SUWASA inavyosimamia miradi ya upatikanaji wa majisafi na salama na usafi wa mazingira Singida


SUWASA PICS

Machi 22 kila mwaka, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya maji. Siku hii hutanguliwa na maadhimisho ya wiki ya maji ambayo haunza Machi 16 ambapo shughuli mbalimbali...

Machi 22 kila mwaka, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya maji. Siku hii hutanguliwa na maadhimisho ya wiki ya maji ambayo haunza Machi 16 ambapo shughuli mbalimbali hufanyika ikiwa ni pamoja na maonyesho ya teknolojia na vifaa vya maji, mikutano ya wadau na uzinduzi wa miradi.

Maadhimisho haya yanatokana na Azimio Na. 47/193 la Umoja wa Mataifa (UN) kuwa kila ifikapo Machi 22 ya kila mwaka nchi wanachama ziadhimishe Siku ya Maji Duniani kwa pamoja.

Hii ni katika kutambua umuhimu na thamani ya maji katika maisha ya binadamu na uchumi wa dunia kwa ujumla. Lengo kuu la maadhimisho haya nchini ni kuungana na mataifa mengine katika kutathimini utekelezaji, mafanikio, changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maji na kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira na kusimamia utunzaji wa rasilimali ya maji nchini.

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) ni moja ya taasisi zinazoadhimisha wiki ya maji kwa kufanya shughuli mbalimbali zenye lengo la kuboresha sekta ya maji mkoani humo, kama anavyoeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Patrick Nzamba.

“Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) ni Taasisi ya Serikali, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya “Water Work Act Cap 272” ya mwaka 1997. SUWASA ilitangazwa kuwa Mamlaka inayojitegemea mwaka 1998 kama Taasisi ya Umma ambayo inafanya shughuli zake kwa kufuata sheria na kanuni mbalimbali za nchi katika utawala na uendeshaji wake wa kila siku,” alisema Mhandisi Nzamba.

Anasema, katika kuboresha na kuongeza ufanisi katika usambazaji wa huduma ya maji safi, sheria hiyo ya maji ilifutwa na sasa SUWASA inafanya shughuli zake kwa kufuata sheria ya maji namba 5 ya mwaka 2019 “The Water Supply and Sanitation Act, No 5”.

“Hapo awali SUWASA ilikuwa inahusika na kusambaza maji maeneo ya mjini pekee, lakini kwa hivi sasa Suwasa inahusika na usambazaji huduma ya maji Manispaa nzima ya Singida (mjini na pembezoni ya mji), pamoja na kusimamia utoaji huduma katika mji wa Manyoni na Itigi” alisema Mhandisi Nzamba.

Anaeleza kuwa, kwa sasa mamlaka imefikia asilimia 69 ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika manispaa ya Singida, na imepokea na kuendelea kuboresha miradi ya maji ya pembezoni ya mji iliyokuwa chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Manispaa ya Singida.

“Pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo, SUWASA inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha huduma ya maji safi na salama katika Manispaa ya Singida na maeneo ya miji midogo ya wilaya inaendelea kusambazwa na kuwafikia wananchi kwa wingi kwa kufanya kazi zake pamoja na wadau mbalimbali wa chama tawala, Wizara ya Maji, Mkoa, Wilaya RUWASA, EWURA na halmashauri husika” anasema Mhandisi Nzamba.

Naye Meneja Ufundi wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Lunango Muwelu, anabainisha kuwa, “Mamlaka inaendelea kutekeleza miradi ya kuongeza mtandao wa mabomba katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Singida ikiwemo Mamise, Unyinga, Mangua Mitogho na Mwaja. Pia zoezi la uchimbaji wa visima linaendelea katika maeneo mbalimbali ya manispaa, Ikungi, Iramba, Kiomboi na Manyoni. Miradi hii ikikamilika italeta uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa maelfu ya wakazi wa maeneo hayo na mkoa wa Singida kwa ujumla.”

Anasema, jukumu kuu la Mamlaka ni kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi unaongezeka kutoka asilimia 69 hadi 95 na usafi wa mazingira unaimarika. Maji ya uhakika yatasaidia kukuza uchumi kwa maana ya kwamba viwanda vitaweza kuendesha shughuli zake ipasavyo na shughuli nyingine kama vile kilimo na ufugaji zitaongeza uzalishaji wake.

“Jitihada mbalimbali zinaendelea ikiwemo kufanya tafiti za (vyanzo vya maji) maeneo ya kuchimba visima ikizingatiwa kwamba SUWASA inategemea maji kutoka ardhini (maji ya visima) na si vinginevyo. Ikumbukwe kwamba maji ya ardhini yana changamoto katika upatikanaji wake, ikiwemo uchafuzi wa vyanzo, mabadiliko ya tabia nchi na ukame. ,” alisema Mhandisi Muwelu.

