Rais Mwinyi aipongeza REPOA kufanya utafiti kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi akitoa hotuba katika ufunguzi wa warsha ya 26 ya mwaka ya Utafiti ya REPOA iliyofanyika Novemba 2-3 2022 Zanzibar. Picha na maktaba

Muktasari:

Ni kama vile dunia bado haijapata mwarobaini wa janga la mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa kila uchwao linaendelea kuleta athari katika kila nyanja ya maisha ya viumbe hai wote ulimwenguni.

Ni kama vile dunia bado haijapata mwarobaini wa janga la mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa kila uchwao linaendelea kuleta athari katika kila nyanja ya maisha ya viumbe hai wote ulimwenguni.

Je, changamoto hii unayoonekana kuwa haiwezi kutatulika bado ituweke katika usingizi mzito?

Ni swali ambalo limejibiwa vyemma na Taasisi ya Utafiti na Sera (REPOA) kwa namna ya kipekee kupitia Warsha ya 26 ya Utafiti na Sera iliyofanyika visiwani Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Benki ya CRDB.

Katika warsha hiyo iliyobeba kauli mbiu isemayo; “Kuhuisha biashara na mabadiliko ya tabianchi kwa ukuaji shindani katika uchumi wa kijamii Tanzania,” ilifanyika kwa siku mbili kuanzia Novemba 2 hadi 3.

Warsha hiyo iliwakutanisha watafiti, wachumi, watunga sera na wataalamu wengine wenye uzoefu katika nyanja tofauti na kuangalia namna ya kukuza uwezo wa tafiti na sera katika kukabilia athari za mabadiliko ya tabianchi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi alikuwa mgeni rasmi wa warsha hiyo.

Rais Mwinyi amepongeza hatua iliyofikiwa na REPOA na Benki ya CRDB katika malengo yao ya pamoja na nia ya kusaidia biashara endelevu, maendeleo ya sekta binafsi na ukuaji wa uchumi.

Kama Serikali, tunahitaji ushahidi wa kitafiti ili kufahamisha michakato yetu ya kutunga sera. Matarajio yetu ni kukuza kizazi na matumizi ya maarifa ambayo yanachangia kuboresha maisha ya watu na kukuza uchumi wa Taifa letu," alisema Rais Mwinyi.

Dk. Mwinyi aliridhishwa na kaulimbiu ya warsha hiyo na anakiri kwamba inaunga mkono ajenda za maendeleo za Serikali ya Muungano na ya Zanzibar kwa sababu kukuza biashara na uwekezaji ni lengo lao la msingi.

Tangu REPOA ianze shughuli zake mwaka 1995, imekuwa ikiandaa warsha kila mwaka ambazo zinahusisha wadau mbalimbali ikiwemo watunga sera na watafiti pamoja na kutoa nafasi ya mitandao ya mijadala miongoni mwa wadau.

Sehemu ya washiriki katika Warsha ya 26 ya Mwaka ya Utafiti iliyohitimishwa hivi karibuni kama inavyoonekana wakati wa ufunguzi.

Hayo yanawezekana kutokana na ubora na uadilifu wa utafiti na juhudi mbalimbali za kusambaza matokeo kupitia machapisho, kushiriki shughuli mbalimbali za Serikali ambavyo vimezaa matokeo chanya vikiongozwa kiufundi na timu na kamati za kupitia na kuendeleza sera na mikakati.

“Sisi tunaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo katika harakati za kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa, kukuza uchumi kwa njia jumuishi iliyo bora na endelevu,” ameeleza Mkurugenzi Mtendaji wa REAPOA Dk Donald Mmari.

Kwa miaka 27 iliyopita, REPOA imewajengea uwezo na kunufaisha maelefu ya Watanzania, watafiti na wachambuzi kutoka seriklini, taasisi za elimu ya juu, Azaki na vyombo vya habari.

REPOA pia imesaidia watumiaji wa tafiti kuhusu uchambuzi wa sera na ujuzi wa utungaji wa sera zenye kutoa ushahidi.

Majadiliano ya wadau

Warsha iliwaleta wadau mbalimbali waliokuwa wakitoa masuluhisho ya njia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kukuza biashara, ushindani, uchumi wa nchi na sekta binafsi kupitia mijadala ya kisekta.

Katika mjadala wa “Uwezeshaji Biashara: Viwezeshi, Vikwazo na Njia za Kukabili” Antony Mveyange wa PASGR, ameiomba Benki ya CRDB kuwapa kipaumbele Watanzania waishio vijijini katika mkakati wa kujenga uchumi wa kijani.

