Salamu za Siku ya Kitaifa ya Ireland 2023

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mary O’Neill.

Leo ni Siku ya Mtakatifu Patrick, siku ya kitaifa ya Ireland, siku ambayo tunasherehekea mambo yote ya utamaduni wa Ireland. Mwalimu Nyerere alipozungumza jijini Dublin mwaka 1979, alieleza jinsi alivyojisikia yuko nyumbani.

Ingawa kisiwa kidogo cha Kaskazini-Magharibi mwa Ulaya na nchi kubwa ya kitropiki ya Afrika inaweza kuonekana kuwa ni marafiki wasiotarajiwa, ninaamini kwamba tunu tatu za kitamaduni hutuunganisha, ambazo ni: mshikamano, utu na mtazamo chanya.


Mshikamano

Ireland na Tanzania zina uzoefu unaofanana wa kipindi baada ya ukoloni na bado ni nchi changa. Mwaka huu, Ireland inaadhimisha miaka 100 ya uwepo wake duniani na hivi karibuni Tanzania iliadhimisha miaka 60 ya uhuru.

Waziri wa Nchi wa Ireland anayeshughulikia Matumizi ya Ardhi na Bioanuwai katika Idara ya Kilimo, Chakula na Bahari, Pippa Hackett pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Dk Damas Ndumbaro na Balozi Mary O’Neill wakiwa katika tafrija ya Siku ya Mtakatifu Patrick jijini Dar es Salaam. Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Ireland, Tanzania/Philemon Kabuje

Tangu uhuru, nchi zote mbili zimekuwa wanachama hai wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukuza demokrasia, amani na usalama. Tulikuwa bega kwa bega kupinga ukoloni na utawala wa wachache barani Afrika na sehemu nyingine.

Ukarimu ni kiini cha tamaduni zetu. Nchini Ireland, badala ya neno ‘karibu’, utasikia fáilte (karibu). Tanzania kwa muda mrefu imekuwa kisiwa cha amani kwa watu wanaokimbia vita katika nchi zao na mwaka jana Ireland ilipokea takribani wakimbizi 80,000 waliokimbia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Taoiseach Jack Lynch akimkaribisha Rais Julius Nyerere katika uwanja wa ndege wa Dublin Novemba mwaka 1979. Picha kwa hisani ya RTÉ

Utu

Hata kabla ya uhuru, watu wa Ireland na Watanzania walifanya kazi pamoja katika ngazi ya kijamii. Wamisionari wa Ireland walihamasisha elimu na afya. Aidha, mapadre wa Ireland waliwafundisha marais kadhaa wa zamani wa Tanzania na sasa mapadre wa Kitanzania wanahudumia jamii nchini Ireland.

Utamaduni huu wa kuwekeza katika watu ndio kiini cha ushirikiano wa kimaendeleo wa Ireland nchini Tanzania. Katika kipindi cha miaka minne ijayo, Ireland itatekeleza programu kwa ajili ya kuwasaidia watu maskini zinazolenga zaidi kwa wanawake na wasichana wasiofikiwa na huduma muhimu, kupitia huduma ya afya ya msingi na ulinzi wa kijamii, kulinda mazingira kupitia mradi wa ‘Bahari Mali’ na kukuza biashara kupitia miradi ya ‘Trademark Africa’ na ‘Maziwa Faida’.


Mtazamo chanya

Nchi zetu zina ari kubwa, zimejaaliwa kuwa na uchumi unaokua na idadi ya watu inayoongezeka. Tumepitia vipindi vigumu, lakini tuna mipango kabambe ya maisha bora ya baadae.

Halima Dumba, mnufaika wa Mpango wa Hifadhi ya Jamii wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unaofadhiliwa na Ireland, katika kijiji cha Magomeni, wilayani Bagamoyo. Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Ireland, Tanzania/Philemon Kabuje

Kuna ongezeko la idadi ya vijana wa Kitanzania wanaosafiri kwenda Ireland kusoma katika vyuo vikuu vyetu vya hadhi ya kimataifa na kufanya kazi katika kampuni zinazoongoza duniani katika sekta ya teknolojia na dawa, nyingi zikiwa na makazi yake nchini Ireland.

Ninafurahishwa na siku njema zaidi zijazo katika uhusiano wa Ireland na Tanzania. Kwa pamoja tunaweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, tunaweza kuimarisha uhusiano wetu wa kibiashara na kiuchumi, tunaweza kuendelea kuwa viongozi katika kuhimiza amani na maendeleo endelevu.

Siku ya Mtakatifu Patrick ni wakati maalum wa kuungana na marafiki wa Ireland duniani kote. Natarajia kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Ireland na kukuza upendo kati ya watu wetu.

Beannachtaí Lá Fhéile Phádraig daoibh go léir. Heri ya Sikukuu ya Mtakatifu Patrick kwa wote.