Upatikanaji, upataji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi nchini

Na Fadhila H. A. Khatibu, Jamal Msami, Ignace A. Mchallo na Julius Gontako

Fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi ni rasilimali fedha zinazokusanywa kwa ajili ya kuwezesha hatua ambazo zinalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza hatari, na kuongeza uhimilivu wa mifumo ya wanadamu na ikolojia dhidi ya athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.


Fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi zinabakia kuwa kitovu muhimu cha kufikia maendeleo ya kuwa na kiwango kidogo cha kaboni na mazingira himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.


Utaratibu wa ugawaji wa fedha za miradi hiyo duniani unahusisha mtiririko wa fedha kupitia njia mbalimbali za kimataifa, ndani na nje ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) na taratibu za kifedha za Mkataba wa Paris, kupitia njia za nchi na nchi, kikanda, kitaifa za mabadiliko ya tabianchi.  


Ufuatiliaji wa mtiririko wa fedha hizo ni jambo gumu na lenye kuhitaji ueledi kwani hakuna ufafanuzi uliokubaliwa wa nini kinachojumuishwa katika fedha hizo za mabadiliko ya tabianchi au sheria thabiti za uhasibu zinazoongoza.


Katika Mkataba wa Makubaliano wa Copenhagen wa 2009 (UNFCCC, 2010), na baadaye kuthibitishwa katika Mkutano wa Cancun (UNFCCC, 2011) na kisha Mkutano wa Mazingira wa Durban (UNFCCC, 2012), nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa fedha takriban dola bilioni 30 kati ya 2010 na 2012.


Mkataba wa Paris ulianzisha wajibu kwa wanachama wa nchi zilizoendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukabili mabadiliko ya tabianchi, sambamba na mwelekeo wa dunia wa upunguzaji gesi chafuzi (GHG) na maendeleo  himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. (Kifungu cha 2.1c).


Hii ni kwa mujibu wa kanuni ya “wajibu wa pamoja kwa utekelezaji tofauti na uwezo halisi” kama ilivyoelezwa katika Mkataba. UNFCCC ilielekeza wanachama wa nchi zilizoendelea kutenga rasilimali fedha ili kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza mkataba huo.


Ili kuwezesha hili, Mkataba huo (chini ya Kifungu cha 11) ulianzisha utaratibu wa fedha ambao usimamizi wake ulikabidhiwa kwa Mfuko wa Dunia wa Kuhifadhi Mazingira (GEF) na Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (GCF) kama vyombo vyao vya uendeshaji.


Utaratibu huo wa fedha huamua kuhusu sera za mabadiliko ya tabianchi na vipaumbele vya programu na vigezo vya kunufaika na fedha hizo (UNFCCC). Chini ya fedha hizi, nchi zilizoendelea zina wajibu wa kuchangia gharama za ziada kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi ambazo ni za manufaa ya kimataifa na zinazihitaji nchi zinazoendelea nazo kuchangia fedha kwa katika miradi hiyo (Muyungi, R, 2021).


Itifaki ya Kyoto pia ilitambua hitaji la uwepo wa utaratibu wa fedha kwa ajili ya kuwezesha shughuli za kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa wanachama wa nchi zinazoendelea na kuanzisha Mfuko Maalum wa Mabadiliko ya Tabianchi (SCCF) na Mfuko wa Nchi Maskini (LDCF) ambayo inasimamiwa na GEF na Mfuko wa Kukabiliana (AF) ambayo hutoa fedha za msaada bila ya kuchangia katika fedha za miradi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi.


AF inapata fedha kupitia tozo ya asilimia mbili ya Upunguzaji Uzalishaji wa Gesi Chafuzi Unaokubalika (CER) inayotolewa kwa ajili ya Miradi ya Mifumo Safi ya Maendeleo (CDM). Fedha kutoka AF hupatikana moja kwa moja kupitia Mashirika ya Kitaifa na ya Kimataifa ya Utekelezaji.