Pia amesema wakati umefika Watanzania wafunguliwe waweze kujifunza masuala mbalimbali kutoka nchi nyingine, “Tunafanya tafiti nyingi na kufanya makongamano ya kimataifa hii ni nafasi ya wadau na Watanzania kwa ujumla ambao wanapenda utafiti na kujifunza maarifa mapya ambayo yamekuwa yakitolewa.”

Kwa upande wa Dk Idil Ires ambaye ni Mchumi wa Siasa amesema kuwa gharama za miamala zinazohusiana na taarifa, makubaliano zinafanya zao la mpunga kutokuchangia katika maendeleo ya biashara nchini.

Katika mjadala wa “Kuchangamkia fursa za ajira, fursa, Urasimishaji wa Rasilimali kwa Ukuaji wa Uchumi wa Kijani” mtafiti na mkufunzi wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Dk Lucy Ssend amesema kuwa ujenzi wa uchumi wa kijani utasaidia kutengeneza ajira nyingi zaidi.

“Tunapoamua kuelekea katika uchumi wa kijani maana yake ni kutengeneza mamilioni ya ajira kwa watu wetu, ni fursa.”

Kuhusu maeneo yanayoibuka ya utafiti, Mwanachama wa REPOA, Professa Samwel Wangwe amesema kuwa kunahitajika kuwapo kwa muundo ya kitaasisi ambao utaruhusu kila mdau kushiriki katika mabadiliko ya tabianchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela anasema CRDB ndiyo benki pekee iliyotambuliwa nchini kusimamia miradi inayozingatia maabdiliko ya tabianchi na kwamba imeandaa mradi wa kilimo utakaowanufaisha zaidi ya wakulima milioni sita nchini katika muktadha huo wa maabadiliko ya tabianchi.

Amesema mradi huo wa miaka mitano unaotegemewa kuzinduliwa hivi karibuni una jumla ya Dola za Marekani milioni 200 sawa na wastani wa Sh466 bilioni ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mradi huu utawagusa moja kwa moja wakulima 1.2 milioni na wafaidika wasio wa moja kwa moja milioni 4.9 mpaka programu inakwisha itakuwa imewagusa Watanzania 6.9 milioni,” anasema.

Mbali na hilo, anasema benki hiyo pia inasimamia miradi ya kilimo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 250 (Sh583 bilioni).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji, Ally Gugu wakati akifunga warsha hiyo amesema watatumia mapendekezo yote katika kuboresha sera za nchi na katika uzalishaji.

Mshauri na mchumi wa nchi, katika Ubalozi wa Norway, Olav Lundstol anasema Tanzania ikiwa nchi inayoendelea bado inahitaji nguvu kubwa kuongeza uzalishaji.

Mtaalamu wa tafiti wa REPOA, Dk Fadhili Ahmed Ali amesema uelewa, ujuzi na kutambua kuhusu mabadiliko ya tabaia nchi bado upo chini hivyo kama taifa ipo haja kuwekeza nguvu zaidi kuwasaidia wananchi na jamii.

Balozi wa Denmark Tanzania, Mette Nørgaard Dissing-Spandet na Balozi wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) Tanzania, Manfredo Fanti wanasema wataendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Manfredo anasema jambo kubwa ni kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano katika kuongeza uzalishaji wa kilimo na chakula.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Amour Hamil Bakar amesema kuna wanufaika 300 wakiwemo wakulima, wasindikaji, watu wa masoko na waagizaji bidhaa kutoka nje ambao wamenufaika moja kwa moja na kazi za REPOA visiwani humo. Pia, amesema watumishi 15 wa wizara hiyo wamepatiwa mafunzo ya utafiti, uchambuzi wa sera na uandishi wa taarifa za kitaalamu na wanaleta utofauti katika utendaji.

Rais Mwinyi aipongeza REPOA

Rais Mwinyi amesema kuwa Serikali yake inatamani kuona tafiti zenye kuleta matokeo chanya zitakazosaidia katika michakato ya uundaji wa sera katika Serikali ya Muungano na Zanzibar.

“Nawapongeza REPOA kwa kuunga mkono juhudi za Serikali yangu kwa kuendelea kufanya tafiti za kisera kwani hili ni jambo la msingi katika juhudi za kuelekea uchumu wa kisasa kupitia mikakati muhimu kama vile uchumi wa Buluu, viwanda na kilimo.”

Rais Mwinyi pia alizungumzia REPOA kuungana na kampuni kubwa katika sekta ya fedha, Benki ya CRDB katika kuandaa warsha hiyo, hivyo akatoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wenye tija na mahusiano ili kupata afua muhimu zaidi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Warsha hiyo pia ilishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya kimkakati kati ya REPOA na PASGR yenye lengo la kuongeza uwezo wa utafiti na sera ili kuchochea maendeleo barani Afrika.