Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utunzaji wa mifumo ya ikolojia unavyoziwezesha jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Mkulima wa Kata ya Maore, kijiji cha Maore wilayani Same, Paulo Mtango akiwa katika shamba lake la mbogamboga anazolima kupitia kilimo cha oganiki.

Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya changamoto kubwa zinazoikumba dunia leo. Matokeo yake ni kama vile kuongezeka kwa joto la dunia, kuyeyuka kwa barafu, kuongezeka kwa kiwango cha bahari na matukio ya hali ya hewa kali kama mafuriko na ukame.

Lakini ikolojia ambayo inahusisha mifumo ya kiasili ya maisha kama misitu, mito,bahari na nyasi ina faida kubwakatika kupunguza kasi ya mabadiliko haya.

Utunzaji wa ikolojia unasaidia kudumisha uwiano wa mazingira, kuhakikisha maisha ya viumbe na kusaidia binadamu kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Utunzaji wa mifumo ya ikolojia (Ecosystem-based Adaptation-EbA) kama misitu, ardhi oevu, na maeneo ya nyasi kunasaidia kudhibiti mtiririko wa maji, hivyo kupunguza kasi ya mafuriko kunasaidia kupunguza ukame na kuhakikisha kuwa jamii zinaendelea kupata maji ya kutosha wakati wa vipindi vya ukame.

Ili kuhakikisha hilo linafanyika zipo jamii ambazo zinafanya juhudi za kulinda mifumo ya ikolojia kupitia shughuli mbalimbali ambazo mbali na kuwajengea uwezo wa kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, pia zinawasaidia kujiingizia kipato.

Hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuanzia Serikali kupitia wizara mbalimbali, watunga sera, wadau wa maendeleo na mashirika ya kitaifa na kimataifa kutambua na kushiriki katika juhudi za kulinda na kutunza ikolojia kwa ajili ya ustawi wa dunia yetu na vizazi vijavyo.

Shirika la CARE Tanzania ni miongoni mwa wadau muhimu wa kuzisaidia jamii katika kulinda mifumo ya ikolojia ili kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Mifumo ya Ikolojia ili Kukabiliana na Mabadiriko ya Tabianchi (New Approaches to Up calling and Resilience Ecosystem-based Adaptation, NATURE).

Mradi huu unalenga kuongeza uwezo wa jamii hasa za vijijini kuboresha huduma za mifumo ya ikolojia ili kuweza kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yenye ukame nchini.

Mradi kutatua changamoto za kijamii kama vile ukosefu wa chakula, upatikanaji wa rasilimali, migogoro ya matumizi ya maji, migogoro ya wanyamapori na binadamu, uhamiaji wa wafugaji na migogoro ya matumizi ya ardhi ili kusaidia kurejesha huduma za mifumo ya ikolojia na kuchangia uboreshaji wa sera na sheria za maendeleo nchini ambalo ni suala la msingi linaloathiri urejeshaji wa huduma za mifumo ya ikolojia.

Mradi wa NATURE unatekelezwa katika Wilaya tano; Mufindi (Iringa), Chemba (Dodoma), Kiteto, na Simanjiro (Manyara) pamoja na Same (Kilimanjaro) na CARE Tanzania kupitia Mfuko wa Global EbA na kufadhiliwa na International Union for Conservation of Nature (IUCN).

Safari yangu ya kuelekea wilaya ambazo mradi unatekelezwa ilianza kwa kuwatembelea wanufaika wa shughuli za utunzaji wa mifumo ya ikolojia (EbA) ili kuzungumzia kuhusu manufaa, mafanikio, mambo ambayo wamejifunza na gharama walizotumia katika shughuli zao.


Mufindi (Iringa)

Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ni miongoni mwa wilaya zenye historia ya kukumbwa na ukame ikiwa ni moja ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Mufindi ambayo ni moja kati ya tano za Mkoa wa Iringa imeweka mikakati kuhakikisha kwamba jamii zinalinda mifumo ya ikolojia kupitia shughuli mbalimbali ambazo pia huwasaidia kujiingizia kipato.

Katika kuhakikisha hilo linafanyika jamii kupitia CARE Tanzania zimeunda vikundi vya kuweka na kukopa (VSLAs) ili kutekeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ambazo zinasaidia katika kulinda mifumo ya ikolojia.

Kikundi cha Lugoda Lutali kilichopo Kata ya Sadan ni miongoni mwa vikundi vinavyofanya vizuri katika utunzaji wa mifumo ya ikolojia kupitia shughuli za uzalishaji mali wanazofanya.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Kelvin Lihweuli anasema kikundi hicho chenye wanawake 14 na wanaume 9 kimejikita katika upandaji za miti rafiki wa maji inayotumiaka kutunza vyanzo vya maji inayofahamika kama Mivengi ambako mpaka sasa wana miche zaidi 750 ambayo wanaiuza.

