Tanzania yaadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani ikidhibiti ueneaji na vifo


ukimwi pic

Mwaka 2019, watu milioni 1.7 walikuwa wanaishi na VVU Tanzania. Hii ni sawa na makadirio ya ueneaji wa VVU miongoni mwa watu wazima (wenye umri kati ya miaka 15-49) ya asilimia 4.8.Mwaka huo huo,...

Mwaka 2019, watu milioni 1.7 walikuwa wanaishi na VVU Tanzania. Hii ni sawa na makadirio ya ueneaji wa VVU miongoni mwa watu wazima (wenye umri kati ya miaka 15-49) ya asilimia 4.8.Mwaka huo huo, watu 77,000 waliambukizwa VVU na 27,000 walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI.

Licha ya idadi hiyo, Tanzania imefanya vyema kudhibiti janga hilo katika muongo mmoja uliopita.Kuongeza upatikanaji wa matibabu ya kufifisha VVU, kumeleta tafsiri ya kuwa kati ya mwaka 2010 na 2018, idadi ya maambukizi mapya ilipungua kwa asilimia 13 na idadi ya watu wanaofariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI, imepungua kwa nusu ya asilimia.

Mpango Mkakati wa Nne wa VVU na UKIMWI wa Sekta ya Afya nchini, unaoendelea kati ya 2017 na 2022, unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma shirikishi za kinga kwa wananchi kwa ujumla ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

Maendeleo makubwa yamepatikana katika kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika miaka michache iliyopita nchini. Serikali ya Tanzania pia inatambua utangazaji wa bidhaa za kondomu kama sehemu muhimu ya mapambano yake dhidi ya janga hili.

Zaidi ya hayo, wakati Tanzania ikiwa na mtaala mpana wa elimu ya jinsia, upatikanaji hafifu wa huduma rafiki kwa vijana, ukosefu wa usawa wa kijinsia, unyanyapaa unaohusiana na VVU, na unyanyasaji wa baa-dhi ya makundi, kama vile wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, vinaendelea kuwa vikwazo vikubwa kwa kuzuia VVU nchini.

T-MARC Tanzania Tanzania ni mshirika mkuu wa serikali ya Tanzania, anayefanya kazi kwa karibu ili kufikia maono ya Tanzania ya “Kumaliza changamoto ya usawa. Kutokomeza UKIMWI. Kutokemeza magonjwa ya mlipuko.”

Likiwa ni shirika lisilo la kiserikali, linalofanya kazi nchini, T-MARC Tanzania imepewa jukumu la kuchagiza athari endelevu za kiafya na kijamii kwa maisha ya Watanzania kupitia utumiaji wa umahiri wa kimsingi katika utafutaji masoko wa kijamii, mawasiliano, usimamizi wa miradi na ushirikiano.

T-MARC Tanzania inatoa huduma bora na bidhaa za afya kwa ajili ya kuzuia magonjwa, kupitia jitihada bunifu na ushirikiano ili kushughulikia changamoto kuu za kijamii na kiuchumi, na hivyo kuchangia ustawi wa jamii lengwa nchini.

T-MARC Tanzania inafanya kazi katika shughuli mbalimbali zinazolenga kutokomeza VVU/UKIMWI. T-MARC Tanzania imekuwa ikihakikisha upatikanaji, matumizi sahihi na thabiti ya kondomu bora na za bei nafuu kupitia bidhaa zake za kondomu za kiume za Dume.

Mradi wa kondomu za kiume za Dume wa T-MARC Tanzania unaojumuisha aina kuu tatu; kondomu za Dume Classic, kondomu za Dume Desire na Dume Extreme, unalenga watu wa rika tofauti na makundi ya kijamii na kiuchumi huku mkazo maalumu ukiwekwa kwa vijana na watu walio katika hatari zaidi.

T-MARC Tanzania imeshauza na kusambaza kondomu za kiume zipatazo milioni 60 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mwaka 2021, Utafiti wa Upimaji wa Ufikiwaji na Utendaji Kazi (MAP), uliofanyika kutathmini ufikiwaji na upatikanaji wa bidhaa za kipaumbele za afya, ulionyesha kuwa wakati kondomu kwa ujumla zilikuwa zikipatikana chini ya asilimia 50 ya maduka ya rejareja na ya jumla, Dume Classic iliongoza soko la kondomu kwa upatikanaji wa asilimia 38 kwenye maduka.Kondomu za Dume zilishika nafasi ya pili katika uongozi wa soko kwa asilimia 32.