Mtiririko wa fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi na mahitaji ya kifedha


Kuna makundi makuu matatu ya fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi: 1) fedha za kimataifa za umma za miradi ya mabadiliko ya tabianchi (zilizoripotiwa kwa OECD), 2) fedha za kimataifa za sekta binafsi za miradi ya mabadiliko ya tabianchi, na 3) fedha za umma na sekta binafsi zinazopatikana ndani za miradi ya mabadiliko ya tabianchi (matumizi ya serikali, hati fungani kwa ajili ya mazingira na fedha).


Mtiririko wa fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unakadiriwa kufikia asilimia 5 ya fedha za mabadiliko ya tabianchi zinazokwenda katika nchi zinazoendelea duniani, wanufaikaji wakuu kati ya 2013-2018 ni Kenya (asilimia 41), Tanzania (asilimia 20) na Uganda (asilimia 19) (NBF/EAC/ Kiambatisho cha Kiufundi/3, 2021).


Fedha nyingi za miradi ya mabadiliko ya tabianchi zimekusanywa kupitia mashirika ya nchi wahisani (asilimia 36), benki za maendeleo za kimataifa (asilimia 57) na mifuko ya mabadiliko ya tabianchi (asilimia 7) zilizopokelewa kwa njia ya mikopo na misaada.


Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, asilimia 74 ya fedha zilipokelewa kama mikopo, asilimia 24 kama misaada na chini ya asilimia 1 kama hisa. Fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zimewekezwa katika kilimo, misitu, na matumizi mengine ya ardhi (AFOLU); na maji na usafi wa mazingira.


Kwa kuzingatia uwasilishaji wa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC), Tanzania imeonekana kuwa na asilimia kubwa zaidi (walau 41) ya mahitaji ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Burundi ndiyo yenye kiwango cha chini (asilimia 1), huku Sudan Kusini ikiwa na hitaji kubwa zaidi la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi la (asilimia 47) katika jumuiya hiyo.


Kuna baadhi ya nchi katika muktadha wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hazijabainishasha mahitaji yote ya kifedha, huku hili likidhihirisha wazi mahitaji ya kukuziwa uwezo wa kitaalamu ili kuweza kuainisha ipasavyo mahitaji ya kifedha ambayo yatafanikisha matarajio yaliyoainishwa katika michango ya nchi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi.


Tathmini ya jumla inaonyesha hitaji la kuongezeka kwa msaada wa kimataifa ili kushughulikia hasara na uharibifu, kutekeleza mipango ya kitaifa ya Kukabiliana na kuongeza matarajio ya michango yao.


Ili kuweza kufanikisha hili, utaratibu mzuri utoaji fedha kwa ajili ya miradi ya mabadiliko ya tabianchi lazima uwekwe ili kuimarisha upatikanaji, uwazi na uwajibikaji. Kupata fedha kwa ajili ya miradi ya mabadiliko ya tabianchi ni mchakato mrefu wenye mahitaji changamano ya kitaasisi na utaratibu wa uidhinishaji na uwasilishaji wa mradi. Hii ni kwa sababu mifuko ya fedha za mabadiliko ya tabiachi zina mahitaji tofauti ambayo lazima yatimizwe.


Miongoni mwa vikwazo vingi vilivyoainishwa katika ripoti ya tathmini ya kiufundi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (2021) inahusiana zaidi na upungufu wa uwezo wa kiufundi na kitaasisi katika maeneo tofauti ambayo yanaweza kupigia chapuo ajenda ya nchi ya fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mifuko ya fedha za miradi hiyo na zana za msingi kwa ajili ya matumizi sahihi na ugawaji.


Kwa kuzingatia Ripoti ya Tathmini ya Maendeleo ya Fedha nchini (MoFP, 2021a), lengo lilikuwa kukusanya jumla ya dola za Kimarekani milioni 304 kutoka vyanzo mbalimbali vya fedha vinavyosimamiwa na taasisi za fedha za UNFCCC (yaani, GEF, GCF, LCDF na AF), Norfund, Finfund na JETRO. Tanzania ilipanga kuanzisha taasisi za kitaifa za ithibati na taasisi za utekelezaji pamoja na kuanzisha mfumo wa kuimarisha fedha za mabadiliko ya tabianchi kupitia Mfuko wa Taifa wa Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi (NCCFM).


