Taasisi ya Ustawi wa Jamii katika kuadhimisha siku ya ustawi wa jamii duniani Machi 2020

Muktasari:

Jumanne ya tatu ya mwezi Machi kila mwaka ni siku ya Ustawi wa Jamii duniani. Mwaka huu inaadhimishwa Machi 17, 2020. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Ukuzaji wa Umuhimu wa Mahusiano ya Watu.”

Jumanne ya tatu ya mwezi Machi kila mwaka ni siku ya Ustawi wa Jamii duniani. Mwaka huu inaadhimishwa Machi 17, 2020. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Ukuzaji wa Umuhimu wa Mahusiano ya Watu.”

Ustawi (welfare) ni hali inayoashiria uhakika wa upatikanaji wa mahitaji yote muhimu kwa maisha ya mwanadamu. Mahitaji hayo ni yale ya kimwili, kiakili, kimahusiano, kiuchumi na ulinzi dhidi ya masuala yanayotishia usalama wa mtu husika.

Ustawi wa Jamii (social welfare) ni mfumo wa huduma unaoratibiwa (haswa na Serikali) kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata mahitaji yanayowahakikishia ustawi wao.

Fani ya Ustawi wa Jamii (Social Work ambayo Kiswahili chake bado kipo katika mjadala) ni taaluma inayolenga kumuwezesha mteja kupanua uwezo wake wa aidha kutatua au kuwa na namna chanya ya kuishi na changamoto fulani.

Neno “mteja” katika muktadha wa fani hii ina maana mtu binafsi, familia, vikundi au jamii. Kazi ya mtaalamu wa fani hii ni kumuwezesha mteja kuhuisha uwezo wake katika kukabili changamoto alizonazo zinazotishia ustawi wake.

Wataalamu wa fani hii hujikita kwanza kufanya kazi na mtu mmoja mmoja kwa sababu wanaamini kuwa kila mtu anao upekee. Kuwekeza katika hali za upekee za wateja kunafanikisha upatikanaji wa afua zinazoendana na hali zao. Wateja wa fani yetu ni watu ambao maisha yao yapo kwenye hali ya uhatarishi zaidi.

Hapa tunazungumzia makundi ya watu wafuatao; watoto, watu waishio na ulemavu, watu waishio na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, wazee, wanawake, wakimbizi, watu watumiao dawa haramu za kulevya na kadhalika.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii inaadhimishaje Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani?

Taasisi ya Ustawi wa Jamii katika dhima yake, sawa na taasisi nyingine za elimu ya juu, imejikita katika mafunzo, utafiti na ushauri wa kitaalamu. Kwa kuzingatia hilo, kwa mwaka huu Taasisi imejipanga kutumia wataalamu wake wa Ustawi wa Jamii kutoa huduma ya uelimishaji kwa vijana juu ya masuala mbalimbali ambayo wakifanikiwa kuyaepuka itazuia uwepo wa matatizo ya kijamii na kuboresha ustawi.

Maadhimisho haya yana maana gani?

Maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii ni yenye mantiki kubwa kwetu. Kimahsusi, Taasisi ya Ustawi wa Jamii ni ya kwanza kutoa elimu hii nchini Tanzania. Kwa miaka arobaini na saba ya kuwepo kwake, taasisi imetoa wataalam wa Ustawi wa Jamii ambao wamekuwa wakifanya kazi katika nyanja mbalimbali serikalini na katika mashirika yasiyo ya kiserikali.

Siku ya Ustawi wa Jamii inatupa fursa ya kukutana na wataalamu ambao wamekuwa wakizifanya kazi hizi moja kwa moja na wananchi. Fursa hiyo hutuwezesha kubadilishana mawazo na kuzidi kufahamishana changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yetu.

Kwa kufanya hivyo, wahadhiri hujifunza mambo mapya na pia kupata maeneo ya changamoto mpya za kijamii na za kiutendaji zin-azoweza kustahili kufanyiwa tafiti za kitaaluma.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii na kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani

Kwanza kabisa ni vema kutambulisha kuwa dhima hiyo inazaliwa ama inatokana na kanuni sita muhimu za kimaadili ndani ya taaluma ya Ustawi wa Jamii. Tunaamini kwamba, ni katika mahusiano ya watu matatizo huweza kuzaliwa na ni katika mahusiano ya watu matatizo huweza kutatuliwa.