T-MARC Tanzania inasambaza kondomu zake na bidhaa nyingine katika mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia wasambazaji wa mikoani 66, waliosambaa katika mikoa 20 inayohudumia pia maeneo ya jirani na kwa kuzingatia majiji manne ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya.

T-MARC Tanzania pia imeendelea kuongeza upatikanaji wa kondomu na bidhaa nyingine za kipaumbele za afya kwa kushirikiana na maduka yaliyoidhinishwa ya Kusambaza Dawa (ADDOs) katika Kanda ya Ziwa kama wasambazaji. Ushirikiano na maduka hayo umeongeza zaidi upatikanaji wa bidhaa katika maeneo ya mbali.

T-MARC Tanzania inatumia mitandao ya kijamii, redio na TV kutangaza aina mbalimbali za kondomu za Dume.

Ushiriki wa ngono wa mapema zaidi ni sababu kuu ya kuenea kwa VVU. Program ya "Families Matter" ya T-MARC Tanzania inayolenga kupunguza tabia hatarishi za ngono miongoni mwa vijana, ikihamasisha vijana kuchelewa kushiriki ngono, jitihada ambayo imeonekana kupunguza viwango vya maambukizi ya VVU na mimba za utotoni miongoni mwa watoto wa shule.

Programu hiyo pia iliboresha ujuzi juu ya malezi sahihi na mawasiliano ya familia kuhusu kupunguza hatari na mada nyingine zinazohusiana na ngono kabla ya vijana kuanza kushiriki matendo hayo.

T-MARC Tanzania pia ilitekeleza mpango bunifu unaojulikana kama "Girls Empowerment" Hakuna Wasichoweza, ili kuimarisha mahudhurio ya shule na mwenendo mzuri wa kitaaluma wa wasichana wadogo katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambako viwango vya ukatishaji masomo na utoro viko juu.

Mradi huo ulitoa taulo za kike za gharama nafuu kwa wasichana wadogo 10,000 walio ndani na nje ya shule ili kuwasaidia kudhibiti hedhi na kuboresha mahudhurio na ufaulu wao shuleni.

Pia, ilisaidia kuongeza viwango vya maarifa ya namna ya kuzuia VVU kwa wasichana waliobalehe ili kuchelewesha ushiriki wao katika ngono, kupunguza tabia hatarishi za kingono, mimba za utotoni, ukatishaji masomo na magonjwa ya zinaa pamoja na VVU.

Vile vile, ushiriki wa ngono na wenza wengi na tabia ya kutotumia kondomu licha ya hatari zilizopo katika mahusiano imara na hata yale ya kawaida ya jinsia mbili tofauti, ni chanzo kingine cha kusambaa kwa virusi.

T-MARC Tanzania, kupitia Mradi wa Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU/UKIMWI ulimwenguni, unaunga mkono jitihada zinazoendelea za Ushauri Nasaha na Upimaji wa Hiari nchini kwa kufikia maeneo lengwa miongoni mwa watu walio katika hatari zaidi na jamii ambazo hazijafikiwa ipasavyo.

T-MARC Tanzania ilianzisha na kusimamia shughuli za ufikiaji jamii kule zilipo, kwa kupitia mawasiliano rafiki kama vile uchapishaji wa vitabu mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu na mafunzo kwa mashirika ya kiraia ili kuonyesha matumizi sahihi ya kondomu za wanaume na wanawake, kukabiliana na unyanyapaa na ubaguzi, kufanya kazi na vituo vya ushauri nasaha na upimaji vya Serikali na mada nyinginezo zinazosaidia utoaji wa huduma hizi muhimu.

Zaidi ya hayo, T-MARC Tanzania ilitekeleza Mradi wa HUSIKA wa kupunguza matukio ya VVU nchini miongoni mwa jamii zilizo katika hatari zaidi na wenza wao wa kingono kwa kuimarisha mazingira wezeshi katika ngazi ya kitaifa, mikoa na wilaya na kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu na zisizo za matibabu zenye ubora wa juu.

