TARURA inavyojipambanua katika ujenzi, ukarabati wa barabara
Sekta ya barabara ni moja ya nguzo kuu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi yoyote. Barabara, kama njia kuu za usafiri, zina mchango mkubwa katika kuunganisha maeneo tofauti, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma na kuboresha maisha ya watu kwa ujumla.
Sekta hii pia ina mchango mkubwa katika kuvutia uwekezaji.Wawekezaji wanapendelea maeneo yenye miundombinu bora ya barabara kwa kuwa inawapa uhakika wa kufikisha bidhaa zao sokoni kwa wakati. Hii inachochea maendeleo ya viwanda, kilimo, na sekta zingine za uzalishaji.
Katika kuhakikisha suala la kuunganisha jamii za vijijini na mijini kupitia barabara linafanyika kikamilifu, Serikali iliunda Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
TARUR ilianzishwa mwaka wa 2017 kwa ajili ya kurahisisha usimamizi wa barabara. Uanzishwaji wa wakala huo chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali ulitangaza mwanzo mpya wa usimamizi wa ubora wa barabara.
Barabara kama njia za kiuchumi
Kwa Watanzania wengi, hasa asilimia 65 waishio vijijini, barabara zinazosimamiwa na TARURA zinaleta tofauti kati ya ustawi na umaskini. Uchumi wa nchi unaendana na ukuaji wa sekta ya kilimo, sekta inayochangia asilimia 26 katika Pato la Taifa.
Chai, Kahawa, Mahindi, Mihogo, mazao haya yote yanategemea barabara zinazopitika kwa ajili ya usafirishaji kutoka shambani hadi sokoni. Bila miundombinu ya uhakika, mazao ya wakulima yana hatari ya kuoza katika mashamba yao ambayo hayawezi kufikiwa na wanunuzi au wasambazaji.
Jukumu la TARURA ni rahisi lakini kubwa sana, kuhakikisha kuwa barabara hizi zinaendelea kufanya kazi katika misimu yote ya mwaka na kwa kufanya hivyo, kudumisha maisha ya mamilioni ya watu.
Takwimu zinaonyesha kuwa, kati ya kilomita 144,429.77 za barabara za wilaya zilizo chini ya TARURA, ni kilomita 3,053.26 tu (asilimia 2.11) ndizo za lami. Kilomita 38,141.21 zilizosalia ni barabara za changarawe (asilimia 26.41) na barabara za vumbi kilomita 103,235.30 (asilimia 71.48), ambazo wakati wa mvua hushindwa kupitika. Barabara hizi, ingawa ni muhimu matengenezo yake ni changamoto ya kudumu.
Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff anakiri ugumu huo akisema kuwa, “Kila kilomita tunapambana kuiboresha, lakini kila kilomita tunayoboresha hubadilisha maisha.”
Hali ya sasa ya barabara nchini
Hadi kufikia Juni 2024, hali ya barabara za wilaya ilikuwa na maendeleo na changamoto ambazo bado zinahitaji kufanyiwa kazi. Kati ya mtandao wote, asilimia 28.22 (kilomita 40,752.98) ziliainishwa kuwa katika hali nzuri barabara ambazo zinaweza kuhimili shinikizo la matumizi ya kila siku bila kuharibika. Barabara hizi ni kielelezo cha mafanikio ya TARURA, matokeo ya jitihada za kuzikarabati na kuziboresha kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu.
Hata hivyo, kilomita 52,750.18, sawa na asilimia 36.52 zimeendelea kuwa katika hali mbaya. Hizi ndizo barabara ambazo hukumbwa na changamoto kubwa katika kipindi cha mvua za msimu ambazo husababisha kushindwa kupitika kwa sababu ya matope huku asilimia 35.26 (kilomita 50,926.60) ziko katika hali ya wastani lakini bado zinahitaji uangalizi.
Juhudi za TARURA katika mwaka uliopita zimewezesha maboresho ya kuvutia. Kwa mfano, mtandao wa barabara za lami uliongezeka kutoka kilomita 2,558.78 Juni 2023 hadi kilomita 2,743.81 kufikia Juni 2024 ongezeko la wastani la kilomita 185.03. Vilevile, barabara za changarawe ziliongezeka kutoka kilomita 21,869.16 hadi kilomita 21,890.53.
