Ufahamu ugonjwa wa presha ya macho (Glaukoma)


JICHO PICS

Ugonjwa wa shinikizo la macho au presha ya macho (Glaukoma) ni ugonjwa ambao huandamana na kuharibika kwa mshipa wa neva ya optiki (Optic nerve).

Ugonjwa wa shinikizo la macho au presha ya macho (Glaukoma) ni ugonjwa ambao huandamana na kuharibika kwa mshipa wa neva ya optiki (Optic nerve).

Ugonjwa huu mara nyingi hujitokeza kwa watu wa makamo hasa baada watu hao kutimiza au kuvuka miaka arobaini (40).Kwa kiasi fulani unaweza kujitokeza zaidi kwa watu wenye vinasaba vinavyofanana, kwa hiyo wakati mwingine ugonjwa huu huonekana kwenye familia au ukoo fulani zaidi kuliko watu wengine.

Vyanzo na aina za ugonjwa wa presha ya macho

Mara nyingi chanzo chake huwa hakijulikani, lakini tafiti nyingi zimeonyesha kuwa uwepo wa presha wa juu zaidi ya kiwango cha kawaida kwenye macho unahatarisha zaidi kuleta ugonjwa huu wa glaukoma.

Uwepo wa kiwango hiki kikubwa cha presha ya macho huweza kuharibu mshipa wa fahamu unaomsaidia mtu kuona.Vyanzo vingine ambavyo vinajulikana kusababisha uwepo wa presha ya macho haviathiri watu wengi ukilinganisha na vile ambavyo vyanzo vyake havijulikani.

Vyanzo hivi vingine ni pamoja na kasoro za kimaumbile katika sehemu ya jicho ambayo kazi yake kubwa ni kutoa maji ndani ya jicho ili kuweka sawa uwiano kati ya presha ndani ya jicho na uzalishaji wa maji ndani ya jicho hilo hilo.

Pia, ugonjwa huu unaweza kusababishwa na majeraha yanayotokea kwenye jicho kama vile yale yanayoweza kusababishwa na kupigwa kwa jicho na kitu kwa kiwango kikubwa ambayo yatasababisha kuharibika kwa sehemu ambayo maji yaliyotengenezwa na jicho hupitia kabla ya kutoka nje ya jicho.

Dalili za kuwa na ugonjwa wa presha ya macho

Kwa ile presha ya macho ambayo chanzo chake hakijulikani, huwa na dalili kidogo tu zikiwamo kama hizi zilizo orodheshwa hapa:

• Kusikia jicho zito

• Maumivu ya wastani.

• Kutokwa na machozi

• Jicho au macho kuwa mekundu hasa karibu na mzunguko ule wa weusi wa jicho karibu na konea

• Kupungua uwezo wa kuona

• Kuona rangi za kama upinde wa mvuaKusikia kichefuchefu na kutapika ambazo huambatana na maumivu makali ya jicho na kichwa huashiria ya kuwa presha ya jicho ipo kwenye kiwango kikubwa sana.

Athari za presha ya macho kuwa juu kuliko kiwango cha kawaida

Presha ya macho inapokuwa juu zaidi ya kiwango cha kawaida kwa muda mrefu bila kutibiwa na kudhibitiwa vyema inaweza kusababisha mshipa wa fahamu unaomsaidia mtu kuona kuharibika taratibu na mwisho unaweza kuleta upofu wa kudumu katika macho.

Kutokana na hali hii ya kuongezeka kwa mbanano ndani ya jicho, husababisha kuongezeka kwa mkandamizo mkubwa wa presha kwenye mshipa wa neva ya optiki.

Hali hii huleta athari kubwa kwenye mshipa mkuu wa fahamu wa jicho, ambao pia huwa unabeba mishipa ya damu katikati yake. Mgandamizo huu wa hali ya juu kupita kiwango cha kawaida, unaweza kusababisha mzunguko wa damu ndani ya jicho kuwa hafifu na hivyo kusababisha kuharibika kwa mshipa wa fahamu ambao unaweza kuwa wa kudumu.

Nini cha kufanya iwapo mtu ana dalili za kuwa na ugonjwa wa presha ya macho?

