Ubunifu, ubora wa bidhaa na utoaji huduma kwa wakati vinavyoipaisha GSM

Afisa Mtendaji Mkuu wa GSM Beverage, Benson Mahenya (kulia), Afisa Mtendaji Mkuu Usafirishaji na Uchukuzi wa GSM, Aisha Mohammed (katikati) na Afisa Biashara wa GSM, Rajab Kondo (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi wa Superbrand Afrika Mashariki.
GSM Group ni miongoni mwa kampuni kubwa Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla ambayo imekuwa ikigusa maisha ya mamia na maelfu ya watu kutokana na ubora wa bidhaa na huduma inazotoa.

Kwa miaka mingi GSM Group imekuwa mkombozi wa watu kwa njia mbalimbali, ikiwemo utoaji wa ajira, bidhaa na huduma bora ambazo zinarahisisha ufanyaji wa biashara na kutengeneza kipato.
Mafanikio haya ya chapa hiyo kubwa Afrika hayakuja kwa usiku mmoja bali ni kutokana na kujitoa, ushirikiano wa wadau wa ndani na nje, kuaminika na wadau inayofanya nao biashara pamoja na wateja wake inaowahudumia.
Ipo mifano mingi ambayo inadhirihirisha umuhimu wa chapa ya GSM kwenye maisha ya mamia na maelfu ya watu katika maeneo mbalimbali.
Kutokana na mafanikio hayo, GSM Group imekuwa moja ya kampuni zinazoaminika zaidi linapokuja suala la ubora wa huduma na bidhaa jambo lililopelekea kuchaguliwa kushiriki na kunyakuwa tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Miongoni mwa tuzo hiyo ni ile ya Superbrand Afrika Mashariki waliyoitwaa hivi karibuni.
Kutokana na ubora wa bidhaa na huduma zake, GSM Group ni miongoni mwa kampuni zilizofanya vizuri kwenye tuzo za Superbrand kwa mwaka 2023 baada ya kutunukiwa cheti cha ubora ambacho kinaashiria ubora wa huduma na bidhaa mbalimbali ambazo GSM inazitoa kwa wateja, wanachama na washirika wake.
Tuzo hiyo ilitolewa na baraza la Superbrand Afrika Mashariki kufuatia mchakato yakanifu uliohusisha kampuni mbalimbali katika ukanda huu.
Baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, uongozi wa kampuni ya GSM Group ulifanikiwa kufanya mahojiano mafupi na gazeti hili ambayo pamoja na mambo mengine walieleza siri ya ushindi huo pamoja na mikakati ya kuendelea kutwaa tuzo hizo. Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo;
GSM Group imekuwa moja ya chapa za kuaminika Tanzania na Afrika, nini siri ya mafanikio haya?
Siri ya mafanikio ya GSM Group ni kufanya kazi kwa bidii, weledi, ubunifu wa hali ya juu na uaminifu mkubwa katika utoaji wa huduma na bidhaa zetu. Tunasikiliza maoni ya wateja wetu na kuyafanyia kazi.
GSM inajitofautisha vipi sokoni kupitia chapa zake mbalimbali?
GSM Group imeweza kujenga, kulinda na kukuza chapa yake kwa kuwa kampuni bora na ya kuaminika. GSM inajitofautisha kwa kusisitiza ubunifu, ubora wa bidhaa zetu pamoja na utoaji huduma kwa wakati.
Hongereni kwa kutunukiwa tuzo ya Superbrand chaguo la Afrika Mashariki. Tuzo hii ina maana gani kwenu?
Kushiriki mpaka kupata tuzo ni kwa mualiko tu. Tuzo hii kwetu ni chachu na ya kufanya kazi zaidi, imetuongezea morali na kujiamini. Kupitia tuzo hii sasa tunaenda mbali zaidi katika kuaminisha wadau wetu kuhusu ubora wa huduma na bidhaa zetu.
Hii ni mara ya ngapi GSM kupata tuzo hii na nini siri ya mafanikio haya?
Hii mara ya kwanza. Mafanikio haya yametokana na utoaji huduma bora na kutotetereka katika hilo. Tuna imani kubwa katika ubora wa huduma na bidhaa zetu na tunaboresha kila wakati.
Nini kinafuata baada ya GSM kushinda tuzo ya Superbrand?
Huu ni mwanzo wa tuzo nyingi za Superbrand pamoja na nyingine. Tutajitangaza zaidi na kuongeza wigo wa huduma zetu ndani na nje ya Afrika Mashariki.
Kwa kiasi gani tuzo hii itaongeza hamasa katika kuendelea kutoa bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya wateja wenu?
Hii tuzo itatusaidia sana katika kutangaza, kunadi na kuelimisha wateja wetu kuhusu ubora wa huduma na bidhaa zetu. Superbrand ni nembo kubwa sana ya ubora na wanapata wale wanaostahili tu.
Kutokana na uzoefu wenu katika biashara ni changamoto zipi mnakumbana nazo?
Changamoto zipo, lakini kubwa ni uchelewashaji katika kivuko cha mpaka wa Tanzania na Zambia pale Tunduma pamoja na Zambia na Congo. Gari zinachukua muda mrefu.
Nini kifanyike ili kuhakikisha changamoto hii inapungua kama sio kuisha kabisa?
Tuna imani na serikali. Tungependekeza Serikali zetu ziangalie namna gani bora na rafiki ya kuharakisha zoezi la forodha mpakani Tunduma.
Mbali na kutambuliwa kama Superbrand Afrika Mashariki, ni mafanikio gani mengine mnajivunia mpaka sasa?
Tunajivunia kukua kwa biashara zetu. Jina na nembo ya bidhaa zetu inaaminika na kuheshimika sana. Kampuni zetu za usafirishaji na uchukuzi zimepata vyeti vya ISO. Tumefanikiwa kushinda tuzo tatu mwaka huu za Africa Company of the year Awards.