Nida inavyoibeba dhana ya ‘utambulisho kwa wote’ mabegani

Wananchi waliojitokeza katika Ofisi ya Usajili ya Wilaya ya Ilala, Siku ya Utambulisho wa Taifa wakiwa wameshika nembo ya ID Day wakiwa na Msemaji wa NIDA, Geofrey Tengeneza (mwenye fulana ya bluu, wa tatu kulia) na maofisa wengine wa NIDA ikiwa ni ishara ya kuadhimisha siku hiyo.

Kila ifikapo Septemba 16, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Utambulisho. Siku hii ni maalumu kwa ajili ya kukuza uelewa kuhusiana na umuhimu wa kuwa na utambulisho wa rasmi kwa watu wote.

Siku hii ambayo haipewi uzito sawa na maadhimisho mengine, ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (lengo na 16.9) ya kuona kuwa mpaka 2030 watu wote wanakuwa na utambulisho rasmi, ikiwamo vyeti vya kuzaliwa.

Barani Afrika, historia inaonyesha Tanzania haikuwa na utambulisho rasmi kwa miongo mingi iliyopita, isipokuwa kwa baadhi ya nchi kama Kenya, kwa ukanda wa Afrika Mashariki, ambayo baada ya ukoloni kukoma bado ilikuwa na utaratibu wa utambulisho kwa kutumia vipande vya chuma vilivyokuwa vinavaliwa shingoni kwa ajili ya kutambuliwa.

Kutokana na kutokuwapo kwa uwiano sawa baina ya walio na utambulisho rasmi na wale wenye utambulisho rasmi hususan barani Afrika, Shirika lisilo la Kiserikali, ID4Africa liliundwa mwaka 2014 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo. Bahati iliyoje, mkutano wa kwanza wa shirika hilo ulifanyikia Tanzania, mwaka 2015 chini ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Harakati hizo hazikuishia hapo kwa kuwa maazimio yalikuwa ni kuzipeleka katika nchi mbalimbali na hivyo zilihamia Rwanda, Afrika Kusini, Namibia na ilipofika mwaka 2018, pale Abuja, Nigeria wazo la kuwa na Siku ya Kimataifa ya Utambulisho duniani lilipitishwa. Iliamuliwa kuwa kila ifikapo Septemba 16, 2023 kuwe na maadhimisho ya siku hiyo.

Mkurugenzi wa Uzalishaji Vitambulisho wa NIDA na Balozi wa Shirika la ID4Africa, Edson Guyai anasema dhana ya utambulisho imepanuka zaidi kutoka kuwa yenye malengo ya kiusalama pekee kuwa pia nyenzo ya kuchochea na kuwezesha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Kuna tofauti baina ya utambulisho na vitambulisho. Utambulisho unakwenda zaidi ya kadi zinazotumika kama vitambulisho, kwa kuwa hapa tunaizungumzia siku ya utambulisho duniani. Ukiwa na namba tayari unatambulika bila ya hata kujali kama una kitambulisho,” anaeleza Guyai ambaye anasema kuwa utambulisho una misingi mikuu mitatu ambayo ni: ujumuishi (watu wote wawe na utambulisho); ulinzi (taarifa za watu zilindwe) na matumizi (kupata huduma mbalimbali kupitia utambulisho wako).

Ofisa wa NIDA akimchukua mwananchi alama za vidole kwa ajili ya utambulisho wake wa Taifa.



Guyai anasema NIDA inashiriki kwa mara ya kwanza katika maadhimisho ya siku hii kubwa na lengo likiwa kuunga mkono jitihada za kuendelea kuelimisha Watanzania kuhusiana na umuhimu wa kujiandikisha kwa ajili ya kupata utambulisho wa kisheria kwa kutoa taarifa sahihi. “Ni muhimu kwa Watanzania kujiandikisha na kutoa taarifa sahihi ili waweze kupata utambulisho wao watakaoweza kuutumia sehemu mbalimbali.”

Anasema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa watu wanaohitaji utambulisho rasmi na watoa huduma kwa kufuata misingi ya mahitaji ya teknolojia ya sasa, ambayo inafanya kazi kulinda taarifa za mtu/mteja kudukuliwa au kutumika bila ya idhini yake na mtoa huduma wakati huo huo kumsaidia mtoa huduma kuthibitisha uhalali na usahihi wa taarifa za wateja wao kudhibiti mianya ya ulaghai au uhalifu. “Haya yote yanafanyika, tukiunga mkono lengo la pili ya siku hiyo la kutoa elimu juu ya matumizi sahihi na ya sasa ya utambulisho wako.”

Guyai anasema pia siku hiyo inasisitiza kuwa na mfumo mmoja wa utambulisho ambao utakuwa ukitumika katika maeneo mbalimbali nchini. Anasema matarajio yao ni kuona kuwa kitambulisho cha Taifa kinatumika kuchukulia pasi ya kusafiria (uhamiaji), kufungulia akaunti (benki), kuchukulia Visa (ubalozini), kuombea leseni ya udereva (polisi) na maeneo mengine mengi bila ya kubeba lundo la vitambulisho vingine kwa wakati mmoja.

