadidifu ikiwa mianya hii ya kodi itafungwa.

Wakatika wajumbe hao wa Mkutano Mabadiliko ya Tabianchi (COP27), wanapokutana nchini Misri, nchi zilizoendelea ambazo ndizo wachafuzi wakubwa wa mazingira na wachangiaji wakubwa wa ongezeko la joto duniani zinapaswa kuwajibika na kufidia hasara na uharibifu utakaoupata nchi zinazoendelea kama Tanzania. Zinapaswa kuleta teknolojia ambayo inahitajika ili kutumia nishati safi kama vile kuvuta na kuhifadhi nishati ya jua.

Ipe Afrika njia za kifedha na tutakabili mabadiliko ya tabianchi. Tupe teknolojia ya bei nafuu na tutaleta nishati jadidifu. Ongeza thamani ya madini yetu ya kijani katika bara la Afrika ili nchi kama Tanzania, Zambia na DRC ziweze kunufaika na faida kutokana na rasilimali zetu za madini.

Tupeni muda wa kutosha ili tuweze kukimbizana nanyi katika utengenezaji wa mifumo yetu ya nishati. Na muhimu Zaidi, sikiliza sauti zetu katika COP27 na tunaweza kupambana kwa pamoja dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kufikia malengo ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu hadi sifuri. Mukomeshe ahadi hewa mufanyee COP27 iwe COP ya Afrika kweli.