Puma Energy kinara wa uhifadhi na usambazaji mafuta ya ndege nchini

Kuna mambo mengi hufanyika nyuma ya pazia kabla ya kuiona ndege ikipaa, baadaye kutokomea mawinguni, hadi kutua salama sal­min.

Achilia nafasi ya rubani, kama ndege inatumia mafuta yasiyo na viwango vya ubora vinavyohitajika kimataifa, basi usalama wa abiria, mizigo na rubani uko shakani na ndege hiyo huenda isipae vyema huko angani.

Inawezekana matukio ya ajali za ndege yanayosababishwa na matu­mizi ya mafuta duni ni mengi lakini hayazungumzwi pengine kuliko yale ya ajali zinazosababishwa na uzembe au hali ye hewa.

Lakini kwa nini tuendelee kufikiria ajali za ndege, wakati tayari tuna mtoa huduma aliyebeba dhamana hii kwa ajili ya Watanzania na wageni wote wanaoingia na kutoka nchini?

Tunamzungumzia Puma Energy ambaye amejipambanua kwa uuza­ji na uhifadhi wa mafuta ya ndege yenye ubora na viwango vya kima­taifa nchini.

Kampuni hiyo ambayo ni kongwe nchini ambayo imehodhi asilimia 50 ya hisa na ubia Serikali, huku nusu nyingine zikiwa chini ya Serikali. Kampuni hii ilianza shughuli zake Tanzania mwaka 2011.

Puma ndiyo mwekezaji mwenye hisa nyingi katika shughuli za uen­deshaji na usambazaji wa mafuta ya ndege nchini.

Meneja Uendeshaji wa Huduma za Usafiri wa Anga wa Puma Energy Tanzania, Benjamin Masige ame­sema kuwa kampuni hiyo inaingiza mafuta ya ndege nchini kupitia taa­sisi ya Serikali ya uingizaji mafuta nchini kama ilivyo kwa wadau wen­gine wa sekta hiyo.

Amesema kampuni hiyo ina hifa­dhi kubwa jijini Dar es Salaam ya kusambaza na kuhifadhi mafuta ya ndege. “Tunaweza kusambaza mafu­ta kwa kutumia magari kutoka katika hifadhi yetu iliyopo Kurasini hadi hapa uwanja wa JNIA, na maeneo mengine tunayoyasambaza ikiwamo; viwanja vya ndege KIA, Mwanza, Arusha, Tabora, Dodoma, Songwe, na Zanzibar.”

Katika eneo la utunzaji wa bidhaa hiyo, Masige amesema kunahitajika uwekezaji mkubwa wa vifaa, ujuzi, wataalamu na fedha kwa pamoja kuhifadhi vile inavyotakiwa.

Hii si biashara ambayo kila mtu anaweza ifanya kutokana na mahi­taji yake na usimamizi wake mkubwa,ambao husimamiwa kwa viwango vya kimataifa kwa umakini.”Ni kazi ambayo inahitaji umakini kwenye kuyapokea, kuyahi­fadhi na kuyasambaza,” ameongeza Masige.

Ameeleza kuwa hata usafirishaji wake kutoka aina moja ya usafiri kwenda nyingine, husimamiwa na viwango vilivyowekwa kimataifa na taasisi ya ukaguzi duniani (JIG). Amesema kuwa JIG ndiyo wasimam­izi wakuu wa upokeaji, utunzaji na usambazaji wa mafuta ya ndege duniani.

Si JIG pekee ndiyo inayokagua shu­ghuli za Puma Energy Tanzania, bali ipo taasisi nyingine kubwa inayosi­mamia maslahi ya kampuni zote za ndege ya (IATA Fuel Quality Pool – IFQP) iliyo chini ya IATA.

Amesema IFQP ina jukumu la kukagua na kufanya uchunguzi wa kampuni zote zinazojihusisha na uendeshaji wa huduma za mafuta ya ndege katika viwanja vya ndege vya kimataifa.

“Kuna kampuni za ndege zaidi ya 300 ambazo zinapata huduma ya ukaguzi kutoka IFQP. Kwa mfano kampuni ya ndege ya Delta Airline inapotaka kufanya safari za kuja nchini Tanzania, haihitaji kutuma mtu kuja Dar es Salaam, wataingia katika mfumo wa IFQP na kuona mtoa huduma za mafuta ni nani na amekidhi viwango kwa hatua gani.”

Hapa nchini, Puma Energy ina leseni ya biashara kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na ithibati za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kwa viwanja vya Tanzania bara, KADCO (Kilimanjaro) na ZAA (Zanzibar) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Mafuta ya ndege

Amesema mafuta ya ndege ni mafuta yanayotokana na chanzo kimoja cha mafuta (crude) ikiwamo petroli, dizeli, mafuta ya taa, gesi, mafuta mazito na lami nk.