Katika fani yetu tunatambua kuwa haiwezekani kusaidia kuleta afua kwa mteja kama hatutozingatia mahusiano ya watu. Mahusiano ya watu inamaanisha mahusiano kati ya mteja na watu wanaomzunguka katika ikolojia yake (familia, ndugu, jamaa na marafiki).

Pia, maneno hayo yanamaanisha wataalamu wa Ustawi wa Jamii hawafanyi kazi kwa mfumo uliojifunga bali hufanya kazi pamoja na watu wa fani yao, wataalamu wa fani nyingine na pia pamoja na mteja na wahusika wa karibu wa mteja.

Lengo la mahusiano haya ni hatimaye kuweza kupata ufumbuzi unaotekelezeka kwa ajili ya mteja. Katika Taasisi yetu tunao wanafunzi ambao ni wateja wetu namba moja. Katika jukumu letu la kutoa mafunzo, Taasisi inazingatia sana mahusiano chanya kati ya wanafunzi na wanafunzi, wanafunzi na walimu pia wanafunzi na uongozi wa Taasisi.

Yote haya yakilenga kufanikisha lengo lililomleta mwanafunzi hapa Taasisi. Pamoja na hayo, mara nyingine wakufunzi hulazimika kujenga uhusiano chanya wa karibu zaidi na mwanafunzi pamoja na wale anaohusiana nao, mathalani, wazazi ama walezi.

Huweza kutokea mara kadhaa changamoto za familia ama za marafiki zinazokinzana na muelekeo wa mwanafunzi kufanikisha azma yake ya kusoma na kuielewa fani. Kwa kuongezea hapo, Taasisi ina kituo cha kutoa huduma za unasihi. Kituo hiki kilijengwa ili kuwanufaisha wanafunzi pamoja na wanajamii wanaoizunguka Taasisi.

Hapa watu hupokea huduma sawa sawa na baadhi ya huduma zitolewazo katika ofisi za Ustawi wa Jamii kwenye halmashauri mbalimbali nchini. Katika kufanya kazi kituoni hapo, tunazingatia kuwekeza kwenye mahusiano ya mteja na wahusika wa karibu yake ili kumsaidia haraka kupata afua stahiki.

Majukumu ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii

Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliundwa kwa sheria Na. 26 ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Taasisi iliundwa kwa kusudi la kuzalisha rasilimali watu wenye weledi wa kuboresha mfumo wa utolewaji wa huduma za jamii nchini Tanzania.

Ili kutimiza lengo hilo, Taasisi imejikita katika kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam. Fani mama hapa kwetu ni Ustawi wa Jamii lakini pia Taasisi inatoa mafunzo katika fani za menejimenti ya rasilimali watu (Human Resources Management) pamoja na mahusiano kazini na menejimenti ya umma (Labour Studies and Public Management).

Kozi za ustawi wa jamii zinazotolewa na taasisi

1. Shahada ya Uzamili ya Ustawi wa Jamii

2. Shahada ya kwanza ya Ustawi wa jamii

3. Stashahada ya Ustawi wa Jamii

4. Cheti cha ufundi cha Ustawi wa Jamii

5. Cheti cha Msingi cha Ustawi wa Jamii

6. Cheti cha Msingi cha kazi ya Jamii watoto na vijana

Nafasi ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii katika kukabiliana na changamoto za kijamii

Fani ya Ustawi wa Jamii inajihusisha moja kwa moja na jamii, jamii ambayo inabadilika badilika kutokana na sababu mbalimbali. Sababu hizo zinaweza kuwa hali ya kiuchumi, kupanuka kwa uelewa wa watu kutokana na elimu, jamii kuchangamana na pia matumizi yaliyoongezeka ya Tehama.

Kazi za taasisi yetu katika kuchangia afua mbalimbali za matatizo ya kijamii zinaangukia katika zile zile tatu; mafunzo, utafiti na ushauri. Katika mafunzo, tunategemea mwishoni kupata wataalamu wa kwenda kufanya kazi na jamii zenye hizo changamoto ulizozitaja.

