UJUMBE WA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) NA MAKAMU WA TATU WA RAIS WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO), DKT. AGNES KIJAZI KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI “THE WORLD METEOROLOGICAL DAY (WMD)”, 23 MACHI, 2020

Muktasari:

Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani (the World Meteorological Day-WMD), siku ambayo Jumuiya ya Hali ya Hewa duniani kote inaadhimisha kumbukizi ya siku ambayo Mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa mnamo Machi 23, 1950. Kwa kawaida siku hii huadhimishwa na kila nchi mwanachama wa WMO na kuratibiwa na Taasisi za Hali ya Hewa za nchi husika.

Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani (the World Meteorological Day-WMD), siku ambayo Jumuiya ya Hali ya Hewa duniani kote inaadhimisha kumbukizi ya siku ambayo Mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa mnamo Machi 23, 1950. Kwa kawaida siku hii huadhimishwa na kila nchi mwanachama wa WMO na kuratibiwa na Taasisi za Hali ya Hewa za nchi husika.

Taasisi za hali ya hewa zikiwa ni Mamlaka zilizopewa jukumu la kutoa na kusimamia huduma za hali ya hewa katika nchi wanachama wa WMO, hutumia siku hii kuonyesha na kueleza huduma wanazotoa katika kuhakikisha usalama wa watu na mali zao dhidi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa. Kwa hapa nchini kwetu Tanzania, shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa husimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

TMA ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2019 kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 kabla ya hapo taasisi hii ilikuwa ni wakala wa Serikali. TMA iko chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya uchukuzi na imepewa jukumu la kutoa na kudhibiti huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo, TMA ikiwa miongoni mwa taasisi 192 za nchi wanachama wa WMO inaungana na Jumuiya ya hali ya hewa duniani kote kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD). Katika kusisitiza na kuhamasisha umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika mipango na maamuzi kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii, sherehe za WMD zimekuwa zikiadhimishwa kwa kaulimbiu maalumu, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”.

Kaulimbiu hii inaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2020, ambayo imejikita katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye sekta ya maji. Kaulimbiu hii ya Hali ya Hewa na Maji inafafanua uhusiano uliopo kati ya hali ya hewa na rasilimali maji, pamoja na umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa katika maende-leo ya sekta ya maji.

Aidha, kupitia Siku hii ya Hali ya Hewa Duniani ni vyema niwafahamishe wadau wa huduma za hali ya hewa hapa nchini kwamba kwa mujibu wa taratibu za mgawanyo wa majukumu katika Umoja wa Mataifa, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limepewa jukumu la kusimamia masuala ya hali ya hewa na maji.

Taasisi za Hali ya Hewa na Maji (NMHSs) katika nchi wanachama wa WMO hufanya uangazi wa hali ya hewa na maji (systematic observation) na data za hali ya hewa na maji hutumika katika kutoa taarifa za mwelekeo wa hali ya hewa na maji ili kusaidia maamuzi katika vikao vya Umoja wa Mataifa vinavyohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Vikao hivyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi (United Nations Framework Convention on Climate Change - UNFCCC-COP) ambao hufanyika kila mwaka. Kwa kawaida maji yapo katika hali mbalimbali ambazo ni yabisi (barafu), kimiminiko (maji ya kawaida) na gesi (mvuke).

Hali hizo zinatokana na mzunguko ambao maji hupitia ujulikanao kama hydrological cycle unaohusisha ardhi, anga, bahari, maziwa, misitu na mazingira mengine. Ongezeko la joto duniani (global warming) linasababisha changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na limeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya mzunguko wa maji kutokana na kubadilika kwa mifumo ya mikondobahari, mvukizo wa anga, ufanyikaji wa mawingu na mtiririko wa maji kwenye uso wa dunia.

Athari hizo zinatokana na uhusiano uliopo wa moja kwa moja wa mifumo ya hali ya hewa na mzunguko wa maji. Changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa imeathiri pia upatikanaji na ubora wa maji na kupelekea upungufu wa maji yanayohitajika kwa matumizi katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Aidha, mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha mabadiliko ya mfumo wa mzunguko wa maji kwa namna tofauti tofauti. Kwa mfano, maeneo yenye joto zaidi hupata mvukizo zaidi wa maji kutoka baharini, ziwani, ardhini na kwenye mimea. Hivyo, anga lililopo katika eneo lenye joto zaidi lina uwezo wa kuhifadhi unyevunyevu kwa asilimia nne (4) zaidi kwa kila ongezeko la nyuzi joto moja katika kipimo cha Celcius na kupelekea kufanyika kwa mawingu ng’amba ambayo huambatana na mvua kubwa na ngurumo.

Kuongezeka kwa joto husababisha mvukizo wa maji kutoka udongoni na kufanya ardhi kuwa kame zaidi na udongo kuwa mgumu. Hali hii hupelekea maji kushindwa kuingia udongoni pindi mvua inaponyesha, badala yake maji hutiririka kukimbilia kuelekea mitoni, ziwani au baharini, na kuiacha ardhi kuendelea kuwa kame. Matokeo yake na uwezekano wa kuongezeka kwa matukio ya ukame na upungufu wa maji safi na salama.

