Ujumbe wa Katibu Mtendaji wa Baraza la TCAA-CCC

UJUMBE WA KATIBU MTENDAJI WA BARAZA KATIKA MAADHIMISHO LA USHAURI LA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA TANZANIA (TCAA-CCC), YA SIKU YA KIMATAIFA YA USAFIRI WA ANGA

Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga huazimishwa kila Desemba 7, kwa lengo la kuelimisha na kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa usafiri wa anga katika kukuza na kuchochea maendeleo katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN).

Kila baada ya miaka minne (4) Shirika la kimataifa la usafiri wa anga (ICAO) huratibu maadhimisho hayo na hutoa kauli mbiu inayobeba dhima ya maadhimisho hayo.

Kauli mbiu ya mwaka huu 2022 ni Kukuza Ubunifu kwa maendeleo ya Usafiri wa Anga Duniani (Advancing Innovation for Global Aviation Development). Kauli mbiu hii ni muendelezo wa kauli mbiu iliyotolewa mwaka 2019 katika maadhimisho ya miaka 75 ya Shirika la kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).

Katika siku hii wadau wote wa usafiri wa anga hufanya tafakari ya kina juu utendaji wa sekta ya usafiri wa anga pamoja na changamoto zake na kutafuta njia sahihi ya kukabiliana nazo. Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA CCC) linaungana na wadau wa sekta ya usafiri wa anga duniani kote katika kuadhimisha siku hii muhimu.

Watumiaji wa huduma za usafiri wa anga hutumia siku hii kupaza sauti zao kuzitaka mamlaka zinazodhibiti usafiri anga kuongeza udhibiti hususani matumizi sahihi ya teknolojia na kuongeza ushindani kwa ajili kupata usafiri salama na bora.

Baraza ni kiungo muhimu kati ya watumiaji na wadau wengine katika sekta na hivyo tunatumia siku hii kuyataka mashirika mbalimbali ya usafiri wa anga kuboresha huduma za usafiri wa anga.

Katika siku hii tunapaza sauti ya watumiaji wa huduma za usafiri wa anga kuhusu maslahi ya watumiaji pamoja na upatikanaji wa huduma bora, salama na nafuu kwa wakati.

Baraza linafanya kazi hii kupitia mfumo wa kiuthibiti kwa kujenga hoja mahususi wakati wa mijadala ya kiuthibiti hususani kupitia utungaji wa kanuni na taratibu za udhibiti wa soko la usafiri wa anga.

Majukumu ya Baraza ni pamoja Ushauri, Uwakilishi, Utetezi na Uelimishaji kwa watumiaji wa huduma za Usafiri wa Anga, juu ya haki, wajibu na maslahi yao.

Tunaendelea kupongeza juhudi za Serikali katika kuendeleza na kusimamia sekta ya Usafiri wa Anga nchini kwetu, sekta ambayo katika miaka ya karibuni imekua kwa kasi na kuchochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi katika Nchi yetu.

Katika mwaka wa fedha 2022/23 miradi ya ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege imetengewa jumla ya Shilingi milioni 86,102.522. Fedha hizo zitagharamia ujenzi, upanuzi wa barabara ya kutua na kuruka ndege na maungio yake, maegesho ya ndege, majengo ya abiria, majengo ya kuongozea ndege, majengo ya uchunguzi wa hali ya hewa, barabara za kuingia viwanjani, maegesho ya magari na usimikaji wa taa katika Viwanja vya Ndege vya Kigoma, Mpanda, Tabora, Songwe, Mwanza, Arusha, Mtwara Sumbawanga, Shinyanga, Msalato, Bukoba.

Hatua hizi zimeonesha dhamira ya dhati ya kuboresha viwanja vya ndege ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za usafiri na usafirishaji kwa njia ya anga.Katika kufanikisha hilo, ujenzi pamoja na uboreshaji wa viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali nchini umeendelea kutekelezwa.

Pamoja na ujenzi wa miundombinu, Serikali imeendelea kuhuisha mikataba ya kimataifa kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na teknolojia na jumuiya ya Kimataifa kwenye sekta ya usafiri wa anga.ili kufungua soko la usafiri wa anga kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa anga, kuvutia mashirika mengine kutoa huduma nchini na kuimarisha ushindani katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga nchini.

Serikali imeingia mikataba mipya ya usafiri wa Anga (BASA) kati yake na nchi za Cape Verde na Ugiriki. Aidha, BASA kati ya Tanzania na nchi za Oman, Uingereza, DRC, Nigeria, Qatar, Rwanda na Kenya imepitiwa upya.

Pamoja na mafanikio hayo, sekta hii bado ina changamoto nyingi hapa nchini. Baraza kwa kushirikiana na wadau wengine tumeendelea kushughulikia ucheleweshwaji wa safari za abiria na mizigo, changamoto ambayo imeongezeka kujitokeza katika kipindi cha hivi karibuni.

Aidha, tumebaini kuongezeka kwa mahitaji ya huduma ya usafiri wa anga inayotokana na kukua kwa uchumi na kipato cha Watanzania. Katika kipindi kinachoishia Julai 2021 watumiaji wa huduma ya usafiri wa anga waliongezeka kwa asilimia 73 kutoka watumiaji 2,964,471 mwaka 2020/21 hadi watumiaji 5,112,742 mwaka 2021/22.

Ni mapendezo ya Baraza kwa mamlaka zote kujenga na kuendesha sekta hii kwa misingi ya uchumi wa soko iliyojengwa kwenye misingi thabiti ya ushindani kwa watoa huduma na Mamlaka husika ili watumiaji wapate huduma bora kwa bei nafuu.

Sambamba na hilo, Baraza linapendekeza kuendelea na uboreshwaji wa viwanja vya ndege nchini ikiwa ni pamoja na kufunga taa za kuruka na kutua ndege, minara ya kuongoza ndege kwa lengo la kuongeza usalama na matumizi sahihi ya viwanja hivyo. Hii iendane na juhudi za kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje kwenye sekta hii muhimu kwa ajili ya kuongeza huduma na fursa nyingi kwa vijana katika sekta hii muhimu sana.

Siku ya kimataifa ya usafiri wa anga ni nguzo muhimu kwa sekta ya usafiri wa anga kwa kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya usafiri wa anga kwa lengo la kujadili mafanikio na changamoto za usafiri wa anga. Siku hii hutumika kuwaelimisha wadau wa sekta hasa watumiaji ambao huitumia kutoa taarifa sahihi kwa umma juu ya mambo yanayowahusu watumiaji duniani kote.

Imetolewa na,

Katibu Mtendaji,

Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA CCC),

Jengo la TBA Na. L1, Kiwanja Na. 6/2,

Kinondoni, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi,

S. L. P 12242,

14110 DAR ES SALAAM.

22/11/2022