Presha ya macho inaweza kuharibu uwezo wa mtu kuona moja kwa moja, kwa hiyo iwapo utakuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa huu, hauna budi kuwahi kwenye kituo au hospitali yoyote inayotoa huduma za macho ili uweze kuchunguzwa kwa kina na kupewa matibabu sahihi.

Tiba yake ikoje na inatolewa kwa muda gani?

Tiba ya ugonjwa wa presha ya macho hutolewa kwa nia kuu ya kuhakikisha uwezo wa kuona uliopo haupungui tena zaidi ya hapo ulipo, na pia kuhakikisha ya kuwa mgonjwa hapati usumbufu wowote wa maumivu ya macho hata kama atakuwa haoni vizuri au kutokuona kabisa.

Tiba ya ugonjwa huu imega-wanywa katika makundi makuu matatu:

1. Kutumia dawa mahsusi kwa ajili ya kudhibiti pre-sha ya macho. Matibabu ya namna hii ni ya muhimu na ni ya lazima. Mgonjwa wa presha ya amacho anatakiwa kutumia dawa atakazopewa kila siku kwa maisha yake yote, labda iwapo hapo baadaye itaonekana ya kuwa dawa anazotumia zinapunguza presha ya macho kwa kiwango kikubwa na kuwa chini ya kile kinachokubalika.

2. Upasuaji wa kutengeneza njia mpya ya kuyatoa maji yanayotengenezwa na jicho ili yaweze kwenda nje ya jicho kwa uwiano ulio sawa na yale yanayotengenezwa ndani ya jicho.

3. Tiba ya mionzi maalum ya kwenye macho (LASER) ambayo hufanya kazi ya aidha kupunguza utengenezaji wa maji ndani ya jicho au kufungua njia ya maji kuyafanya yale yaliyokwisha kutengenezwa ndani ya jicho kutoka kwa wepesi zaidi. Tiba hii mara nyingi hutumika pale hatua ya ugonjwa inapokuwa ni kubwa zaidi na hatua hizo mbili za awali zimeshindikana kuleta matunda yanayotemewa na kuidhibiti presha ya macho.

Je, kuna kinga yoyote kuzuia mtu asipatwe na ugonjwa huu?

Sehemu kubwa ya wagonjwa wenye Glaukoma wanaangukia kwenye kundi la wale ambao chanzo cha ugonjwa huu hakijulikani.

Kwa hiyo hakuna kinga yoyote inayojulikana ambayo inaweza kutolewa au kuzuia mtu asi-patwe na ugonjwa huu wa presha ya macho.

Nini cha kufanya Iwapo una ndugu yako mwenye ugonjwa wa presha ya macho?

Kwa sababu ugonjwa huu kwa kiasi fulani unahusishwa na kujitokeza kwa watu wenye vinasaba vinavyofanana kwa karibu, basi kuna umuhimu wa kwenda hospitali ya macho kwa ukaguzi wa macho walau mara moja kwa mwaka mmoja hadi miwili ili kuweza kubaini kama kuna dalili zozote za ugonjwa huo kijitokeza.

Dokezo la muhimuPresha ya macho ni ugonjwa unaoharibu uwezo wa kuona taratibu kwa kuuharibu mshipa wa fahamu unaomsaidia mtu aweze kuona. Hakuna mtu ambaye ana uhakika ya kuwa hawezi kuupata ugonjwa huu. Kwa hiyo kuna umuhimu wa:

• Kupima macho yako walau mara moja kwa kila mwaka

• Kufuata na kuzingatia masharti yote ya tiba ya ugonjwa wenyewe iwapo umeshathibitishwa ya kuwa unao ugonjwa wa presha ya macho.

• Kumuhimiza mgonjwa wa presha ya macho kuhudhuria matibabu yake kwenye kituo kinachotoa huduma za tiba ya macho.

• Kutambua ya kuwa ugonjwa huu haumbukizwi, kwa hiyo kuna umuhimu wa kuwahudumia wagonjwa wenye presha ya macho kwani baadhi yao wana uoni hafifu ambapo uhitaji msaada wa kuwekewa dawa kwenye macho kama sehemu ya tiba au kusindikizwa hospitali kufuatilia matibabu yao kadri wanavyokuwa wamepangiwa.

Makala hii imeandaliwa na Dk Emeritus B. Chibuga ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya macho na upasuaji wa retina katika hospitali ya macho ya Dr. Agarwals iliyopo Dar es Salaam, Tanzania.