“Miti hii ni rafiki na maji na inatumika katika kutunza vyanzo vya maji. Mbali na miti hiyo pia tunafanya shughuli za ufugaji wa nyuki ambapo mpaka sasa tuna mizinga 60 inayojumuisha ya kisasa na kienyeji, tuna chanzo cha maji chenye uwezo wa kuhifadhi lita 21,000 za maji,” anasema Lihweuli.

Kuhusu changamoto Lihweuli anasema mtaji imekuwa moja katika kikwazo kikubwa kwenye shughuli zao huku ikawaomba wadau pamoja na Serikali kujitokeza kuwanga mkono kwenye shughuli zao ili waweze kufika mbali zaidi.

Katika kijiji cha Igomeakikundi cha kijiji hicho kinafanya shughuli mbalimbali ikiwemo ufugaji samaki. Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Elias Mtambalike anasema kitu kikubwa ambacho wanajivunia ni utunzaji wa mto Liendembele ambacho ndiyo chanzo kikubwa cha maji kwa wananchi wa kijiji hicho.

“Tumejiwekea sheria ndogo ambazo zinamtaka kila mtu kuwa mlinzi wa mazingira hususani vyanzo vya maji kwa sababu mto huu ndiyo tunautegemea katika shughuli nyingi ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, kunyweshea mifugo, matumizi ya nyumbani lakini pia katika ufugaji wa samaki na viumbe wengine wa majini,” anasema Mtambalike.

Afisa Mipango wa Wilaya ya Mufindi Elisey Ngoi anasema wamekuwa wakivisaidia vikundi hivyo kwa kuvipatia mikopo ya halmashauri ambayo inawasaidia katika kuendeeza shughuli zao.


Chemba (Dodoma)

Chemba ni miongoni mwa wilaya zinazokabiliwa na changamoto ya ukame pamoja na mvua zisizo na uhakika jambo ambalo linahatarisha usalama za chakula, migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji vichache vilivyopo.

Vikundi vya utunzaji wa mazingira, upandaji miti, ufugaji wa nyuki, samaki, uhifadhi wa vyanzo za maji, ni miongoni mwa juhudi kubwa ambazo zinafanyika katika wilaya hii zikiongozwa na uongozi wa halmashauri kwa kushirikiana na wadau.

Meneja Mradi Mwandamizi wa Shirika la CARE Tanzania ambaye ni Meneja wa Mradi wa NATURE, Alfei Maseke (kulia) akimsikiliza Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Chemba Zena Omary (kushoto) akimuelezea kuhusu mbegu na miche ya miti mbalimbali ambayo halmashauri hiyo inaiotesha na kuigawa kwa wananchi.

Vijiji kama Waida, Gwandi na Kwa Mtoro ni miongoni mwa vijiji vya mfano ambavyo vimepata mafanikio makubwa kutokana na shughuli za ulinzi wa mifumo ya ikolojia zinazoongozwa na vikundi.

Mkulima wa Kata ya Maore, kijiji cha Maore wilayani Same, Paulo Mtango akiwa katika shamba lake la mbogamboga anazolima kupitia kilimo cha oganiki.Wanajamii wa vijiji hivyo wameshuhudia mafanikio makubwa ikiwemo upatikanaji wa maji kunakosababishwa na upandaji miti katika vyanzo vya maji, kutunga sheria ndogondogo zinaosaidia kulinda vyanzo vya maji, ufugaji wa nyuki ambako ni moja katika ya njia za kulinda misitu pamoja na vyanzo vya maji.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Vumilia, Pius Chima anasema ufugaji wa nyuki ni moja ya njia wanazotumia katika kulinda vyanzi vya maji pamoja na misitu.

“Sehemu yenye mizinga ya nyuki mifugo haiwezi kuingia kwa sababu ng’ombe wanaogopa sana nyuki hivyo kwa kufuga nyuki mbali na kujipatia kipato kkinachotokana na uvunaji wa asali pia tunalinda mazingira na vyanzo vya maji,” anasema Chima.


Simanjiro na Kiteto (Manyara)

Simanjiro na Kiteto ni miongoni mwa Wilaya zilizopo Mkoa wa Manyara ambazo mradi wa NATURE unatekelezwa. Wilaya hizo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya ukame, migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo inahatarisha shughuli za kiuchumi.

Katika Wilaya ya Simanjiro ziko shughuli mbalimbali za kilimo zinazofanyika katika Wilaya hii kuna kilimo cha mpunga katika kijiji cha Ngage na maeneo mengine.

