Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mirerani inavyorahisisha shughuli za uchimbaji

Ofisi ya Afisa Madini Mkazi (RMO) Mirerani inayohudumia Wilaya ya Simanjiro inafanya shughuli zake ambapo madini yanayopatikana ni Tanzanite, Graphite, Marble, Green Garnet, Ruby, Rhodolite, Tourmaline, Limestone, Magnesite na Feldspar.
Afisa Madini Mkazi (RMO) wa Mkoa wa kimadini wa Mirerani, Mhandisi Menard Msengi anasema ofisi yake ina jumla ya wafanyakazi 28 wa kudumu wa kada za uhandisi migodi, jiolojia, mazingira, jiomolojia, mifumo ya kompyuta, umeme, uhasibu na watumishi saba ambao ni wa mikataba ambao kazi zao kuu ni wakaguzi wasaidizi wa madini.
RMO Msengi anasema shughuli za uchimbaji kwenye ukuta zinaongozwa na kanuni maalum na zinazosimamiwa na kamati tendaji ya eneo tengefu la ukuta (MCA) ambalo lina wajumbe wa taasisi mbalimbali na Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro na Katibu ni afisa madini mkazi.
Amewataja wajumbe wa kamati hiyo ni taasisi za jeshi la polisi, ofisi ya usalama wa Taifa, uhamiaji, Takukuru, ofisa tarafa, ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, mwakilishi wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani na viongozi wa vijiji vinavyozunguka eneo la machimbo.
RMO Msengi anasema ofisi hiyo imefanikisha makusanyo ya Sh 2.6 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 sawa na asilimia 52.23 ya malengo waliyowekewa.
Ametaja baadhi ya sababu zilizochangia wasifikie malengo ni shughuli za kijiolojia mashapo kuwa katika kina kirefu hivyo migodi mingi kutumia muda mrefu kufanya utanuzi na uwekezaji mdogo.
“Pia ukosefu wa teknolojia za kisasa kwa wachimbaji wadogo, mvua ziliathiri miundombinu ya uchimbaji na usafirishaji madini ujenzi, ukosefu wa miundombinu ya umeme kwenye baadhi ya machimbo ya vito,” anasema RMO Mhandisi Msengi.
Anataja mikakati waliyonayo ni kuongeza vituo vya madini ujenzi, kulingana na jiografia ya Wilaya ya Simanjiro, utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara wa madini wasio rasmi ili waweze kukata leseni, kufuatilia na kusimamia kwa kina miradi ya ujenzi wa viwanda vya madini ya kinywe.
“Pia tunaendelea kutoa elimu zaidi kwa wachimbaji ili kuweza kupunguza ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini,” anasema RMO Mhandisi Msengi.
Anasema soko la madini linaendelea vizuri na kuna wafanyabiashara wakubwa (Dealers) 27 mpaka sasa na pia ujenzi wa soko litakalotumika kuwahudumia wafanyabiasha wa madini ya Tanzanite unaendelea chini ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Anasema kazi za uchimbaji madini zinazofanyika katika eneo tengefu la machimbo ya madini ya Tanzanite, lina ulinzi wa kutosha muda wote ambapo pia kuna taa na kamera zinazofanya kazi muda wa saa 24.
“Eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite limegawanyika katika vitalu mbalimbali ikiwemo kitalu A na C ambalo ni eneo la wachimbaji wakubwa na kitalu B na D ni eneo la wachimbaji wadogo,” anasema RMO Mhandisi Msengi.
Anasema eneo la kitalu C, linalomilikiwa na mwekezaji kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, linaendelea vyema na shughuli za uchimbaji madini.
Anasema udhibiti wa madini kwenye machimbo ya Tanzanite huanzia migodini chini ambapo kunakuwa na wadhibiti wa madini wa Serikali na wadhibiti wa mwenye mgodi, wadhibiti wa mwekezaji na wachimbaji wenyewe.
“Madini hukusanywa na kuwekwa kwenye mfuko na baadaye hufungwa lakiri ya Serikali pamoja na ya mwenye mgodi kisha hupandishwa juu,” anasema RMO Mhandisi Msengi.
