Ni suala la kuchagua baina ya vyanzo vingi au vifo vingi

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa na viongozi wengine wa Serikali na pamoja na uongozi wa hospitali ya Taifa Muhimbili alipotembela hospitali hiyo kuhakikisha huduma za maji ndani ya hospitali hiyo.

Licha ya rasilimali maji iliyopo nchini kukadiriwa kufikia mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama imeendelea kuwa changamoto katika maeneo mengi nchini, huku baadhi ya maeneo yakipata huduma hiyo kwa mgawo na maeneo ya vijijini wakitegemea vyanzo vya asili visivyo salama.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Maji, rasilimali ya maji juu ya ardhi inakadiriwa kuwa na mita za ujazo bilioni 105, wakati iliyopo ardhini ni mita za ujazo bilioni 21 na mahitaji ya maji kwa matumizi mbalimbali nchini kufikia Aprili, 2022 yalikadiriwa kuwa ni mita za ujazo bilioni 47 kwa mwaka, sawa na asilimia 37.37 ya maji yaliyopo nchini, ikimaanisha kuwa asilimia 62 ya rasilimali maji iliyopo nchini haijatumika.

Mgawo wa maji ulisababishwa na kupungua kwa kina cha maji kwa baadhi ya maeneo ya nchi; ikiwamo Dar es Salaam ambao umekuwa ukitegemea chanzo cha Mto Ruvu, umetoa somo kwa Serikali na wadau wengine wa sekta ya maji kuangalia vyanzo vingine ili kuacha kutegema chanzo cha aina moja.

Maji yanaendelea kuwa rasilimali na hitaji la msingi la maisha ya binadamu ambapo kutokupatikana kwake kwa uhakika kunadhorotesha uchumi, kunaweka hatarini afya ya jamii ambayo ndiyo injini ya ujenzi wa taifa lolote lile.

Inaelezwa kuwa nusu ya vituo vya afya hapa nchini havina maji ya uhakika jambo linalosababisha wauguzi kushindwa kuwahudumia akina mama wajawazito kujifungua vyema.

Takwimu za hivi karibuni za Sensa ya Watu na Makazi zinaonyesha kuwa Tanzania ina watu wapatao milioni 61.74 (ongezeko la asilimia 34) kutoka watu milioni 44 mwaka 2012 huku idadi vituo vya kutolea huduma za afya ikiongezeka kufikia 10,067 mwaka 2022 kutoka 6,663 mwaka 2012.

Ongezeko hilo la watu na vituo vya afya kunaleta tafsiri ya kuongezeka kwa mzigo mkubwa kwa Serikali wa kutoa huduma za afya bora kwa watu wake katika kipindi ambacho tayari nchi haina uhakika wa upatikanaji na utoshelevu wa maji kwa baadhi ya maeneo ikizingatiwa maji ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika utoaji huduma bora za afya.

Licha ya haya yanaoendelea kuhusu uhakika wa upatikanaji wa rasilimali maji, Serikali haijalala, inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha upatikanaji na utoshelevu wa maji ni wa uhakika kwa ajili ya Watanzania wote wawapo katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Kuthibitisha hilo, Waziri mwenye dhamana ya maji nchini, Juma Aweso alikutana na uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kueleza mikakati ambayo Serikali inayo katika kumaliza shida ya maji katika hospitali hiyo.

Katika ziara yake hiyo, alisema kuwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga aweze kuhakikisha fedha inapatikana ya ununuaji wa tanki kubwa litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni moja ili kuhakikisha huduma ya maji inakua ya uhakika.

Waziri Aweso alisema kuwa Dawasa wanajipanga kutoa tanki la lita 18,000 na huku lingine la lita 10,000 litakalotokea Arusha yataifanya hospitali hiyo kuwa na akiba ya maji ya lita 28,000 pale kunapotokea shida ya maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi akiwasilisha jambo kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na ujumbe wake

“Lazima tuwe na altenative source (chanzo mbadala) tumekuja na watu wetu wa bonde kesho watu waanze survey (utafiti). Sisi suala la uchimbaji visima tumeshapata magari ya uchimbaji ya kisasa 25 ambayo Mheshimiwa Rais atatukabidhi hivi karibuni na hatutasubiri kukabidhiwa baadhi ya magari hayo yaanze kutumika kuchimba visima hapa Muhimbili,” anaeleza Waziri Aweso.

Aidha aliielekeza Dawasa waweze kuboresha mfumo wa maji yanayoingia hospitalini hapo na Bodi ya Bonde la Wami/Ruvu waweze kufanya tafiti na kuchimba kisima kitakachokuwa suluhu ya kudumu ya upatikanaji wa maji katika hospitali hiyo.

Katika hatua nyingine, akitoa taarifa ya upatikanaji wa maji hospitalini hapo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi alieleza umuhimu wa kuwa na akiba ya maji ndani ya hospitali zote nchini ili kuepusha usumbufu wowote kwa huduma za tiba kwa Wananchi.

Mbali na hatua hizo, Serikali imeshatoa vibali kwa mamlaka za uchimbaji wa visima kuanza kuchimba visima kwa mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Pwani.

Serikali inamalizia ujenzi wa mradi wa maji wa Kidunda ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu, unaokwenda kunufaisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

“Serikali inatambua kuwa mradi huu wa Kigamboni ni wa kupunguza makali tu, lakini suluhisho la uhakika la changamoto ya maji katika jiji la Dar es Salaam ni Bwawa la Kidunda,” alisema Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara yake ya kuzindua rasmi mradi wa wa maji wa Kidunda, Kigamboni.

Kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu aliiagiza Bodi ya Bonde la Ruvu kuvifufua visima 197 vilivyokuwa havifanyi kazi ili kukabiliana na tatizo la maji nchini.

Pia, inaendelea na ukaguzi wa vyanzo vya maji ili kuona kama vina akiba toshelevu katika kipindi hiki cha ukame. Kwa upande mwingine, imelazimika kusitisha vibali 12 vya watumiaji maji ili kupunguza matumizi ya maji na kukabiliana na hali ya ukame iliyopo inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Serikali ya Tanzania haiko peke yake katika hili kwani Taasisi ya WaterAid imedhamiria kuendelea kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi muda wote katika kipindi hiki ambacho, pamoja na mambo mengine, mabadiliko ya tabianchi yameathiri vyanzo vya maji.

"Ni wakati muafaka kwa serikali kuweka kipaumbele katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na mipango ya kukabiliana na hali hiyo ili watu kumaliza changamoto iliyopo ya maji. Tunatoa wito kwa serikali na wadau wa sekta ya maji kuwekeza katika ubora wa maji na kutumia maji ya chini ya ardhi katika jiji la Dar Es Salaam badala ya kutegemea maji ya mvua ya msimu.

Mabadiliko ya hali ya hewa yamefika, na yanatuathiri sisi sote. Iwe Dar Es Salaam au mkoa mwingine wowote nchini Tanzania, athari za mabadiliko ya hali ya hewa sasa ziko wazi.

Shirika la WaterAid Tanzania, litaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maji ili kuhakikisha kwamba tnaunga mkono kuongeza ufumbuzi wa maji yanayostahimili hali ya hewa ambayo yatamfikia kila mtu kila mahali kwa maji safi na salama bila kujali mabadiliko ya wingi wa mvua,” anasema Anna Tenga Mzinga, Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania.

Kuna mambo mengi ya kufanya ili kupunguza changamoto ya maji hususan katika vituo vya afya ambayo kama hayatashughulikiwa leo yatakuwa na madhara makubwa kwa kizazi kijacho.