Katika hatua nyingine ya kuboresha utoaji huduma ya maji kwa wateja, SUWASA imeweza kujenga vituo vya kuchotea maji kwa wananchi wasio na uwezo wa kuunganisha mtandao majumbani. Meneja Biashara wa SUWASA, James Malima anasema, “hadi sasa kuna vituo vya kuchotea maji (magati/vioski) 524 (Mia tano ishirini na nne) ambavyo vinawahudumia wananchi wa Manispaa ya Singida kwa gharama nafuu”.

Moja ya Malengo Endelevu ya Maendeleo, lengo Na. 06 ni kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya maji safi na salama yaliyo nafuu ifikapo 2030. Hivyo, ili kufanikisha malengo hayo, suala la kuwa na ushirikiano na wadau mbalimbali ni la msingi, na ndiyo maana SUWASA tunaendelea kushirikiana na RUWASA, Bodi ya maji Bonde la Kati, Serikali ya Mkoa, Manispaa na Serikali za Mitaa/Vijiji katika kuhakikisha shughuli zetu za kuwafikishia wananchi maji ya uhakika na endelevu linatekelezeka.

“Changamoto hazikosekani sehemu ambapo kuna mikakati ya kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya maji kwa mkoa wa Singida. Ulipaji wa Ankara za maji wa kusuasua kwa baadhi ya wateja unakwamisha jitihada za Mamlaka ya Maji Singida kusonga mbele katika kuboresha huduma ya maji ikiwemo wizi wa maji kwa wateja wasio waaminifu,” alisema Malima.

Na kuongeza kuwa, kazi inaendelea ya kufunga dira za malipo ya kabla kwa wateja (taasisi na biashara) na vituo vya kuchotea maji vinavyotumia kadi maalumu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa masaa 24. Miradi inayotekelezwa hivi sasa ya kusambaza huduma ya maji katika maeneo mbalimbali itasaidia wananchi kuwa na afya njema na hatimae kushiriki kikamilifu katika kulijenga taifa.

Aidha, malipo ya ankara za maji za wateja kwasasa zinalipwa kwa kutumia mitandao ya simu ya makampuni yote nchini na kwa kuwa mahali popote. Mfumo huu wa malipo ambao pia unahusisha mfumo wa Serikali (GePG), umeondoa usumbufu kwa wateja na umeongeza kiasi cha makusanyo tofauti na hapo awali. Mamlaka ina mkakati wa kuongeza maapato hadi kufikia milioni 350/- kwa mwezi ikilinganishwa na sasa ambapo wastani ni milioni 295/- kwa mwezi.

“Hadi sasa tuna dira za malipo ya kabla zaidi ya 210 zilizofungwa kwa wateja wetu na tunategemea kuongeza dira zingine 300 hadi ifikapo Juni 2021.Vilevile, tuna mradi wa kuboresha vituo vya kuchotea maji 50, na kuviwezesha kutumia mfumo wa kadi ili kuongeza upatikanaji maji kwa saa 24,”. Kupitia wadau wetu wa I4ID (Institution for Inclusive Development) tumeweza kujenga magati (vioski) 4 (manne) ya kutumia kadi maalum zinazotumia mfumo wa jua katika maeneo ya Magwe na Mitunduruni alisema Malima.

Maadhimisho ya wiki ya maji 2020

Mhandisi Nzamba anasema, “Kauli mbiu ya siku ya maji mwaka huu ni “maji na mabadiliko ya tabia nchi, uhakika wa maji salama kwa wote” hivyo mbali na mambo mengine, tunaitumia wiki hii kupima utekelezaji wa shughuli zetu zinavyokwenda, kujitathmini na kuangalia mipango yetu ya mbele. Je, tulipotokea ni wapi, tulipofikia sasa na tunapoelekea na ili kuhakikisha kwamba kiwango cha kuwapa wateja wetu huduma ya maji kinaongezeka.”

“Katika wiki ya maji tutapanda miti katika chanzo cha maji Kisaki/Irao ili kutunza mazingira. Pia, tutazindua vituo vya kuchotea maji katika maeneo ya Mwaja, Mitunduruni na Unyinga (vituo vitazinduliwa, pasipo mikutano ya hadhara wala mkusanyiko wa watu ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Korona). Sambamba na hayo, tutatoa elimu kupitia redio na vipeperushi juu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, matumizi sahihi ya maji, umuhimu wa ulipaji wa ankara za maji bila kusahau kuwakumbusha wajibu wa SUWASA pamoja na haki za wateja ,” alisema Mhandisi Nzamba.