Changamoto za kibajeti
Mahitaji ya bajeti ya TARURA kwa mwaka ni Sh 1.635 trilioni, lakini inapokea takribani Sh 850 bilioni tu ikiwa ni zaidi ya nusu ya kile inachohitaji. Upungufu huu wa kifedha ndiyo changamoto kuu ya TARURA na unapunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kile ambacho wakala unaweza kufikia. Pamoja na vikwazo hivyo, TARURA inaendelea kusonga mbele, ikiongozwa na mpango mkakati wake wa miaka mitano (2021/22 – 2025/26) unaolenga kuboresha mtandao wa barabara za wilaya.
Mpango huo unaelekeza ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,450.75, uboreshaji wa barabara za changarawe zenye urefu wa kilomita 73,241.57 na ujenzi wa madaraja 945. Hadi kufikia Juni 2024, TARURA ilikuwa imejenga kilomita 923.96 za barabara za lami, kuboresha barabara za changarawe zenye urefu wa kilomita 22,815.98 na kujenga madaraja 378.
Ni mafanikio ya kuvutia, lakini kama Mhandisi Seff anavyokiri, “Tuko mbali na tunapohitaji kuwa. Pengo kati ya matarajio yetu na rasilimali zetu ni kubwa.”
Sehemu kubwa ya mtandao wa barabara za TARURA inajumuisha barabara za vumbi kilomita 99,032.93 kati ya hizo au asilimia 68.57 ya barabara zote. Barabara hizi ndizo zilizo dhaifu zaidi, ngumu zaidi kutunza na pia ndizo muhimu zaidi.
Jamii za vijijini zinazitegemea kwa kila kitu kuanzia kusafirisha mazao ya kilimo hadi kupata huduma za afya, lakini mara nyingi zinaathirika kutokana na mvua za msimu. Kwa TARURA, dhamira ni kuwezesha barabara hizi zipitike mwaka mzima, bila kujali hali ya hewa.
Matumizi ya teknolojia na ubunifu katika ujenzi wa barabara
Mtazamo wa TARURA kwa sasa haujumuishi tu ukarabati na matengenezo ya barabara zilizopo lakini pia matumizi ya teknolojia mpya za kibunifu ambazo zinalenga kuwezesha matumizi ya rasilimali chache za wakala kadiri inavyowezekana.
Moja ya ubunifu huo ni teknolojia ya ECOROADS ambayo imetumika katika Jiji la Dodoma kujenga barabara yenye urefu wa kilometa moja na katika Wilaya ya Chamwino kujenga barabara za kilomita 6.95. Teknolojia ya ECOZYME ni mbinu nyingine inayojaribiwa katika Wilaya ya Itilima, ambapo kilomita 5.2 za barabara zinaendelea kujengwa. Teknolojia hizi hutumia nyenzo zinazopatikana nchini, kupunguza gharama na athari za mazingira.
“Tunatafuta njia za kufanya kazi kubwa zaidi kwa kutumia rasilimali kidogo. Hatuwezi tu kutegemea njia zilizozoeleka. Tunapaswa kuwa wabunifu na wafanisi zaidi. Barabara zetu lazima zijengwe ili zidumu,” anasema Mhandisi Seff.
Dhamira ya TARURA ya ujenzi wa barabara endelevu na wa gharama nafuu haitegemei teknolojia pekee, bali wakala umeweka kipaumbele katika matumizi ya rasilimali za ndani kila inapowezekana, sio tu kupunguza gharama lakini pia kusaidia uchumi wa Taifa. Mkakati huu tayari umeonyesha mafanikio katika miradi kama vile ujenzi wa kilomita 58.5 za barabara za lami katika mji wa Serikali wa Mtumba na Daraja la Berega lenye urefu wa mita 140 katika Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Maendeleo na changamoto za utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu
Licha ya ufinyu wa bajeti na ukubwa wa kazi, TARURA imeweza kukamilisha miradi kadhaa muhimu ya miundombinu ambayo imebadilisha sura ya mtandao wa barabara nchini. Kwa mfano Wilaya ya Kibaha, wakala umeweka lami kilomita 12.5 za barabara, umeboresha upatikanaji wa maeneo muhimu ya viwanda na kukuza uchumi.
Jijini Dar es Salaam, kilomita 12.8 za barabara za lami zimekamilika katika eneo la Mbweni na kutoa unafuu kwa wakazi ambao hapo awali walilazimika kupita kwenye njia za udongo zenye hali mbaya.