Ameongeza kuwa mafuta ya ndege yana tabia zake tofauti kutokana na yanavyotunzwa na kusimamiwa.

Utunzaji wake unahitaji umakini wa hali ya juu kwa kuwa yana uwezo wa kubadirika na kuleta athari katika mitambo yakikosewa katika utunzaji wake.

“Kwa nini umakini wa hali ya juu unahitajika ni kwa sababu ya usal­ama na utendaji kazi wa injini za ndege kwa kuwa tunafahamu ndege ikishapaa haisimami mahali popote huko angani mpaka inapotua hivyo hautakiwa kuathiri utendaji kwa aina yoyote ile.”

Kampuni zinazohudumiwa

Masige amesema Puma Energy inahudumia makampuni yote makub­wa ya ndege zinazofanya safari zake hapa nchini na zile za hapa nyum­bani. Huduma zinazotolewa ni sawa kwa kampuni zote.

Akijibu swali la ujazo wa lita za mafuta ya ndege zinazoweza kuingia katika ndege moja, Masige amesema ndege hutofautiana ujazo wa mafuta kulingana na vigezo vingi, ikiwepo aina ya ndege, urefu wa safari, lakini katika uhalisia wa ujazo wa ndege moja ikiwa haina kitu, zipo zenye kuchukua lita 1000 mpaka 180,000 za ujazo wa mafuta, kulingana pia na aina ya ndege.

Mafanikio

Katika yale ya kujivunia, Masige amesema kama kampuni inayo mam­bo kadhaa inayoyaona kama mafani­kio katika eneo hilo la biashara ya mafuta ya ndege.

Kwanza, amesema ni uwezo wao wa kusambaza mafuta usio na kikomo kutokana na mtandao wake mpana wa mafuta. Kampuni hiyo ipo katika viwanja vingi hapa nchini na duniani kwa ujumla hii ikimaanisha ni kampuni inayotegemewa katika huduma ya mafuta ya ndege.

Pili, ni watoa huduma wa mafuta ya ndege yaliyo katika mazingira salama, safi, na yasiyo na shaka sam­bamba na kupata huduma ndani ya muda mfupi na kwa kiwango cha hali ya juu.

Tatu, uwekezaji wake katika kue­ndesha shughuli zake kidijitali ni jambo lingine la kujivunia. Amese­ma wanaondokana na utaratibu wa makaratasi kwa kutumia vifaa vya kidijitali (tablets) kujaza mafuta, ikiwa ni sehemu pia ya utunzaji wa mazingira kwa kuokoa misitu yetu kwenye uzalishaji wa karatasi.

Funzo la ajali ya Precision Air

Amesema hawezi kutolea ufa­fanuzi tukio la ajali lakini wanalichu­kua kama funzo kwa kuwa uende­shaji wa biashara ya mafuta ya ndege yanahitaji uzingatiaji wa viwango na usalama wa hali ya juu.

“Ajali si tukio tunaloliombea au kulipenda lakini ni funzo kati­ka kuhakikisha usalama wa ndege tunazozihudumia mafuta, kuhakiki­sha kila siku tuna toa huduma zetu tukijua usalama wa chombo na abiria wake, ni msingi mkuu wa uthabiti wa maarifa yetu katika kuhakikisha wanaruka na kutua salama.”

Amesema wanajitahidi kuendelea kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kulingana na matakwa ya mam­laka zinazowasimamia na ndiyo maa­na wanaendelea kuaminika katika soko la sekta ya huduma za mafuta kwenye viwanja vya ndege.

Uhusiano wake na Serikali

Masige anakiri kuwa kampuni hiyo imeendelea kufanya biashara katika misingi halali kiasi cha kuweza kulipa kodi zinazostahili za Serikali.

“Sisi pia tunalipa gawio kwa Seri­kali kama sehemu ya uwekezaji wake katika kampuni.”

Pia amesema huwa wanalipa kodi zinazohusiana na ajira kwa mamla­ka husika ambapo makusanyo hayo yanakwenda kusaidia maendeleo ya sekta husika moja kwa moja.

Miradi ya kijamii

Katika eneo la ushiriki wa miradi ya kijamii, amesema kuwa kampuni imekuwa ikishiriki katika kampeni ya kuboresha elimu ya usalama baraba­rani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini.

Pia, kampuni imekuwa ikiendesha program ya kukuza uelewa kwa wana­funzi wa shule mbalimbali kuhusiana na elimu ya usalama barabarani.

Wito

Amesema wanawashukuru wateja wao wote kwa kuwawezesha kufika hapo na wanawaomba waendelee kufanya biashara vizuri.