Taarifa za hali ya hewa ni muhimu katika uzalishaji wa kilimo

Mponda Malozo, mtumiaji wa programu tumishi ya Ugani Kiganjani wakati wa uzinduzi huduma za Ugani Kiganjani katika Maonyesho ya Siku ya Chakula duniani yaliyofanyika Moshi Oktoba 2021. Picha ©UNTZIstan Mutashobya.

Muktasari:

  • Uzalishaji bora, mazingira bora, lishe bora na maisha bora kwa wote

Na Mponda Malozo na Alice Maro

Ali Haji ni kiongozi wa mtaa ‘Sheha’ wa eneo la Mahonda ndani ya Wilaya ya Kaskazini B katika Kisiwa cha Unguja, Zanzibar.

Ni mmoja wa wakulima walionufaika na mradi wa miaka minne wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na Usalama wa Chakula Tanzania, unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

FAO na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilifanya kazi pamoja kutoa na kusambaza taarifa na ushauri wa hali ya hewa wa ndani kwa wakati katika wilaya saba za mradi nchini kote.

Kama ilivyo kwa Ali, wakulima wengi wanaendelea kutegemea kilimo cha mvua. Matokeo yake, mabadiliko ya hali ya hewa na yale ya tabianchi, yameathiri kilimo cha mazao, usimamizi wa mifugo na uvuvi; huku athari kubwa zikielekezwa katika maeneo ya uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula.

Ali alijifunza namna ya kuandaa kalenda ya kilimo kwa kuzingatia hali ya hewa kupitia katika mashamba ya majirani zake. Miezi miwili baadaye aligundua mazao katika mashamba yale yamekua vizuri na kuanzia hapo Ali alishawishika kutumia njia hiyo.

“Ningependa kuwashukuru TMA kwa kutoa utabiri wa hali ya hewa. Shukrani nyingi kwa wakulima wenzangu ambao walitumia taarifa iliyotolewa pia,” Ali anasema, akitoa mfano wa jinsi mipango mizuri imeboresha kalenda yake ya kilimo na wenzake.

Katika msimu mzima wa kilimo, maofisa ugani na wakulima lazima wapate taarifa za hali ya hewa ili kufanya maamuzi sahihi kuhusu mahitaji ya uzalishaji katika kilimo.

Programu tumishi inayojulikana kama Ugani Kiganjani inawawezesha maofisa ugani na wakulima wasikose taarifa muhimu na za mara kwa mara kuhusu hali ya hewa na ushauri unaotolewa na TMA.

Taarifa za hali ya hewa zinabadili maisha

Kutokana na mafanikio makubwa ya mradi FAO iliamua kuuelekeza mradi katika wilaya zote nchini.

Mohammed Kombo Hamad, Mwenyekiti wa Kamati ya Wavuvi Kisiwani Pemba, anashukuru kwa mafunzo aliyopata ya jinsi ya kupanga shughuli za uvuvi kwa kutumia taarifa za hali ya hewa na ushauri.

Anasema, kabla ya kupata mafunzo hayo, yeye na wavuvi wachache walishuhudia mfululizo wa matukio na ajali baharini zilizogharimu maisha ya watu wengi na kuharibu vifaa vya uvuvi.

“Kulikuwa na angalau matukio matatu ya wavuvi kukumbwa na dhoruba au hali mbaya ya hewa baharini na kutoweka. Sio tu kutoweka bali kufariki. Boti hizo zilipinduka, na miili ikasombwa hadi kwenye fukwe za mbali za Lamu huko Mombasa, Kenya, na Tanga, Tanzania.” anasimulia, akionyesha huzuni kubwa anapokumbuka.

Kwa kuzingatia matokeo chanya ya mradi huo, FAO itaendelea kufanya kazi na Serikali na washirika wa maendeleo kusaidia mipango inayolenga kufikia utokomezaji wa balaa la Njaa, uzalishaji endelevu wa kilimo wa muda mrefu, na usalama wa chakula unaostahimili hali ya hewa.

* Mponda Malozo (Mtaalamu wa Mapinduzi ya Kilimo na Dijitali Kitaifa wa Miradi ya FAO Tanzania) Alice Maro (Ofisa Mawasiliano FAO Tanzania