Tamko la pamoja la kuanzisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais wa China Xi Jinping afanya hafla ya kumkaribisha anayemtembelea Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kabla ya mazungumzo yao katika ukumbi wa Great Hall of the People huko Beijing, mji mkuu wa China, Novemba 3, 2022.

Tarehe 2 Novemba 2022 Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara nchini China kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.

Aidha, tarehe 3 Novemba 2022, Mheshimiwa Rais Xi Jinping alifanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Katika mazungumzo yao Wakuu hao wa nchi walizungumzia kwa kina uhusiano kati ya nchi hizo mbili, uhusiano kati ya China na Afrika pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa  yenye maslahi kwa pande zote mbili na kufikia makubaliano. Vilevile, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na Mheshimiwa Li Keqiang, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mheshimiwa Li Zhanshu, Mwenyekiti wa Bunge la China.

Marais hao wawili walifurahishwa na urafiki wa  kidugu uliopo kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na kuridhika na matokeo ya uhusiano na ushirikiano wa kirafiki na kidiplomasia ulioanzishwa takribani miaka 58 iliyopita .  Ili kuendeleza zaidi uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kukuza ushirikiano katika nyanja zote na kwa watu wote, Marais hao wawili walitangaza kuukuza uhusiano wa nchi hizo mbili na kuwa Ushirikiano wa Kimkakati.

Aidha, ziara hiyo iliitimishwa kwa kutolewa tamko la pamoja la viongozi hao wawili ambalo liliweka mkazo zaidi kwenye masuala yafuatayo:-

I. Pande zote mbili zilikubaliana umuhimu wa viongozi wa nchi nchi hizi mbili kuimarisha na kukuza uhisiano wa kisiasa na kidiplomasia, kuendeleza kuwepo kwa mikutano ya viongozi wa juu wa Serikali, kuendelea kuimarisha urafiki wa kidugu na kuaminiana kisiasa, kuimarisha uratibu wa kimkakati, kubadilishana uzoefu wa kiutawala, na kuimarisha ubadilishanaji wa uzoefu na ushirikiano kati ya Serikali Kuu na za Mitaa, Bunge na Vyama vya Siasa katika ngazi zote.

II. Serikali ya Tanzania iliipongeza Serikali ya China kwa kufanikisha kwa mafanikio makubwa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC). Halikadhalika, kuipongeza China kwa mafanikio na mabadiliko ya kihistoria katika kuleta maendeleo mbalimbali ya watu wake chini ya uongozi wa CPC, kuiunga mkono China katika kujenga nchi ya kijamaa ya kisasa katika nyanja zote. Serikali ya China iliipongeza Serikali ya Tanzania kwa mafanikio makubwa katika juhudi zake za kuliletea taifa lake maendeleo chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuutakia mafanikio makubwa Mkutano Mkuu ujao wa 12 wa Chama Cha Mapinduzi.

III. Pande zote mbili ziliahidi kuendelea kuheshimiana katika masuala yanayohusu uhuru wa kujiamulia masuala yake ya ndani pamoja na masuala mengine ya msingi. Serikali ya Tanzania ilirejea msimamao wake kuhusu Sera ya China Moja, ambayo inaitambua Taiwan kama sehemu ya China na kupinga vitendo au matamshi yoyote ambayo yanadhoofisha uhuru wa China na ulindaji wa mipaka yake. Serikali ya China inaiunga mkono kwa dhati Tanzania katika kutafuta maendeleo ya taifa na watu wake.


IV. Pande zote mbili zilikubaliana kuendelea kukuza biashara na kuongeza ujazo wa biashara.  Serikali ya China ilikubali kuondoa ushuru wa forodha kwa asilimia 98 ya bidhaa kutoka Tanzania kuingia katika soko la China na kuwa itafanya juhudi za kuhakikisha inafungua zaidi soko lake kwa bidhaa kutoka Tanzania.