Mwisho, chini ya mradi wa Tulonge Afya, T-MARC Tanzania inaelekeza nguvu zake katika kuleta mabadiliko ya tabia katika ngazi ya wilaya na jamii. Mradi huo unachochea Watanzania kuboresha hali zao za kiafya kwa kubadilisha mifumo yao ya kijamii na kitamaduni na kuunga mkono mienendo bora ya afya.

Mradi umetekeleza programu zake kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii ya kimkakati, vipindi vya redio za jamii, maigizo, na vikao vya mazungumzo ya vikundi vidogo vidogo na WAVIU.Mradi umeweza kufikia jumla ya watu takriban 1,609,460 katika mkakati huu.

Kwa kutumia njia jumuishi katika kushughulikia VVU/UKIMWI na masuala mengine muhimu ya afya kama vile Kifua Kikuu na Uzazi wa Mpango.Shughuli za T-MARC Tanzania zinahusisha utengenezaji wa vipindi vya redio vya kitaifa na kikanda, vinavyohusishwa na shughuli za ngazi ya jamii (mazungumzo ya vikundi vidogo, redio ya jamii, na ukumbi wa michezo ya kuigiza wa jamii) ili kuendesha zoezi la upimaji wa VVU.

Pia ushiriki katika huduma za uzuiaji maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto, miongoni mwa wanawake wajawazito, pamoja, na kuhimiza mahudhurio yao kupata huduma muhimu kabla ya kujifungua, huduma ya kujifungua katika vituo maalumu na huduma baada ya kujifungua, ambazo zitasaidia kupunguza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto pamoja na uchunguzi wa vichanga.

Zaidi ya hayo, T-MARC Tanzania pia inahimiza ukamilishaji wa ratiba za chanjo ya watoto na upimaji wa TB unaolenga makundi na mikoa yenye hatari zaidi kupitia matumizi ya kimkakati ya redio za kitaifa na kikanda zinazohusishwa na shughuli za ngazi ya jamii.

T-MARC Tanzania inashirikiana na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) kuongeza upatikanaji wa huduma za matunzo na matibabu miongoni mwa WAVIU, wenzi wao na watoto wao wa kuwazaa ili kuondoa utofauti katika lengo la 95-95-95 la upimaji na matibabu katika PEPFAR.

Mradi uliwashirikisha na kutoa mafunzo kwa watetezi 148 wa matibabu wa NACOPHA ili kuwezesha vikao vya vikundi vidogo na uhamasishaji wa jamii unaolengwa juu ya umuhimu wa upimaji wa fahirisi, ufichuzi wa washirika miongoni mwa WAVIU, pamoja na kufuatilia na kuunganisha wateja wa LTFU kwenye huduma.

Hili lilifanyika katika vituo 23 vya afya vilivyo chini ya PEPFAR katika mikoa ya Iringa, Njombe na Tabora na kufikia WAVIU 42,937 kupitia madarasa kadhaa yaliyoendeshwa kupitia programu shirikishi/rafiki na kuhakikisha wagonjwa 2,545 waliotokomea kwingineko, wanarejea kupatiwa huduma na matibabu.

Chini ya mradi wa USAID Tulonge Afya, T-MARC Tanzania pia inashirikisha viongozi wa kidini kama mabalozi wakuu wa Furaha Yangu ili kuchochea uzingatiaji wa mienendo ya kipaumbele, huduma za upimaji wa kina, na huduma na matibabu miongoni mwa makundi yaliyo hatarini na yale yasiofikiwa kwa urahisi, wakiwemo wanaume.

Ni asilimia 52 tu ya Watanzania walio na VVU wanajua hali zao. Ipo haja ya kuendelea kuhimiza watu wengi wapime afya zao maana wakishajua ni faida kwao, ni muhimu kueleza matumizi ya kondomu mpaka pale hali za watu wengi zifahamike, na wakati huo huo kuangalia uwezekano wa matumizi ya vifaa binafsi na vya siri vya kujipima VVU kwa hiari.

Mwaka 2022, T-MARC itazindua kifaa cha kupima VVU kwa njia ya mdomo ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuzuia VVU na hivyo kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95.