Katika kufundisha, wakufunzi tunajitahidi kuwa na taarifa za hivi karibuni zaidi ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na taarifa za kisasa ili kukabiliana na changamoto za jamii ya wakati huu. Kila baada ya miaka mitano Taasisi hufanya mabadiliko makubwa ya mitaala yake ili kuweza kukidhi mahitaji ya mafunzo yatakayokwenda na wakati.

Pia, tunafanya tafiti kuhusu matatizo ya kijamii na afua zake kwa lengo la kufahamu kwa kina kile kinachofanya matatizo haya yaendelee kuwepo. Ni imani yetu kuwa, tukijiwekeza zaidi katika utafiti wa matatizo ya kijamii pamoja na afua zake, tutajiweka karibu zaidi na utatuzi utakaokidhi mahitaji.

Sehemu ambayo jamii inakwama katika kuboresha ustawi wa jamii

Kwanza kabisa ni uelewa mdogo wa masuala ya Ustawi wa Jamii. Uelewa wa mtu mmoja mmoja, familia, vikundi, mashirika na baadhi ya watendaji serikalini. Tunapozungumzia ustawi, tunazungumzia ubora wa hali ya mtu kihisia, kiakili, kimahusiano, kimwili, kimaadili, kiuchumi na kadhalika. Tukiangalia mambo hayo kwa umakini tutagundua kuwa, kuwekeza katika ustawi wa mtu kutatupa nafasi kubwa ya mtu huyu kuweza kufanikiwa katika masuala mengine yahusuyo maisha yake.

Fani ya Ustawi wa Jamii inalenga kufanikisha mambo matatu; kuzuia matatizo (prevention), kurekebisha (rehabilitation) na kuleta tiba (remediation). Uwekezaji mkubwa umefanyika katika kuwawezesha wataalamu wa Ustawi wa Jamii kuleta tiba na kidogo katika kurekebisha ambapo tunaona wananchi wengi wakitafuta msaada wa wataalamu hawa pale ambapo tatizo limekuwa kubwa.

Hata hivyo Taasisi imejielekeza katika kutafuta suluhu kabla matatizo hayajajitokeza, kwa mfano, utoaji wa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika namna ya kujitambua, kujiamini na kujiwekea malengo chanya katika ustawi wao binafsi, familia zao na Taifa kwa ujumla.

Aidha Taasisi inaandaa programu mbalimbali katika jamii ili kuzijengea uwezo jamii namna ya kukabiliana na matatizo mbalimbali pindi yanapotokea.

Hii pia ni utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya kuzihusisha jamii kupata majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili. Kwa sasa Taasisi inaandaa programu mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Kijitonyama.

Alama ya mafanikio ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii

Alama kubwa ya kujivunia ya Taasisi yoyote ya elimu ya juu ni wahitimu wanaofanya kazi kwa weledi na kuwatumikia wananchi kwa kiwango zaidi hata ya kile walichopokea darasani. Taasisi ya Ustawi wa Jamii inajivunia wahitimu wa fani ya Ustawi wa Jamii ambao wamekuwa wakifanya kazi ya kuleta afua katika jamii ya Watanzania kwa miaka zaidi ya arobaini.

Wengi wakifanya kazi katika halmashauri, mashirika binafsi ya ndani na nje ya nchi. Baadhi ya mifano ya taasisi za huduma zilizoanzishwa na wahitimu wetu ni; New Hope New Winners’ Foundation, Tanzania Child Welfare, New Beginning na Tanzania Mis-sion on Community Opportunity (TAMCO).

Ujumbe wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii katika maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani

Rai tuliyonayo kwa wata-alamu wa Ustawi wa Jamii nchini, ni kuongeza ufanisi katika kazi ambazo zitalenga zaidi kuzuia matatizo ya kijamii kuliko kusubiri wateja wenye matatizo tayari. Pia, tunawapa rai wataalam wa fani hii kujenga utamaduni wa kuhifadhi kazi zao katika maandishi ili iwe faida kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo kufahamu nchi inapotoka na inapoelekea katika utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii.

Mwisho tunatoa rai kwa Serikali na wadau mbalimbali kuwekeza katika tafiti za ustawi wa jamii ambazo zitalenga katika kuufahamisha umma juu ya namna bora zaidi za utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii.

Makala hii imeandaliwa na:-

Ofisi ya Uhusiano na Idara ya Ustawi wa Jamii Taaluma.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii.