Uchakachuaji gesi unatishia usalama wa watu, kupoteza mapato

Muktasari:

Kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imewekamata watu wawili wanaodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya uchakachuaji gesi.

Kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imewekamata watu wawili wanaodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya uchakachuaji gesi.

Operesheni hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ilifanikisha kukamatwa kwa Justin Roman eneo la Mamba Makabe Wilaya ya Ubungo akiwa na vifaa vya mitungi ya Oryx (sild) ndani pamoja na mitungi 12 ya kampuni nyingine ikiwa imehifadhiwa nyuma ya nyumba.

Mtu mwingine Pollin Munisi ambaye alikamtwa Kimara Bonyokwa akiwa anauza mitungi hiyo isiyoonyesha msambazaji wala risiti anakonunulia.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Mohamed Seif alisema biashara haramu ya gesi ya kupikia ina athari kubwa, sio tu kwa wawekezaji hata kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.

Alisema kwa wananchi wanajaziwa gesi bila kupitia kwenye viwanda maalum vya kujazia gesi, au utaratibu wa kuangali ubora wa mitungi kabla ya kuingia sokoni.

“Ujazaji wa mitungi hiyo hauna uhakika kama imejazwa katika kiwango kinachotakiwa, mara nyingi unakuta gesi imejazwa kwa kiwango cha chini hivyo mtumiaji anakuwa anadhulumiwa, kwani bei anayolipia na kiasi cha gesi kinakuwa kidogo,”alisema Seif.

Kwa upande wa mwekezaji alisema wanawekeza fedha nyingi kwenye biashara hiyo kwa kununua mitungi na mfumo mzima wa usambazaji, mitungi inaponunuliwa huuzwa kwa bei ya ghali sana kuliko bei inayowekwa sokoni na kampuni za gesi.

“Matarajio ya mwekezaji ni kwamba kila gesi inapouzwa kwa muda fulani, zile fedha zirudi kupitia mauzo yake, mwekezaji anapokuwa kawekeza kwa matarajio hayo na kukuta mitungi haitumiwi inavyotakiwa kwa kujazwa gesi inayotakiwa au aliyoinunua na badala yake inajazwa na wachakachuaji inamuathiri kwenye kurudisha mitaji,”alisema.

Alibainisha athari nyingine ni kwa upande wa Serikali, kwani wachakachuaji wamekuwa hawalipi kodi na matokeo yake wanauza gesi nje ya mfumo na kusababisha Serikali, wawekezaji, wasambazaji na wauzaji mtaani kukosa mapato na kusababisha kupoteza muda wao bure.

Hata hivyo Seif amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwa ni changamoto waliyonayo pale wanapohisi lipo eneo watu wanafanya uchakachuaji wa gesi, kwani mara nyingi hufanyika katikati ya makazi ya watu jambo ambalo sio salama.

“Mara nyingi tunapokuwa tunawakamata wanakuwa wakifanya hii biashara katikati ya makazi ya watu jambo ambalo si salama, inaweza kuhatarisha maisha na kusababisha mali kuungua,”

“Unaposikia harufu ya gesi na huitambui, au magari yenye gesi yanaingia kwenye makazi ya watu toa taarifa kwa kuwa gesi haiwezi kuhifadhiwa sehemu ambayo sio salama,”alisema na kuongeza.

Mkurugenzi huyo amezitaka kampuni nyingine za gesi, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) pamoja na vyombo mbalimbali vya Serikali kushirikiana kupiga vita biashara hiyo haramu ya uchakachuaji gesi.

Walichokisema majirani

Mjumbe wa nyumba wa shina namba nne mtaa wa Mamba Makabe Amina Said alisema, kijana huyo hamfahamu kwani kwa kuwa ni mgeni eneo hilo na mmiliki wa nyumba hiyo aliyempangisha hayupo.

Alisema taarifa ya biashara ya gesi huwa anaisikia na wakati wa uhakiki wa Sensa ya Watu na Makazi, tulipoulizia tuliambiwa hapatikani kwa kuwa yuko na mwenzake na huwa wanaondoka asubuhi na kurudi usiku.

“Tulikuwa hatufahamu kama kuna biashara ya hatari inayofanyika, endapo kungetokea athari yoyote jamii ingeweza kuathirika, kwa kuwa eneo hili liko katikati ya makazi ya watu,”alisema Amina.

Regnald Moshi ambaye ni jirani naye alikiri kutomfahamu kijana huyo kwa kuwa yeye ni fundi ujenzi, huwa anatoka asubuhi na kurudi usiku.

Alibainisha kuwa anachofahamu kwa maelezo ya watu wengine nyumba hiyo wapo vijana wawili wanaoishi na   huwa wanaingia na gari ndogo ikiwa na mitungi ya gesi na kutoka pia na mitungi.

“Mmiliki wa nyumba hii alihama wakaja wapangaji ingawa siwafahamu, kutokana na majukumu yangu kuwa mengi huwa nawaona wakiingia na gari na kutoka lakini hatufahamiani,”Moshi.

Kauli ya EWURA

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo alisema moja ya majukumu ya mamlaka hiyo ni kufanya ukaguzi wa LPG mara kwa mara.

Alibainisha kuwa wakati wa ukaguzi huo wanapobaini mitungi fulani imehusika, humchukulia hatua mhusika wanayemkuta na tatizo hilo pamoja na mmiliki wa mtungi.

“Kwa kufanya hivyo wamiliki wa mitungi nao wanapambana kuhakikisha wanaondosha uovu katika biashara hiyo, lakini pia tumepiga marufuku kwa watu wa kawaida kununua mitungi mikubwa ya kilo 67, bali kwa taasisi kama hoteli, hospitali na majeshi,”alisema Kaguo.

Aidha Kaguo alisema mitungi mingi inatumika kupunguzia gesi kwenye mitungi midogo, lakini umma umeshatahadharishwa kutonunua mtungi usiokuwa na Seal, bila hiyo mtungi huo hautauzika.

Kauli ya Jeshi la Polisi

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumaane Muliro alisema taarifa za biashara hiyo zipo na tayari wao kama jeshi hilo limeanza uchunguzi, endapo ikibainika wahusika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Kwa mawasiliano zaidi tupigie Oryx huduma kwa wateja 0800750183