Namna mfumo wa viwango vya tozo katika sekta ya madini unavyochochea ukuaji wa uchumi Tanzania

Muktasari:

Toka kupata uhuru, Tanzania imefanya moberesho ya kisera na sheria ili kuimarisha ukuaji na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa nchi. Msingi huu ndio umeifanya HakiRasilimali kufanya uchambuzi yakinifu uliojikita katika kuchunguza ufanisi wa mifumo au viwango vya tozo vilivyoainishwa kuchochea mchango wa sekta ya madini nchini.kta ya madini na mchango wake.

Toka kupata uhuru, Tanzania imefanya moberesho ya kisera na sheria ili kuimarisha ukuaji na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa nchi. Msingi huu ndio umeifanya HakiRasilimali kufanya uchambuzi yakinifu uliojikita katika kuchunguza ufanisi wa mifumo au viwango vya tozo vilivyoainishwa kuchochea mchango wa sekta ya madini nchini.kta ya madini na mchango wake.

Mfumo wa viwango vya tozo unajumuisha sera, sheria na kanuni zinazosimamia mgawanyo wa faida za kiuchumi na mapato kati ya Serikali na wawekezaji katika sekta ya madini.

Maelezo ya jumla kuhusu sekta madini

Shughuli za uchimbaji madini nchini Tanzania zimekuwepo hata kabla ya uhuru, zikihusisha uchimbaji mkubwa na uchimbaji mdogo. Hii ni kwa sababu Tanzania imejaaliwa utajiri wa madini ya aina mbalimbali kama vile dhahabu, shaba, almasi, Tanzanite, zinki, makaa ya mawe, uranium, vito n.k. Kwahiyo ili kutathimini sera na sheria zinazosimamia sekta ya madini kwa undani ni muhimu kuangalia mwenendo mzima kupitia historia ya uchimbaji madini Tanzania.

II.            Sheria zinazosimamia sekta ya madini tanzania

Sekta ya Madini Tanzania, inasimamiwa na sheria mbalimbali zikiwemo Sheria ya Madini ya 2019, Sura ya 123 ambayo inatoa udhibiti wa shughuli za uchimbaji madini, pamoja na utafutaji, uchimbaji na usindikaji wa madini, na kuweka ruzuku, umiliki, masharti, kukomesha upotoshwaji wa madini, ulipaji wa ushuru anuwai, ada, ushuru, mirabaha na ada zingine zinazotumika katika sekta ya madini; Sheria ya Mamlaka ya Kudumu kwenye Utajiri wa Asili wa Rasilimali na Maliasili ya mwaka 2017, ambayo inaweka masharti juu ya umiliki wa kudumu wa utajiri wa asili wa rasilimali na maliasili na kuainisha kuwa utajiri na mamlaka hayo juu ya watu wa Tanzania na Serikali; ambapo Rais amepewa mamlaka ya usimamizi kwa niaba ya raia wa Tanzania; na kwa kusudi hilo, shughuli zote zinazohusiana na utafutaji wa maliasili na rasilimali zinapaswa kufanywa kwa uangalizi wa Serikali kwa niaba ya wananchi; Sheria ya Mikataba na Utajiri wa Maliasili na Rasilimali (Upitiaji na Uboreshaji Masharti Yenye Shaka) ya mwaka 2017 ambayo inatoa mamlaka kwa Bunge kukagua mikataba iliyohitimishwa na Serikali na kutoa haki kwa Serikali kupitia na kujadili tena masharti ambayo inaona hayakubaliki katika mikataba ambayo tayari imesaini; na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015 ambayo inaanzisha Kamati ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa madhumuni ya kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uziduaji na maswala mengine yanayohusiana na sekta hiyo


III.           Mfumo wa viwango mbalimbali vya tozo katika sekta ya madini

Mfumo wa viwango vya tozo katika sekta ya madini nchini Tanzania unaundwa na sheria na kanuni mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sheria ya Madini, Sura ya 123; Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004; Sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982; Sheria ya Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) sura ya 148 na Sheria ya Forodha. Hii pia inajumuisha ada na tozo mbalimbali zilizowekwa na Mamlaka za Serikali kama vile zinazosimamia masuala ya mazingira (NEMC &TFS), usalama kazini (OSHA & Jeshi la Zimamoto na Uokoaji), usimamizi wa maji (Mamlaka ya bonde la maji chini ya ofisi ya Makamu wa Rais), kemikali, vyakula na viwango vya bidhaa za viwandani (GCLA, TMDA &TBS), kuuza nje na kuagiza bidhaa (TASAC) n.k.

Ni kwa namna gani mfumo wa tozo katika sekta ya madini unachochea ukuaji wa uchumi wa tanzania

Uchumi wa Tanzania unakua kutokana na mchango wa sekta mbalimbali, ambapo kwa mwaka wa fedha 2019/20 na 2020/21 ripoti za uchumi na Benki kuu zinaonyesha kua sekta ya madini imekuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye uchumi ikilinganishwa na sekta nyingine za kiuchumi kama vile sekta ya Kilimo.

Viashiria muhimu vya mchango wa sekta ya madini katika uchumi ni pamoja na mchango wake kwenye: Kuvutia uwekezaji kutoka nje; mapato ya Serikali; Uuzaji madini nje ya nchi; Ajira; Ushirikishwaji wa wazawa katika mnyororo wa thamani; Mchango kwenye pato ya taifauchumi wa madini; Uwekezaji wa makampuni kwenye jamii; Fedha za kigeni

i.              Kuvutia uwekezaji kutoka nje

Uwekezaji binafsi kutoka nje kwenye sekta ya madini umechangia ushiriki wa ndani, kuongeza uwezo wa uzalishaji, utafiti na mendeleo, kuinua sekta nyingine, kutengeneza ajira na biashara nyingine zinazohusiana. Kwa mujibu wa UNICTAD 2020, katika mwaka 2019, wekezaji kwenye sekta uliongezeka kwa asilimia 5 na kufikia dola bilioni 1.1

ii.             Mapato ya Serikali

Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000,  mchango wa sekta ya madini umeonekana kwenye pato ghafi la Taifa, pia kwenye mapato ya Serikali na mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi. Kwa kipindi cha 2017/2018, Kwa mfano, makusanyo ya maduhuli ya Serikali katika sekta ya madini  yaliongezeka kutoka Tshs. 168 bilioni mwaka 2014/15 mpaka Tsh. 528.24 bilioni mwaka 2019/20, huku mapato yatokanayo na mrabaha yakifikia 85% ya mapato ya Serikali.


iii.            Mchango wa madini kwenye uuzaji bidhaa nje ya nchi

Sekta ya Madini inachangia kwa kiasi cha asilimia 50 ya mauzo yote ya nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazoongoza kuuza madini nje. Mwaka 2017, Tanzania ilitajwa kuwa nchi ya nne kwa uuzaji nje wa dhahabu, nyuma ya Afrika kusini, Ghana na Mali. Lakini pia Tanzania ni nchi ya 32 duniani kwa uuzaji nje ya nchi wa dhahabu.

iv.           Mchango kwenye ajira

inakadiriwa kuwa watu 7,355 wameajiriwa moja kwa moja na sekta ya madini, na wengine zaidi ya 3,000 kwenye ajira zisizo za moja kwa moja. Taarifa ya mwaka 2011 ya Wizara ya nishati na madini iliyokadiria idadi ya wachimbaji wadogo kufikia Watanzania 600,000.

v.            Uwezeshaji wazawa katika mnyororo wa thamani kwenye sekta ya madini.