“Kwa kuwa Serikali ni moja kuwekeza katika mifumo ya utambulisho mbalimbali ni gharama kubwa kwake, hivyo kuwa na mfumo mmoja wa utambulisho utaokoa fedha na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi za Serikali,” anaeleza Guyai huku akikiri kuwa litakuwa na ahueni kubwa ukizingatia tayari tunaelekea katika kuwa na bima ya afya kwa wote.


Utendaji kazi wa NIDA

Kisheria, NIDA ndiyo iliyokasimiwa jukumu la kusajili, kutoa vitambulisho na kutunza kanzidata ya taarifa za watu hapa nchini. Anasema wakati taasisi hiyo ikianza kutekeleza majukumu yake ilikuta bado mazingira si rafiki ikihusisha kutokukamilika kwa usajili wa vizazi na vifo, usajili wa watu katika daftari la makazi kuchukua muda mrefu sambamba na uhakiki wa usahihi wa taarifa zilizotolewa, kiasi cha kusababisha uzalishaji wa vitambulisho kwenda kwa awamu na kuchelewa kwake katika uzalishaji wa vitambulisho hivyo. “Wananchi waelewe kuwa vitambulisho havikuchelewa bila sababu ya msingi na tulichokuwa tunafanya ni kutengeneza kwanza msingi mzuri wa kanzidata ya NIDA ili kurahisisha uchakataji wa taarifa na uzalishaji wa vitambulisho.”

Anasema kuwa ofisi za wilaya za NIDA mara nyingi zimeonekana kuelemewa na idadi kubwa ya watu wanaotaka vitambulisho na ni kwa sababu watu wengi hupendelea kusubiria mpaka siku za mwisho wa zoezi na kufanya mamlaka ionekane imezidiwa uwezo wa kuwahudumia, akidai jambo hili kuchangiwa na uelewa mdogo wa watu kuwa na utambulisho, endapo wangekuwa nao, pengine idadi isingekuwa kubwa kama ilivyo.

Mpaka sasa NIDA imeshasajili watu takriban milioni 24.1, huku namba za usajili zilizotolewa zikifikia milioni 20.1 na vitambulisho vilivyozalishwa ni takriban milioni 13.8. Watu ambao wamepata vitambulisho mpaka sasa ni asilimia 67.5 huku wale ambao hawajapata wakiwa asilimia 32 ambao mpaka kufika Januari 2024, watakuwa wameshapatiwa wote. Pia, anasisitiza kuwa kutokuwa na kadi hakuwafanyi watu hao kushindwa kupatiwa huduma yoyote ile kwa sasa.

Tanzania ni nchi iliyo mbele katika matumizi ya teknolojia katika usajili na utambulisho wa watu barani Afrika huku nchi za Uganda, Kenya na Rwanda kwa ukanda wa Afrika Mashariki, zilijifunza kwetu. Guyai anasema ukweli ambao hausemwi ni kwamba Tanzania ndiyo nchi ya kwanza barani Afrika kufanya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole kwa kutumia kanzidata ya Vitambulisho vya Taifa.


Tunakoelekea

Anasema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kuwa watoto wasajiliwe na kutambuliwa tangu wanapozaliwa, hiyo ni hatua nzuri zaidi kwani inakwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya kuona utambulisho unakuwa jumuishi kinyume na hapo awali ambapo watu wenye umri wa kuanzia miaka 18 pekee ndiyo walikuwa wanakidhi sifa. Guyai anasema ili kufanikisha hilo sheria inahitaji kufanyiwa marekebisho ya kushusha umri wa mtu kusajiliwa iwe chini ya miaka 18.

Katika miaka inayokuja, kupitia mfumo mmoja wa utambulisho, tunakwenda kuwa na utambulisho wa kidijitali ambao hautahitaji kuwa na kadi ngumu. Mfumo huo, anasema, utaunganishwa na mifumo ya ku-scan misimbo kupitia simu au kompyuta ili kufanya uhakiki wa utambulisho.

Pia, NIDA inaangalia uwezekano wa kuongeza teknolojia katika usajili kutoka katika kutumia alama za vidole (fingerprint) pekee na kutumia usajili wa kutumia uso (facial recognition) au macho (iris recognition) ili kuwapa fursa wale ambao alama zao za vidole zimeharibika, kuweza kusajiliwa na kutambuliwa.


Rai

Kwa upande wake, Meneja wa Uzalishaji Vitambulisho wa NIDA na Naibu Balozi wa ID4Africa, Brenda Kileo anatoa rai kwa wale ambao bado hawajajisajiri, wafanye hima kwani ofisi ziko wazi. “Wanapokuja kujisajili, tunawaomba waje wakiwa na nyaraka halali zitakazotoa taarifa sahihi kwa ajili ya utambulisho wao.