Sportpesa ni chachu ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kupaa viwango Afrika

Soka kama ingekuwa dini mpya, basi asilimia kubwa ya Watanzania wangebadili imani, kutokana na mapenzi mazito waliyonayo katika mchezo huu, licha ya kiwango cha mahaba yao na ubora wa kile kinachotoka kwa vilabu vyao pendwa havikuendana kwa miongo mingi.

Tumeishi katika mapenzi na mchezo huu huku vilabu vyetu pendwa (Simba na Yanga) vimekuwa vikiongoza ligi kwa kupishana miaka kwa miaka bila ya upinzani halisi hata visipokuwa bora.  

Tumekuwa na historia ya kuzalisha wachezaji bora na mashuhuri kama akina Zamoyoni Mogela, Dua Said, Lunyamila, Mwameja, Kaseja, Mbwana Samata, Simon Msuva, Sunday Manara huku ligi yetu ikiwa bado si bora katika ngazi ya kikanda na hata barani Afrika. Lakini kwa kuwa kila nabii na zama zake, kwa miaka miwili mfululizo kuanzia 2022 ligi kuu ya Tanzania imepanda hadhi.

Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za mpira wa miguu duniani (IFFHS) liliitangaza Ligi Kuu ya Tanzania bara  kuwa ligi ya tano kwa ubora Afrika kwa mwaka 2022 na 2023.

Taarifa hiyo iliyotolewa na tovuti ya IFFHS January 19, 2023, pia imeonesha Ligi ya Tanzania imepanda kidunia kutoka nafasi ya 62 kwa mwaka 2021 hadi 39 kwa mwaka 2022.

Hatua hii ni matunda ya kuongezeka kwa thamani ya ligi kunakotokana na mikataba ya udhamini wa vilabu nchini ambapo katika eneo hili hauwezi kuacha kuitaja SportPesa ambayo tangu kuingia kwake nchini mwaka 2017 na kuvidhamini vilabu vya Simba, Yanga, baadaye Namungo na Singida FG imeleta mapinduzi makubwa yaliyoongoza ushindani na kufanya ligi yetu kupaa viwango Afrika na Dunia.

Udhamini huu wa Sportpesa ulivisaidia vilabu hivi kujiendesha ikiwamo ulipaji mishahara, gharama za usafiri, malazi, chakula na mengineyo ambayo kimsingi yanahitajika kufanywa na vilabu vyenye hadhi ya kucheza ligi kuu.

Hilo liliendana sambamba na mchango wa Sportpesa pia katika kuboresha miundombinu ya michezo ikiwemo ukarabati wa viwanja kama walioufanya katika uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ni sehemu ya utambulisho wetu wa ligi inayotangazwa hivi sasa Afrika na duniani kupitia vituo vya televisheni.

Mchango wa Sportpesa kusaidia maandalizi ya timu ya Serengeti Boys iliyokuwa ikijiandaa na michuano ya vijana ya AFCON iliyofanyika nchini Gabon mwaka jana, pia ni chachu ya Sportpesa kutaka kunyanyua damu changa ambazo leo tunaziona zikicheza katika ligi hiyo na kufuatiliwa na wadau wa soka barani Afrika.

Wachezaji hivi sasa wanalipwa fedha nyingi wakati mwingine kuliko makocha, wana udhamini binafsi, wanalala mahala pazuri, wana uhakika wa kusafiri, kuna posho na mambo chungu nzima. Ligi hivi sasa inavutia wachezaji wa kigeni ambao wanawapa chachu wazawa kufanya vizuri. Haya yote ni sehemu ya matunda ya wadau ikiwemo Sportpesa.

Kama nchi tunatakiwa kujivunia na kutembea kifua mbele kutokana na kuwa na mdau muhimu wa michezo kama Sportpesa na tutakuwa tumefanya kosa kubwa ikitokea siku tukaipoteza Sportpesa.