Rais Ndayishimiye: Burundi imeipokea Benki ya CRDB

Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye akiagana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, baada ya kumaliza mazungumzo yao walipomtembelea kwenye makazi yake rasmi yaliyopo eneo la Kiriri, Bujumbura, Novemba 25, 2022. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay (wa tatu kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Hosea Kashimba (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Burundi, Fredrick Siwale (wapili kulia), Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwille (kulia), Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, Mjumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Kahumbya Bashige na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Burundi, Menard Bucumi.

Muktasari:

Rais wa Jamhuri ya Burundi, Eva­riste Ndayishimiye ameipongeza Benki ya CRDB Burundi kwa mafani­kio makubwa iliyopata katika kipindi cha miaka 10 ya uwepo wake nchi­ni humo na kusema kuwa Burundi imeipokea Benki ya CRDB kwa miko­no miwili na inajivunia uwepo wake katika Taifa hilo.

Bujumbura. Rais wa Jamhuri ya Burundi, Eva­riste Ndayishimiye ameipongeza Benki ya CRDB Burundi kwa mafani­kio makubwa iliyopata katika kipindi cha miaka 10 ya uwepo wake nchi­ni humo na kusema kuwa Burundi imeipokea Benki ya CRDB kwa miko­no miwili na inajivunia uwepo wake katika Taifa hilo.


Rais Ndayishimiye ametoa pongezi hizo katika mkutano na ujumbe wa Benki ya CRDB ulioongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliyeambatana na Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi ya kampuni Mama ya Benki ya CRDB pamoja na kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi.


Ujumbe huo umemtembelea Rais Ndayishimiye ikiwa ni mfululizo wa ziara zilizofanywa na viongozi waan­damizi wa Benki ya CRDB na Benki Kuu ya Burundi kutoa shukrani kwa Serikali na wadau mbalimbali ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika miaka 10 ya utoaji huduma za Benki ya CRDB Burundi.


Akizungumza katika mkutano huo, Rais Ndayishimiye amesema Tanzania na Burundi ni ndugu wa karibu sana na hata mipaka iliyopo ni matokeo ya historia ya ukoloni lakini mipaka hiyo kamwe haiwezi kuwa kikwazo cha mahusiano mazuri kati ya nchi hizo mbili zenye historia kub­wa ya ushirikiano.

Rais wa Jamhuri ya Burundi, Évariste Ndayishimiye akiwa kwenye mazungumzo na ujumbe wa Benki ya CRDB, ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Ally Laay na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati walipomtembelea kwenye makazi yake rasmi yaliyopo eneo la Kiriri, Bujumbura, Novemba 25, 2022.

“Tunashukuru kuwa Tanzania ilishiriki kwa kiasi kikubwa sana katika kupatikana kwa amani nchini Burundi na sasa mnakuja tufanye maendeleo kwa pamoja kwa manu­faa ya nchi zetu lakini pia Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki” alisema Rais Ndayishimiye ambaye katika mkutano wa 22 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ulio­fanyika Julai 2022 alitangazwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais Ndayishimiye aliingia mada­rakani mnamo Juni 2020, ambapo katika kipindi chake Benki ya CRDB imeendelea kufanya vyema sokoni hadi kufikia kushika nafasi ya tatu kati ya benki kumi na tatu zinazotoa huduma za kibenki nchini Burundi. Katika kipindi hicho Benki imeweza kufungua matawi manne huku tawi la tano likitarajiwa kufunguliwa mapema mwaka 2023 katika makao makuu mapya ya nchi ya Burundi, Gitega.

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay (wa pili kushoto) akimkabidhi zawadi Waziri wa Fedha wa Burundi, Audace Niyonzima wakati ujumbe wa Benki ya CRDB ulipotembelea Burundi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya CRDB Burundi. Kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Hosea Kashimba.

“Tunawashuru sana kwa jitihada zenu ya kutoa elimu za fedha kwa Warundi ili wajifunze namna nzuri ya usimamizi wa fedha na kuweke­za lakini pia tungependa kushiriki­ana nanyi zaidi katika programu za vijana na wanawake ambao ni kipa­umbele chetu kikubwa kwa sasa,” aliongeza Rais Ndayishimiye.