Anasema madini yanapofika juu hupokelewa na afisa wa Tume ya Madini akishuhudiwa na maofisa wa vyombo vyote vya usalama na mamlaka ya mapato nchi ni (TRA), madini hupimwa na kurekodiwa na baadaye hufungwa tena lakiri.
“Baada ya hapo madini hayo huletwa kwenye jengo la kituo cha Tanzanite Magufuli kwa ajili ya kufanyiwa uthaminishaji unaofanywa ana maofisa wataalamu wa ofisi ya madini wakishuhudiwa na vyombo vyote vya usalama,” anasema RMO Mhandisi Msengi.
Anasema baada ya hapo mteja hulipa stahiki za Serikali na baadaye hupewa kibali cha kupeleka madini hayo sokoni na sokoni madini hupokelewa na afisa wa Tume ya Madini na kurekodiwa na baadaye mteja huruhusiwa kuuza madini yake kwa wafanyabiashara wakubwa walipo sokoni (Dealers).
“Shughuli zote za madini zinamalizika soko la madini ambapo pale kuna wafanyabiashara wakubwa wa madini (Dealers), wachimbaji na wafanyabiashara wa kati (brokers) hufanya biashara zao za kuuza madini hayo na Dealers husafirisha madini hayo nje ya nchi baada ya kupata vibali husika,” anasema RMO Mhandisi Msengi.
Anasema kwa sasa changamoto mbalimbali zilizopo kwenye maeneo ya machimbo ni pamoja na ukosefu wa huduma za kijamii, maji safi na salama, umeme, mawasiliano na huduma za afya.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar atembelea ujenzi wa soko la madini
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma ametembelea soko la madini ya Tanzanite linalojengwa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara na kusema kuwa litazidi kuitangaza Tanzania na kuvutia watalii zaidi.
Mgeni ameyasema hayo baada ya kutembelea soko la madini ya Tanzanite linalojengwa mji mdogo wa Mirerani, akiwa na Mawaziri watatu na manaibu mawaziri watano na wajumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar.
Anasema ujenzi wa soko hilo utaitangaza zaidi Tanzania kupitia madini ya Tanzanite kwani wale waliokuwa na dhana potofu kuwa madini hayo yanapatikana nje ya Tanzania wataelewa.
“Tumeambiwa Tanzanite ni madini pekee duniani yanayopatikana Tanzania hivyo soko hilo la madini hayo litakapokamilika hapa Mirerani litaongeza sifa ya nchi na zaidi kuitangaza Tanzania kimataifa," anasema Mgeni.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga anasema ujenzi wa soko hilo umefikia asilmia 65 ili jengo likamilike na wanatarajia hadi mwezi Oktoba mwaka 2023 litamalizika.
"Tunatarajia jengo la soko la madini kukamilika kwenye kilele cha mbio za mwenge wa uhuru ambao kwa mwaka huu 2023 zitahitimishwa hapa kwetu Mkoani Manyara," anasema Sendiga.
Pia, ameishuku Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyofanikisha miradi mingi mikubwa na midogo mkoani Manyara.
Mhandisi wa ujenzi wa soko hilo la madini Goodluck Masika anasema walianza shughuli za ujenzi Mei 22 mwaka 2022 na wanatarajia kukamilisha mwezi Oktoba mwaka 2023.
Mhandisi Masika anasema mradi wa soko hilo unatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa thamani ya Sh5.49 bilioni chini ya mshauri chuo cha ufundi Arusha.
Afisa madini mkazi (RMO) Mirerani, Mhandisi Menard Msengi anasema kukamilika kwa soko hilo kutaongeza tija kwenye mnyororo wa thamani ya madini ya Tanzanite.
“Soko la madini ya Tanzanite linaendelea vyema hiyvo likikamilika litaanza kazi mara moja kwani tunatekeleza agizo la Serikali la kuwepo na soko la madini ya Tanzanite mahali madini haya yanapochimbwa,” anasema Mhandisi Msengi.
Julai 7 mwaka 2021, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa mji mdogo wa Mirerani, aliagiza kwa kutoa miezi mitatu, shughuli za uuzaji na uongezaji thamani wa madini ya Tanzanite zifanyike Mirerani na soko lijengwe.