Ripoti ya Baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC) ya mwaka 2020 inaeleza kua sekta ya madini imefanikisha kuongeza/ kuchangia thamani ya jumla ya kiasi cha Tsh 2,401,072,998,521, kati ya kiasi hicho Tsh. 1,576,033,614,142 sawa 66% ilitokana na manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka makampuni ya wazawa, huku kiasi cha Tsh. 825,039,384,379 sawa na 44% kilitokana na manunuzi yaliyofanywa kutoka kwa makampuni ya nje ya nchi.

vi.           Mchango katika fedha za kigeni

Sekta ya madini imeripotiwa kuingiza fedha za kigeni kwa kiwango kikubwa takribani 50% ya mapato ya mauzo yote ya nchi za nje. Kwa mwaka 2019 sekta ya madini iliingiza fedha za kigeni kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.7. Kiwango hiki kilizidi kiwango cha fedha za kigeni zilizoingizwa na sekta ya utalii ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiongoza.

vii.          Maeneo mengine ambayo sekta ya Madini ilifikia mchango wa utendaji kwa uchumi

a)            Ukuaji wa sekta ya madini kwa wastani wa asilimia 17.7%.

b)            Kuongezeka kwa Uzalishaji na Sekta ndogo ASM kufikia kilogramu 15,593.67 za Dhahabu zenye thamani ya TZS 1,536,832,201,590.31, mnamo mwaka 2019/2020, sawa na 29% ya jumla ya uzalishaji wote wa dhahabu nchini.

c)            Kuongezeka kwa uzalishaji wa vito vya madini ya Tanzanite, mnamo mwaka 2020, mawe makubwa ya madini ya Tanzanite yenye uzito wa 9.12 kg , 5.1kg na 6.3 kg yalichimbwa katika eneo la tengefu la Mererani na kununuliwa na Serikali kwa ada ya takribani ya dola za Kimarekani 5.4 milioni.

d)            Serikali kupata hisa zisizopungua asilimia 16 (undiluted free carried interest shares) katika kampuni za uchimbaji wa ubia za Twiga Minerals Corporation Limited na Tembo Nickel Corporation kufuatia ubia kati ya Serikali na Barrick Gold Corporation na Kabanga Nickel. Serikali pia itapata 50% ya ya mgawanyo wa faida za kiuchumi kupita ubia huo.


IV.          Mapendekezo

i.              Utulivu wa sekta ya madini katika kuchangia ukuaji wa uchumi unategemea sana mfumo wa mapato ya Serikali uliopo katika sekta ya madini, hivyo utulivu wa sheria za kodi utasaidia kuwawekezaji zaidi katika sekta hii.

ii.             Serikali iharakishe utekelezaji wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara (Blue-Print), andiko lililohibitishwa na Baraza la Mawaziri mwaka 2019 ambalo litasaidia kutatua malalamiko mengi kama kuunganisha majukumu ya baadhi ya taasisi za usimamizi na kupunguza mrundikano wa kodi yameelezwa kwenye azimio hilo.

iii.            Shughuli za utafiti wa madini ni moja ya shughuli muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa sekta ya madini. Serikali ishirikiane na wadau wa utafiti wa madini kuhakikisha vifungu vyote visivyo rafiki vinapitiwa upya ili kuhakikisha kuwa vinalinda rasilimali lakini wakati huo huo vinalinda na kuvutia uwekezaji wa watafiti.

iv.           Ni muhimu kwa Tanzania kutunga Sheria ya usimamizi wa mapato ya madini ili kuunda mfuko wa madini, utaratibu unaopaswa kuigwa kutoka kwenye Mfuko wa mafuta na gesi.

v.            Mikataba ya kuzuia utozaji kodi mara mbili kwa mapato au mali inayoingiwa kati ya mataifa mawili au zaidi (DTAs) ni mikataba muhimu katika kurahisisha usimamizi wa kodi kwa makampuni ya kimataifa endapo tu mikataba hiyo itatengewa vizuri. Ili kudhibiti makampuni ya kimataifa kukwepa kodi, Tanzania inatakiwa kuiangalia upya mikataba hii ili kuwezesha kuondoa uwezekano wa makapuni ya kimataifa kuyatumia majukwaa hayo kwa malengo ya kukwepa kodi