Moja ya mafanikio makubwa ya TARURA ni ujenzi wa madaraja kadhaa ya chuma katika mikoa muhimu kama Kihansi-Mlimba, Ruipa-Kilombero na Miyuge-Ikungi. Madaraja haya yanatumika kama kiunganishi muhimu kati ya jamii za vijijini ambazo hapo awali zilitengwa wakati wa msimu wa mvua. Daraja la Kalambo mkoani Rukwa ni mradi mwingine muhimu unaounganisha jamii na kutoa huduma muhimu kwa mwaka mzima.
Mbali na miradi hii iliyokamilika, kuna baadhi ambayo imekwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha, jambo linalosababisha mtandao wa barabara za TARURA kuwa hatarini haswa wakati wa mvua ambao barabara za vumbi zinakuwa katika changamoto kubwa.
Jinsi TARURA inavyosaidia ukuaji wa kilimo
Mradi wa Agri-Connect ni mojawapo ya mipango muhimu inayolenga kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya kimkakati ya kilimo nchini. Mradi huo wa miaka mitano uliozinduliwa mwaka 2018, umetengewa bajeti ya Sh 116.44 bilioni iliyogawanywa katika awamu tatu.
Lengo ni kuleta mabadiliko, kuhakikisha kwamba wakulima walio katika mikoa inayolima chai, kahawa, mbogamboga na matunda wanaweza kupeleka bidhaa zao sokoni kwa haraka na kwa ufanisi.
Awamu ya kwanza ya mradi huo ililenga wilaya za Kilolo, Mufindi na Mbeya ilishuhudia ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 87.6 kwa gharama ya Sh 40.5 bilioni. Barabara hizi ambazo sasa zimekamilika kwa asilimia 100 tayari zimeleta faida kubwa katika uchumi, zimepunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufikiaji wa masoko kwa wakulima.
Awamu ya pili kwa sasa inaendelea, ambapo barabara zenye urefu wa kilomita 49.12 zinaendelea kujengwa katika wilaya zote kama vile Wanging’ombe na Mbozi.
Mhandisi Seff ana matumaini kuhusu uwezo wa muda mrefu wa mradi huo kwa kusema kuwa “Barabara hizi ni zaidi ya miundombinu bali pia ni njia za maisha kwa wakulima wetu. Kwa kuwa na barabara bora, wanaweza kufikia masoko haraka, kupunguza ubadhirifu na kuongeza mapato yao.”
TARURA na mkakati wa kuziinua jamii za vijijini
Mpango mwingine muhimu ni Mradi wa Uboreshaji wa Barabara za Vijijini na Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE). Mradi huu uliotengewa bajeti ya Sh 822.5 bilioni, umebuniwa ili kuboresha barabara za vijijini na kutengeneza fursa za ajira. Kwa ufadhili wa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, RISE unalenga kujenga barabara za lami zenye urefu wa kilometa 535 (kilomita 400 ambazo zinasimamiwa na TARURA) huku ikitunza kilomita 23,000 za barabara za wilaya.
RISE tayari umeanza kuzaa matunda kwani barabara za Wenda-Mgama na Mtilili-Ifwagi katika wilaya za Iringa na Mufindi zimekamilika kwa asilimia 60 na usanifu wa barabara katika wilaya nyingine muhimu kama vile Ruangwa na Mbogwe unakaribia kukamilika.
Mradi pia unalenga ushirikishwaji wa jamii ili huhakikisha kwamba wakazi wa eneo hilo wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo, kupata ajira kuwa na umiliki wa miundombinu inayojengwa.
Mhandisi Seff anajivunia kile ambacho mradi wa RISE unakifanya kwa kusema “Sisi hatujengi barabara tu bali pia tunajenga mustakabali imara. Barabara hizi huunganisha watu, hutengeneza fursa na kuinua jamii nzima.”
Mkakati wa kuboresha maeneo ya mijini
Wakati barabara za vijijini ndizo lengo kuu la TARURA, wakala pia unahusika katika miradi inayolenga kuleta mabadiliko katika maeneo ya mijini yanayokua kwa kasi nchini kwa kupitia utekelezaji wa mradi wa Kubadilisha Miundombinu na Ushindani wa Miji Tanzania (TACTIC) uliotengewa bajeti ya Sh 1.66 trilioni unaofadhiliwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Lengo la TACTIC ni kuboresha miundombinu katika halmashauri 45 za miji, ikiwa ni pamoja na miji mikuu mitano kama Arusha, Dodoma na Mwanza. Mradi huo ulioanza mwaka wa 2022 hauangazii tu ujenzi wa barabara bali pia ujenzi wa masoko, vituo vya mabasi na mifumo ya mifereji ya majitaka. Mikataba ya awamu ya kwanza ya ujenzi ilitiwa saini mwishoni mwa 2023, na kazi tayari inaendelea katika miji 12 na barabara na mifumo ya mifereji ya majitaka ikiwa ndiyo kipaumbele cha kwanza.
Kukabiliana na changamoto za kimazingira
Changamoto za miundombinu ya Tanzania haziko kwenye ujenzi wa barabara pekee bali hata mafuriko ambayo kwa muda mrefu yamekuwa suala la kudumu katika baadhi ya maeneo, hasa katika Bonde la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Mradi wa Maendeleo ya Bonde la Mto Msimbazi unalenga kukabiliana na suala hili, kupanua na kuongeza kina cha mto huo ili kudhibiti mtiririko wa maji na kuzuia mafuriko. Mradi huo unafadhiliwa kupitia mchanganyiko wa mikopo na misaada kutoka Benki ya Dunia, Hispania na Uholanzi.
Mradi huu hauhusu tu kuzuia mafuriko bali pia kubadilisha bonde hilo kuwa eneo jipya la kiuchumi. Mipango yake ni pamoja na uundaji wa hekta 57 za maeneo ya wazi na makazi pamoja na ujenzi wa Daraja la Jangwani, ambalo litakuwa kiungo muhimu cha usafiri wa jiji hilo. Mhandisi Seff anaona mradi wa Msimbazi ni ishara ya kile ambacho TARURA inaweza kufikia. “Tunachukua eneo ambalo limekuwa tatizo kwa miongo kadhaa na kuligeuza kuwa mali ya jiji,” anasema.
Safari kuelekea 2025
TARURA inasonga mbele kupitia mpango mkakati wake, ikiendelea kuweka malengo yaliyoainishwa katika Ilani ya CCM ya 2020. Wakala tayari umevuka malengo kadhaa, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa mtandao wa barabara za wilaya hadi kilomita 144,429.77 na kuvuka lengo la awali la kilomita 143,881. Vilevile, TARURA imevuka lengo la ujenzi wa barabara za changarawe na kufikia kilomita 42,059.17 sawa na lengo la 2025 la kilomita 35,000.
Lakini bado kuna kazi nyingi za kufanywa ambapo Wakala unaendelea na ujenzi wa barabara za lami unaolenga kufikia kilometa 3,337.66 ifikapo mwaka 2025 na kushirikiana kikamilifu na halmashauri ili kuhakikisha kuwa fedha zinatengwa kwa ajili ya matengenezo na uboreshaji wa barabara.
Dhamira ya TARURA katika ubunifu pia inaendeleza mipango yake ya mbeleni. Wakala unafanyia majaribio teknolojia mpya za ujenzi wa barabara zinazotumia nyenzo zinazopatikana nchini ili kupunguza gharama na athari za kimazingira.
Miradi kama vile majaribio ya ECOROADS na ECOZYME inafungua njia kwa mustakabali endelevu zaidi, ambapo barabara za Tanzania zitajengwa ili kudumu na zenye uwezo wa kuhimili mifumo ya hali ya hewa isiyotabirika.
Safari ya TARURA bado inaendelea, lakini maendeleo ambayo imefikia hadi sasa hayana ubishi. Kuanzia barabara za vumbi za vijijini hadi barabara za mijini zenye shughuli nyingi, kazi ya wakala ni kurekebisha sura ya nchi, barabara moja baada ya nyingine. Mhandisi Seff ana matumaini na mikakati iliyopo kwa kusema kuwa “Hatujengi barabara tu, tunajenga Taifa.”
Safari ya kuelekea 2025 ni ndefu na imejaa changamoto nyingi, lakini kadri Tanzania inavyoendelea kukua na kustawi, TARURA nayo inaendelea kuwepo ikitengeneza njia ya kuelekea kwenye mustakabali mzuri na endelevu. Barabara zinaweza kuwa mbovu kwa sasa, lakini kwa kila kilomita kufanyiwa kazi, Tanzania inakaribia kufikia uwezo wake kamili wa kuwa nchi iliyounganishwa na barabara zenye ubora.