Rais Ndayishimiye pia alituma salamu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alisema kuwa Rais Samia ni dada yake ambaye wanashirikiana vyema katika uongozi wao. Katika hatua nyingine, Rais Ndayishimiye alitoa wito kwa Benki ya CRDB Burundi kukaa pamoja na idara maalum inay­oshughulika na mipango mikakati ya Serikali ya Burundi ili kuweza kuan­galia maeneo ya kushirikiana zaidi.

Ujumbe wa Benki ya CRDB ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Dk Ally Laay (wa nne kulia) na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulmajid Nsekela (wa tatu kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Burundi, Desire Musharitse (wa tano kushoto) walipotembelea ofisi ya Naibu Gavana huyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya CRDB Burundi.

Waziri wa Fedha wa Burundi, Audace Niyonzima alisema Serikali ya Burundi imejidhatiti katika kush­irikiana na sekta binafsi kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa sekta binafsi ambapo kwa kuanzia Serikali imejipanga kufanya mageuzi ya kisera ili kuchochea biashara na ushirikiano na sekta binafsi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa tatu kushoto) akizungumza katika kikao cha ujumbe wa benki hiyo na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Burundi, Desire Musharitse (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara ya ujumbe wa Benki ya CRDB ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Dk Ally Laay (wa pili kushoto) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya CRDB Burundi.

“Tunatamani kuona mnaongeza ujumuishaji wa huduma za fedha kwa wananchi wa Burundi na Seri­kali ipo tayari kuendelea kutoa ush­irikiano katika eneo hilo na niendelee kuwaomba muongeze ushiriki wenu katika uwezeshaji kwenye sekta ya kilimo na viwanda” aliongeza Waziri Niyonzima.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Burundi, Desire Musharitse alisema Benki Kuu ya nchi hiyo inafurahia sana kwa uwepo wa Benki ya CRDB nchini Burundi kwani imekuwa seh­emu ya uwezeshaji wa miradi mingi ya kiuchumi kwa nchi lakini pia imechangia uwezeshaji wa wafan­yabiashara.

“Tulipata matatizo yaliyopelekea changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha za kigeni mwaka 2015 lakini tulipata msaada mkubwa sana kutoka Benki ya CRDB na hakika hilo limedhihirisha ule usemi wa rafiki wa kweli hujulikana wakati wa shi­da,” alisema Musharitse.

Wateja wa Benki ya CRDB Burundi wakijumuika katika hafla ya chakula cha usiku katika maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya CRDB Burundi.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulma­jid Nsekela ameishukuru Serikali ya Burundi kwa ushirikiano mkubwa kwa Benki ya CRDB Burundi ulio­pelekea kampuni tanzu hiyo kupata mafanikio makubwa ndani ya kipindi kifupi cha miaka 10. Sambamba na hilo Nsekela ameishukuru Serikali ya Rais Ndayishimiye kwa kuipatia eneo Benki ya CRDB Burundi katika makao makuu mapya ya nchi ya Gitega ili kufanikisha ujenzi wa tawi jipya.

“Nilipata bahati ya kushiriki katika mikutano yako pamoja na Rais Samia na niliona kiu yenu ya kuona ush­irikiano wa sekta binafsi za Tanza­nia na Burundi hivyo nikuahidi kuwa Benki ya CRDB itaendelea kuunga mkono jitihada zako za kukuza uchu­mi wa Burundi kwa manufaa ya watu wa Burundi lakini pia Tanzania na Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki” alisema Nsekela.

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay (wa kwanza kulia), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Hosea Kashimba (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Burundi, Fredrick Siwale (wa pili kushoto) na Waziri wa Fedha wa Burundi, Audace Niyonzima wakijumuika katika hafla ya chakula cha usiku pamoja na wateja wao katika maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya CRDB Burundi.

