Umuhimu wa Pori la Akiba Kilombero linalosimamiwa na TAWA mkoani Morogoro

Pori la Akiba Kilombero limetokana na Pori Tengefu la Kilombero lililoanzishwa mwaka 1952 kwa Tangazo la Serikali Na. 107 na ilipofika tarehe 17/02/2023 Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan alitangaza kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba Kilombero kwa tangazo la Serikali Na. 64 la tarehe 17/02/2023.

Hatua hii ilifikiwa kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi na kutokana na Sheria ya Wanyamapori sura ya 283 kifungu cha 14(1).

Pori hili lina ukubwa wa kilomita za mraba 6,989.30 ndani ya Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero, katika Mkoa wa Morogoro linalosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).


Umuhimu wa kiuchumi

Sehemu kubwa ya Mto Kilombero upo ndani ya Pori la Akiba la Kilombero ambao unakadiriwa kuwa na fursa (potential) ya kuchangia katika ufuaji wa umeme wa kiwango cha zaidi ya Megawati 2,100 katika mradi wa kuzalisha umeme wa Mto Rufiji. Mto huu unachangia takribani asilimia 65 ya maji ya Mto Rufiji. Pori hili pia ni muhimu kwa utalii wa picha na uwindaji.

Uvuvi ni moja ya shughuli muhimu ya kiuchumi katika Pori la Akiba la Kilombero kwa wananchi waishio pembezoni mwa Pori hilo kwa kupata kipato mbadala pamoja na kuchangia mapato ya Wilaya ya Kilombero na Ulanga.

Kwa kuzingatia hilo, TAWA imetoa fursa ya uvuvi endelevu kwa wananchi waishio pembezoni mwa Pori la Akiba Kilombero kupitia vibali maalum ili kukuza kipato kwa jamii na kudumisha mahusiano mema kati ya wananchi na wahifadhi.


Umuhimu wa kiikolojia

Eneo hili ni makazi na kimbilio kwa wanyamapori katika kipindi cha kiangazi na pia lina wanyamapori adimu aina ya Sheshe (Kobus vardonii) wanaokadiriwa kuwa 75% ya wanyamapori hao duniani wanapatikana katika Pori la Akiba Kilombero ambao wako katika orodha ya wanyama walio hatarini kutoweka duniani.

Ndani ya Pori la Akiba la Kilombero kuna aina takriban 400 za ndege mbalimbali, aina 23 za samaki wakiwemo njege (Citharinus congicus na Alestes stuhlmanni) ambao baadhi husafiri kati ya Delta ya Mto Rufiji na Pori la Akiba Kilombero katika mzunguko wa kuzaliana.

Pori hili ni shoroba (corridor) kati yake na maeneo mengine yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi ya Milima ya Udzungwa, Hifadhi za Taifa za Nyerere, Mikumi, Hifadhi ya Jamii ya ILUMA, Msitu wa Udzungwa (Uzungwa Nature Reserve) pamoja na misitu mingine inayolizunguka.

Kutokana na uwoto wake wa asili wa ardhioevu wenye utajiri mwingi wa maliasili hususan misitu pamoja na wanyamapori adimu, Pori la Akiba Kilombero ni sehemu ya Bonde la Kilombero ambalo lilipata hadhi ya Kimataifa ya uhifadhi mwaka 2002 kupitia mkataba wa Ramser.


Hitimisho

Katika kuadhimisha siku ya wanyamapori duniani, TAWA inapongeza uamuzi uliochukuliwa na Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza Pori la Akiba Kilombero. Uamuzi huu una tija kwa uhifadhi na Taifa kwa ujumla.