V. Pande zote mbili zitatekeleza Hati ya Makubaliano kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Kukuza kwa Pamoja Ujenzi wa Miundominu ya Usafirishaji wa majini na nchi kavu (Building of the Silk Road Economic Belt and the 21st Century Maritime Silk Road) na kuimarisha ushirikiano wa Ukanda Mmoja na Njia Moja (Belt and Road Cooperation). Pande zote mbili ziko tayari kuendeleza kikamilifu uboreshaji na ukarabati wa Reli ya TAZARA na kupanua ushirikiano wa uwekezaji. Serikali ya China itazishawishi kampuni nyingi za China kuwekeza nchini Tanzania na kushiriki katika maeneo mbalimbali yakiwemo maendeleo ya reli, barabara, bandari, usafiri wa anga, nishati, habari na mawasiliano pamoja na miundombinu mingine.  Serikali ya Tanzania itaboresha zaidi mazingira yake ya biashara na kuziwezesha kampuni za China kufanya kazi nchini Tanzania.  Serikali ya China itawawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kufanya biashara kwa urahisi na China.


VI. Pande zote mbili zilikubaliana kukuza ushirikiano wa viwanda kwa lengo la kuongeza uzalishaji pamoja na kushirikiriana katika maeneo kama vile nishati na madini, viwanda, maendeleo ya kijani na uchumi wa kidijitali na kuisaidia Tanzania kufikia uchumi wa kisasa wa viwanda kwa haraka.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

VII. Pande zote mbili zilipongezana kwa mafanikio ya ushirikiano katika maeneo kama vile utamaduni, utalii, elimu, afya ya umma, kukabiliana na magonjwa ya mripuko, michezo, vijana, taasisi za wataalamu na vyombo vya habari, na kukubaliana kukuza zaidi mwingiliano wa watu na watu na utamaduni. Aidha, pande zote mbili zitatoa uwezeshaji wa kufanyika shughuli za kukuza utalii na kukubaliana kuandaa Mwaka wa Utalii na Utamaduni wa China na Tanzania kwa wakati mwafaka. Halikadhalika, pande zote mbili zitawezesha kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na vyombo vya habari. Serikali ya China itatoa nafasi zaidi za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania na kuendelea kutuma timu za Madaktari kuja Tanzania bara na Zanzibar.


VIII. Pande zote mbili zilikubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano katika ulinzi na usalama na kushirikiana kupambana na uhalifu wa kimataifa, kujengeana uwezo wa kitaasisi, mafunzo ya watumishi, vifaa na teknolojia na maeneo mengine. Pande zote mbili zilikubaliana kuongeza ulinzi wa usalama na haki za kisheria na maslahi ya raia na taasisi za kila mmoja katika mipaka yao.


IX. Pande zote mbili zimeahidi kuimarisha uratibu na ushirikiano katika masuala ya kimataifa na taasisi za kimataifa, kuunga mkono kwa pamoja umajumui wa kweli, kulinda mfumo wa kimataifa na Umoja wa Mataifa katika msingi wake na utaratibu wa kimataifa unaoungwa mkono na sheria za kimataifa, na kuendeleza ujenzi wa jamii yenye mustakabali wa pamoja kwa watu wote. Serikali ya Tanzania iliunga mkono Mpango wa Maendeleo wa Kimataifa ulioanzishwa na China na itashiriki kikamilifu katika shughuli husika. Serikali ya China ilishukuru juhudi za Tanzania katika kukuza amani na maendeleo kikanda na kimataifa.


X. Pande zote mbili zilipongeza jukumu muhimu la Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) katika kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Afrika, na kukubaliana kuimarisha mashauriano na uratibu wa masuala yanayohusiana na Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika na kwa pamoja kutekeleza masuala mbalimbali, kutekeleza ushirikiano wa vitendo chini ya Mpango wa Utekelezaji wa Dakar (2022-2024).


XI. Pande zote mbili zilikubaliana kuwa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China ilikuwa ya mafanikio makubwa na ina umuhimu mkubwa katika kuendeleza uhusiano kati ya China na Tanzania na kukuza ujenzi wa jamii ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja katika nyakati mpya. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ilitoa shukrani za dhati kwa Rais Xi Jinping na Serikali ya China na watu wake kwa ukarimu aliopewa wakati wa ziara yake. Mwisho, pande zote mbili zilikubaliana umuhimu wa kuendelea kuwa na ziara za kiserikali na kwa muktadha huo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alimwalika Mheshimiwa Rais Xi Jinping kufanya ziara nyingine nchini Tanzania mwaka 2024 ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano wetu wa kidiplomasia.