Aidha, ongezeko la joto katika maji ya mito, maziwa, bahari na mabonde ya maji husababisha uhaba wa hewa safi ya oksijeni katika maji na kupelekea vifo kwa viumbe hai wanaoishi kwenye maji ikiwa ni pamoja na samaki, wadudu na wanyama ambao hutegemea hewa ya oksijeni.

Matukio ya mvua kubwa na ongezeko la mtiririko wa maji pia husababisha usafirishwaji wa udongo, vijidudu vya magonjwa na kemikali kama vile mabaki ya mbolea na pembejeo kutoka maeneo mbalimbali yakiwemo mashamba, viwanda na mashimo ya maji taka kuelekea kwenye vyanzo vya maji (mito, maziwa na bahari). Mbali na kuua viumbehai wanaoishi kwenye maji, kemikali hizo pia husababisha uoto juu ya maji, ambao huathiri upatikanaji wa hewa kwenye maji na kusababisha kuzaliana kwa bakteria pamoja na vijidudu vingine vya magonjwa.

Hali hii inayotokana na wingi wa chembechembe za udongo, matope na kemikali zingine zinazosafirishwa na maji yanayotiririka kutokana na mvua kubwa, husababisha gharama za kusafisha maji kuongezeka. Hivyo, kwa upande mwingine, matukio ya mvua kubwa yanayosababishwa na ongezeko la joto huathiri ubora wa maji kwa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Aidha, miongoni mwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa ni ongezeko la kina cha bahari duniani kote. Hii husababishwa na mambo makubwa mawili: kwanza, ni kutanuka kwa maji ya bahari kutokana na kuongezeka kwa joto la maji, na pili ni kuyeyuka kwa barafu katika maeneo yenye barafu, hususan katika uzio wa actic na antaktika.

Ongezeko hilo la kina cha bahari linahatarisha miundombinu, mazingira na maisha ya jamii zinazoishi maeneo ya fukwe za bahari na visiwa, na kuathiri ubora wa maji kwa kusababisha mwingiliano wa majichumvi na vyanzo vya maji baridi hali inayopelekea hitaji la kutumia teknolojia yenye gharama kubwa kusafisha maji hayo ili kuyafanya bora na yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.

Kutokana na shughuli mbalimbali zinazotegemea maji kwa namna moja au nyingine, mabadiliko haya katika mifumo ya maji yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya viumbe katika uso wa dunia katika siku za usoni.

Hali hii inaonyesha kwamba hali ya hewa ina mchango mkubwa na wa pekee katika mtawanyiko na upatikanaji wa maji katika uso wa dunia, pamoja na ubora wa maji yanayohitajika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu. Ipo mifano halisi ya matukio ya hali mbaya ya hewa yaliyotokea hapa nchini kwa mwaka 2019 na kuathiri upatikanaji na ubora wa maji katika baadhi ya maeneo.

Matukio hayo ni pamoja na kuchelewa kuanza kwa mvua za msimu wa Machi hadi Mei (masika), hata hivyo kumekuwa na matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika msimu huo ambapo mwezi Mei 2019 ulikuwa ni mwezi wenye mvua nyingi zaidi ya kawaida. Matukio ya vimbunga Keneth na Idai katika msimu huo wa masika 2019 ambavyo vilisababisha athari katika maeneo mbalimbali hapa nchini ni miongoni mwa changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Kwa msimu wa mvua za mwezi Oktoba hadi Disemba (vuli) 2019 kulikuwa na mvua nyingi zaidi katika miezi ya Oktoba na Disemba.

Aidha, katika mwaka 2020 tumeshuhudia matukio ya mafuriko ya kutisha katika maeneo mbalimbali ya nchi hususan mkoani Lindi ambayo yalisababisha athari katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya maji. Inatazamiwa kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame yataongezeka kwa wingi (frequency) na ukubwa (intensity) na hivyo kusababisha athari katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji, nishati, usafirishaji na kilimo.

Pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii zinazote-gemea upatikanaji wa maji.

Taarifa hizo ni pamoja na data za hali ya hewa za kipindi kirefu (klaimatolojia), utabiri wa hali ya hewa na matazamio ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate change projections). Hivyo, ni muhimu kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu hali ya hewa ya eneo husika na kutumia taarifa za hali ya hewa katika mipango ya shughuli za kiuchumi na kijamii hususan katika sekta ya maji.

Katika kuhakikisha taarifa za uhakika za hali ya hewa zinakuwepo ili kusaidia kupanga shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa lengo la kufikia maendeleo endelevu, kumekuwa na jitihada za kuboresha huduma za hali ya hewa katika ngazi ya kidunia na kitaifa. Katika ngazi ya kidunia, Programu ya Kidunia ya Huduma za Hali ya Hewa inayoongozwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani “Global Framework for Climate Services (GFCS)” ndiyo program inayoongoza jitihada za matumizi ya huduma za hali ya hewa katika mipango ya maendeleo.