Hadi kufikia mwaka 2020 ilikadiriwa kuwa Sh24.7 trilioni sawa na Dola za Kimarekani milioni 10.7 ziliweza kupatikana kwa ajili ya miradi ya mabadiliko ya tabianchi, ambayo ni asilimia 3.6 tu ya kiasi kilicholengwa (ukiziondoa taasisi zisizo za serikali). Baadhi ya changamoto za matumizi hafifu ya fedha za mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mikakati iliyopendekezwa ya upatikanaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi, uwezo wa kuandaa nyaraka zinazokidhi matakwa ya mfuko, ukosefu wa taasisi zenye ithibati ya kupata fedha hizo kama GCF pamoja na mbinu duni za kutambua na kufuatilia fedha za mabadiliko ya tabianchi zinazotoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali.


Inakadiriwa kuwa wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Awamu ya Tatu (FYDP III), jumla ya Sh705.2 trilioni sawa na dola milioni 304 za Marekani zitakusanywa kutoka katika vyanzo hivyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Katika kipindi cha miaka kumi (2013-2023) Washirika wa Maendeleo wametoa ahadi ya dola milioni 230 kama fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi na Dola milioni 540 kusaidia usimamizi wa rasilimali.

Tunapoazimia kufika Tanzania

Kiwango cha utayari wa Tanzania katika kupokea fedha za mabadiliko ya tabianchi kinatathminiwa kwa kuzingatia kiwango chake cha upangaji kimkakati (sera, mfumo wa udhibiti na motisha zinazoathiri uwekezaji unaoendana na mabadiliko ya tabianchi), uwezo wa kitaasisi na upatikanaji, na matumizi (kutafuta, kupokea na uwajibikaji katika masuala ya fedha). Haya yote yanachangia katika uundaji wa utaratibu unaofaa wa kifedha utakaofungua njia ya kupata fedha kwa ajili ya mikakati ya kukabili mabadiliko ya tabianchi.


Utaratibu huu wa kifedha umejumuishwa katika Mkakati wa Fedha wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26 na kwamba hatua za kimkakati za kukuza nafasi ya Tanzania kuelekea fedha za hali ya hewa zitawekwa.


Hatua nyingine zitajumuisha kutambua maeneo ya msaada wa kifedha ili kufanikisha michango ya nchi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi, na kuanzisha utaratibu wa ushirikiano wa kitaasisi kati ya Serikali na sekta binafsi. Pia itatoa mwongozo wa kimkakati wa kupata fedha zaidi ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na hatua za kukabiliana kuelekea mbele.


Kuanzisha Mfumo wa Taifa wa Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi

Kama nchi inayoendelea, Tanzania imekuwa ikipokea fedha kutoka katika vyanzo vya fedha vya UNFCCC na mashirika mengine yaliyopo baina ya nchi mbili, kimataifa na sekta binafsi.


Kupitia Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NCCRS) na Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZCCS), Tanzania imejaribu kuweka vipaumbele vya jumla vya utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi.


Mipango ya Utekelezaji iliyoainishwa katika NCCRS na ZCCS imeonyesha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mabadiliko ya tabianchi, lakini chanzo cha fedha kinachohitajika ili kutekeleza Mkataba wa Paris kikamilifu kinategemea fedha kutoka nje.


Ili kuweza kuharakisha upatikanaji wa fedha hizo, mbinu iliyoratibiwa na Serikali kuu inahitajika ambayo itachangia fedha za ziada za mabadiliko ya tabianchi, kushughulikia hatari, na kujenga imani ya wahisani wa kimataifa juu ya mifumo ya nchi ya kuelekeza fedha za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha ubora wa mapendekezo ya bajeti ili kusaidia mikakati ilioegemea katika utendaji kazi zaidi.


FYDPIII imebainisha fursa zinazowezekana za kuanzisha Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (CCF) kama mojawapo ya jitihada muhimu za kimkakati za kuimarisha upatikanaji wa rasilimali, na pia imetambua haja ya kuanzisha Mfumo wa Taifa wa Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi (NCCFM) kwa ajili ya uratibu na matumizi bora ya fedha hizo (MoFP, 2021b).


NCCFM ni mfumo unaotia wa kuijumuisha ajenda ya mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya Taifa na michakato ya bajeti ili kupanga, kusimamia na kutafuta fedha zinazosaidia malengo ya kimkakati ya mabadiliko ya tabianchi.


Machaguo ya sera yatawekwa kwa ajili ya kupunguza pengo linaloonekana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuangalia bajeti halisi; kuimarisha uwazi na uhasibu sahihi wa fedha na kuwezesha nchi kutumia vyema taarifa za fedha (kama vile fedha za kwa ajili ya kaboni na zile za sekta binafsi) ambazo zitaongeza upatikanaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi, uhamasishaji wa sekta binafsi na kuimarisha uwekezaji wa ndani (Hodes, 2019; Nicholson na wengine, 2021).


Itatoa mwongozo wa kufanya mabadiliko na kuunganisha jitihada mbalimbali zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi zinazofanywa na Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa maarifa, uboreshaji uwezo, uundaji wa sera, na kusaidia zaidi watoa maamuzi ili kuimarisha uwezo wa nchi wa kuchangia fedha za mabadiliko ya tabianchi kwa usawa zaidi, na hatimaye kuchangia kwa ufanisi zaidi katika Malengo ya Maendeleo Endelevu. Pia kutakuwa na utaratibu wa kusimamia na kufuatilia matumizi ya uwekezaji unaopendekezwa wa mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji.


Mfuko wa CCF unatarajiwa kusimamia vyanzo vyote vya mapato vinavyoingia vinavyohusiana na mabadiliko tabianchi na kuwa mfuko mmoja unaosimamiwa na Serikali kuu ambayo itatenga rasilimali kwa miradi ya kiwango kidogo cha kaboni na kuchangia malengo ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.


Kwa kuangalia uzoefu kutoka nchi nyingine, muundo wa pamoja wa CCF unajumuisha vyanzo vya fedha, bodi zinazosimamia (zote za kiufundi na kiutawala), wadhamini, na mawakala wa utekelezaji, na Serikali inapaswa kuhusika katika usimamizi, lakini unatakiwa uwe huru katika maamuzi ya uwekezaji wake huku pia ikiwa huru dhidi ya mashinikizo ya kisiasa (Meirovich et al, 2013). Katika muktadha wa Tanzania, mabadiliko ya tabianchi yataratibiwa na kusimamiwa na MoFP.


Hatua kuu zilizopendekezwa za kuanzisha CCF kama ilivyoainishwa katika Mkakati wa Fedha wa FYDP III ni pamoja na:-

Maeneo yanayopendekezwa ya ujumuishaji katika NCCFM

Uundaji wa NCCFM utashirikisha wadau wote muhimu kwa ajili ya upangaji, usimamizi na utafutaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi. NCCFM inatarajiwa kushughulikia maeneo muhimu yafuatayo:

1. Tathmini ya mipangilio iliyopo, ikiwa ni pamoja na mfumo wa udhibiti (uchambuzi wa hali);

2. Malengo na mawanda ya pendekezo la utaratibu wa fedha

3. Ukokotoaji wa hasara na athari za kifedha za mabadiliko ya tabianchi:

  1. Ufafanuzi wa shughuli zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
  2. Kuanzisha mfumo wa kuhesabu hasara na uharibifu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

4. Mapitio ya mwenendo wa matumizi ya fedha za mabadiliko ya tabianchi ili kuondoa pengo lililopo la uwezeshaji wa kifedha nchini.

  1. Tathmini ya gharama za miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi dhidi ya rasilimali zilizopo.
  2. Kufafanua mazingira yenye uwezekano wa kupata fedha na kulinganisha mazingira yaliyopo sambamba na mipango iliyowekwa. Matukio haya yatajumuisha rasilimali zinazotoka ndani, za kimataifa na sekta binafsi.

5. Kufafanua chaguzi za sera za kupunguza pengo la uwezeshaji fedha za miradi ya mabadiliko ya tabianchi:

  1. Kukadiria jumla ya faida kutokana na chaguzi za sera zilizopendekezwa kulingana na upunguzaji wa hasara na uharibifu.
  2. Kuimarisha mikakati ya matumizi sahihi ya rasilimali.
  3. Mazingatio ya jinsia na makundi mengine yaliyo hatarini katika mikakati inayopendekezwa ya mabadiliko ya tabianchi.

6. Utambulisho wa alama za kitaasisi za mipango ya mabadiliko ya tabianchi, uteuzi wa mradi na ufuatiliaji katika mfumo wa bajeti wa Taifa.

7. Uratibu, ikijumuisha ujanibishaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi kupitia Halmashauri na wadau wa ngazi ya jamii.

8. Uwajibikaji juu ya matumizi ya bajeti na fedha zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi (kufuatilia fedha kwa njia ya usimamizi na utoaji taarifa).

Utaratibu wa uratibu

Hivyo, inapendekezwa kuwa uratibu wa shughuli za mabadiliko ya tabianchi ufanyike kupitia Kamati za Kitaifa za Uendeshaji na Ufundi (Bara na Zanzibar). Kwa hali hiyo mabadiliko ya tabianchi yatasimamiwa na MoFP. Utaratibu wa kina unapaswa kuwekwa ili kujumuisha wadau wote wanaohusika serikalini, watendaji wasio wa serikali na sekta binafsi.


Mahitaji ya kiuwezo

NCCRS na NDC zimebainisha mahitaji ya uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika ngazi tofauti, wakati FYDPIII imezingatia uendeshaji wa NCCFM na mifumo saidizi. Mambo hayo ni pamoja na, utayarishaji wa nyaraka na mifumo inayohitajika, ithibati kwa taasisi zilizokidhi vigezo na taasisi za utekelezaji, utayarishaji wa miradi ya kibenki, uimarishaji wa mifumo ya uratibu na ufuatiliaji, hususan kwa fedha zinazokusanywa na watendaji wasio wa serikali.

Ili kuimarisha upatikanaji wa fedha, mkazo unahitajika kuwa katika mafunzo na mazoezi ya kujenga uwezo ili kusaidia Mamlaka Zilizoteuliwa Kitaifa (NDAs) ziweze kuratibu na kusimamia vyema fedha za mabadiliko ya tabianchi. Pia kuna fedha za utayari, zilizotengwa kusaidia nchi zinazoendelea kusaidia utayarishaji wa mawazo bora ya maandiko, mapendekezo ya fedha na ubadilishanaji maarifa.


Pia kuna vyanzo vingine vinavyopatikana kwa ajili ya programu za majaribio ya mapendekezo, ikiwa ni pamoja na maombi ya pendekezo la: Malipo yanayotokana na matokeo ya utaratibu wa REDD+; kutafuta fedha kwa ajili ya kampuni, ndogo na za kati; upatikanaji wa fedha wa moja kwa moja ulioimarishwa; na mchakato wa uidhinishaji uliorahisishwa.

“Majukumu ya msingi ya REPOA ni kutoa maarifa kupitia tafiti pamoja na kutoa taarifa na ushahidi vinavyohitajika kwa ajili ya utungaji sera na kuchangia katika ukukuza uwezo wa utafiti nchini. Lengo mama ni kuchochea mabadiriko ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya maendeleo jumuishi na uboreshaji wa maisha ya Watanzania.”