Aidha Nsekela alisema Benki ya CRDB inatarajia kuingia nchini DRC hivi karibuni ambapo inatara­jia kufungua matawi katika mikoa iliyo karibu na mpaka wa Burundi na DRC ili kuchochea biashara kati ya nchi hizo mbili ambazo ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tutajikita katika matumizi ya teknolojia ili kuweza kujumuisha Warundi wengi zaidi katika mfumo rasmi wa kifedha ambapo nafura­hi kuwa mpango wetu wa kutumia Wakala umeendelea kufanya vyema ambapo hadi hivi sasa tuna mawaka­la zaidi ya 600 wanaosaidia kutoa huduma kwa matawi yaliyopo,” aliongeza Nsekela.

Nsekela aliongeza kuwa uwezo wa Benki ya CRDB sambamba na washirika wake wa kibiashara unaipa nguvu kubwa benki katika kuweze­sha sekta mbalimbali ambapo hivi karibuni Benki imeweza kuingia makubaliano na mashirika makubwa ya fedha kama IFC, PROPARCO na INTESA ambapo kiasi cha Dola Mil­ioni 5 za Kimarekani zimeelekezwa katika kuwezesha biashara ndogo na kati nchini Burundi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni Mama ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay na yeye alitoa shukrani kwa Rais Ndayishimiye na Serikali yake kwa ushirikiano ulio­changia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Benki ya CRDB Burundi katika kipindi cha miaka 10 tangu kuingia katika soko la Burundi.

“Wakati tunafanya uamuzi wa kufungua biashara yetu nchini Burundi haikuwa rahisi kufikia uamuzi ule kwa kuwa ilikua ni mara ya kwanza tunafungua biashara nje ya nchi na maswali yalikua mengi juu ya uamuzi wa kuchagua Burundi laki­ni leo hii sote tunajivunia na kuona nchi zote mbili zinanufaika ambapo hapa Burundi tunalipa kodi na kutoa ajira lakini pia faida inayopatikana hapa inawanufaisha wanahisa wetu hadi Tanzania,” alisema Dk Laay.

Waziri wa Fedha wa Burundi, Audace Niyonzima (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay (wa kwanza kushoto) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela (wa tatu kushoto) wakicheza ngoma ya asili wakati wa hafla ya maadhimisho ya Benki ya CRDB Burundi.

Naye Mwenyekiti wa Benki ya CRDB Burundi, Hosea Kashimba ali­toa shukrani zake kwa Rais Nday­ishimiye na kusema kuwa mapinduzi makubwa ya uchumi yanaonekana nchini Burundi katika kipindi chake na moja ya sekta ambayo inafanya vizuri ni sekta ya ujenzi jambo linalo­ashiria imani kubwa ya wawekezaji kwa Serikali.

Kuhusu Benki ya CRDB Burundi

Benki ya CRDB Burundi ilianzish­wa nchini Burundi mnamo mwaka 2012 chini ya sheria ya makampu­ni nchini Burundi. Benki ya CRDB Burundi inatoa huduma kwa wateja wa taasisi na makampuni pamoja na wateja binafsi huku ikimilikiwa na kampuni Mama ya Benki ya CRDB kwa asilimia 100.

Benki ya CRDB Burundi inatoa huduma kupitia matawi manne sam­bamba na mawakala wa benki zaidi ya 600. Hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka 2022, Benki ya CRDB Burundi imetoa mikopo ya zaidi ya Faranga Bilioni 300 za Burundi kwa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda na utalii.

Maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya CRDB Burundi yameambatana na shughuli mbalimbali zenye lengo la kushukuru jamii ya watu wa Burundi kuiwezesha Benki ya CRDB Burundi kufanya vizuri sokoni. Sehemu ya shughuli zilizofanyika ni pamoja na kutoa misaada kwa makundi yenye uhitaji maalum, uandaaji wa shin­dano la mchezo wa mpira wa kikapu kwa vijana pamoja na ujenzi wa mra­di wa usafi kwa jiji la Bujumbura.