Katika kutekeleza program hiyo kwenye ngazi ya kitaifa kwa nchi wanachama wa WMO, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa “the National Framework for Climate Services (NFCS)”, ambayo ina malengo ya kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta zilizoathiriwa zaidi na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate sensitive sectors) ikiwemo sekta ya maji.

Katika kutimiza mahitaji ya wadau na matakwa ya program ya NFCS pamoja na sheria iliyoanzisha TMA, Mamlaka ya Hali ya Hewa hufanya shughuli za uangazi wa masuala ya hali ya hewa. TMA hufanya uangazi kupitia mtandao wake wa vituo vya hali ya hewa vilivyopo nchi nzima, ambavyo vinajumuisha vituo vilivyopo kwenye uso wa dunia nchi kavu (ground weather stations), vilivyopo bandarini (marine weather stations) na vilivyopo katika anga la juu ambavyo vinajumuisha mtando wa RADAR (upper air stations).

Taarifa zinazotokana na uchambuzi wa takwimu za hali ya hewa kutoka katika vituo hivyo hutumika katika mipango ya maendeleo na utoaji maamuzi. Data za hali ya hewa, hususan mvua ni za muhimu sana kwani zinatoa tabia halisi ya eneo na hivyo ni mwongozo muhimu katika kufanya mipango ya muda mrefu ya maendeleo katika sekta zinazotegemea maji kama vile kilimo, mifugo, nishati, uvuvi n.k.

Aidha, TMA hutoa utabiri wa hali ya hewa unaotumika katika mipango kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi. Utabiri unaotolewa na TMA ni pamoja na utabiri wa kila siku (saa 24), siku tano, siku kumi (dekadal forecast), mwezi, msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa (severe weather warnings and alerts). Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla, ziki-wa na ushauri unaolenga sekta ambazo shughuli zake hutegemea zaidi hali ya hewa na maji.

Aidha, TMA hutoa taarifa mahsusi kwa sekta mahsusi kama vile sekta ya usafiri wa anga na usafiri wa kwenye maji. Utabiri huu husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz), radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter, Youtube, na WhatsApp), magazeti na mfumo wa kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi (FarmSMS).TMA imeendelea kupata mafanikio zaidi katika kutekele-za mpango mkakati wake.

Mafanikio hayo ni pamoja na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Huduma Bora “Quality Management System (QMS) na kuendelea kumiliki cheti cha ubora wa huduma kutoka Shirika la Viwango Duniani (ISO 9001:2015 Certification) katika huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga. Aidha, TMA imeshiriki kikamilifu katika majukumu yake ya kuiwakilisha Tanzania Kikanda na Kimataifa katika masuala ya hali ya hewa.

TMA pia imeendelea kupiga hatua katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii na kuwafikia watu wengi zaidi hususan kwa kutumia redio za kijamii (community radios) ambapo katika mwaka 2019 kumekuwa na ogezeko la asilimia thelathini la redio za kijamii zinazosambaza taarifa za hali ya hewa. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2019, TMA ilifanikiwa kuzindua jarida la huduma za hali ya hewa, ambalo ni mahsusi kwa kuwafikia wadau na jamii yote kwa ujumla ikiwemo sekta ya maji.

Katika eneo la vifaa vya hali ya hewa, TMA imeendelea na mkakati wake wa kuboresha vifaa kwa kununua vifaa vya kisasa na kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki. Mkakati huu umelenga kuboresha vituo vyote vya hali ya hewa nchini ili kuendana na ukuaji wa teknolojia ya hali ya hewa duniani, na pia kutekeleza mkataba wa Minamata (Minamata Convention) unaozitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kusitisha matumizi ya zebaki kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2020.

Aidha, katika kuhakikisha TMA inaboresha huduma zake na kuchangia katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, TMA imeendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa ambazo zimechapishwa katika machapisho mbalimbali ya kisayansi ya kimataifa (International Scientific Peer Reviewed Journals).

Hata hivyo pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji jitihada za wadau wote wa huduma za hali ya hewa, wakiwemo wadau wa maendeleo “Development Partners (DPs)” ili kuunga mkono na kuendeleza jitihada za Serikali.

Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa, mabadiliko ya matumizi ya teknolojia katika huduma za hali ya hewa, mahitaji ya taarifa za sekta maalumu na maeneo madogo madogo (downcaled information) na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika misimu ya mvua ambayo husababisha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa.

Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu wa 2020, napenda kutoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka katika sekta zote za kiuchumi na kijamii kuhakikisha wanazielewa na kuzitumia ipasavyo huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa letu.

Huduma hizo ni pamoja na utabiri wa hali ya hewa na matarajia ya hali ya hewa ya muda mrefu (Climate Projections). Napenda pia kuwaomba wadau wote kutuunga mkono katika utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) ili kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa hapa nchini na kupunguza athari kwa jamii na sekta ambazo zinaathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hewa iki-wemo sekta ya maji.Mwisho, nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteoro-logical Day” (WMD) 2020 yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”.