Aidha Simanjiro ni wilaya mojawapo inayoongoza kwa shughuli za ufugaji kutokana na asili ya watu wanaoishi katika wilaya hiyo kuwa ni kabila la wamasai. Katika kuhakikisha kwamba shughuli za kilimo zinakuwa endelevu hata katika kipindi cha ukame, wanajamii wameanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zinazosaidia kutunza mazingira pamoja na kuboresha mifumo ya ikolojia.

Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji, shamba darasa, ufugaji wa nyuki, ufugaji wa samaki, kilimo cha ‘nyumba kitalu’ (Greenhouse farming).

Shughuli hizi zinawawezesha wananchi kujitengenezea kipato huku wakilinda mifumo ya ikolojia inayowawezesha kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Mkulima wa kilimo cha nyumba kitalu wilayani Simanjiro akiwa katika shamba lake ambalo analitumia kwa kilimo cha mbogamboga.

Kijiji cha Ndedo kilichopo Wilaya ya Kiteto ni miongoni mwa vijiji vilivyopata mafanikio makubwa kutokana na utunzaji wa mazingira na ulinzi wa maliasili.

Kijiji hicho kimeanzisha Maeneo ya Usimamizi wa Wanyamapori (Wildlife Management Area-WMA) kwa lengo la kuhakikisha eneo la halivamiwi lakini pia linawanufaisha wananchi.

Ofisa wa WMA kijiji cha Ndedo, Kisaro Thomas anasema biashara ya uvunaji wa hewa ukaa huwaingizia mapato ya Sh 1.5 bilioni kwa mwaka huku shughuli za uwindaji na utalii katika eneo hilo zikiwaingizia Sh 500 milioni kwa mwaka fedha ambazo zimesaidia kuleta maendeleo makubwa katika kijiji hicho.

Mapato yanayopatikana kutokana na mauzo ya kaboni pamoja na leseni za uwindaji hulipwa moja kwa moja kwa jamii kupitia WMA jambo linalowawezesha kutekeleza shughuli zao za maendeleo.

Jamii hupokea mapato yao kwa malipo ya kila mwaka mara wanakijiji wanapokutana ili kuamua jinsi ya kugawana mapato hayo. Fedha zinazopatikana hutumika katika shughuli za maendeleo ikiwemo elimu kwa kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni na ofisi za walimu, mipango ya maendeleo ya jamii, ujenzi wa nyumba za walimu, ujenzi wa vituo vya polisi na ofisi za vijiji.

Kulipa mishahara kwa watumishi wa WMA ikiwemo Skauti wa Kijiji wanaofanya doria na ufuatiliaji wa misitu na wanyamapori wake, huduma za afya, kuboresha miundombinu ya afya na kuimarisha utawala katika ngazi ya mtaa, kata na wilaya ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu inayotakiwa ili kutekeleza sheria ndogo za vijiji.


Same (Kilimanjaro)

Wilaya ya Same imekuwa na mikakati kwa kuhakikisha jamii zinajengewa uwezo wa kulinda mazingira ikiwemo kupanda miti, kutunza vyanzo vya maji, kusimamia matumizi bora ya ardhi ili kuhakikisha kwamba changamoto ya migogoro ya ardhi inapungua.

Pamoja na zoezi la upandaji wa miti, uhamasishaji wa uanzishaji wa vitalu vya miti hufanyika kwa jamii ili kupata vyanzo vya miche kwa ajili ya kupanda. Mpaka sasa jumla ya vitalu vya miti 35 vimeanzishwa na jamii katika Kata za Hedaru, Vunta, Makanya, Maore, Kisiwani, Vumari, Mtii, Bombo na Myamba.

Kuanzia Julai 2023 hadi Julai 2024, wilaya hiyohiyo ilipanda miti 1,235,156 katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na karibu na vyanzo vya maji, maeneo ya wazi, karibu na mashamba na katika taasisi za umma.

Mbali na hilo, kuna vikundi vya ufugaji nyuki ambayo mbali na kunufaikia na mazao ya nyuki pia hutumika katika kulinda uvamizi wa wanyamapori katika misitu na vyanzo vya maji.

Muonekano wa shamba la miti mbalimbali ikiwemo ya matunda, miti rafiki wa maji na mingine ambayo hutumika katika kutunza mazingira na vyanzo vya maji kwa wananchi wa Wilaya ya Simanjiro.

Katika kijiji cha Maore kilichopo Kata ya Maore wanajamii wameunda vikundi mbalimbali kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za kulinda mazingira ikiwemo upandaji miti, utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na vikosi vya walinzi kwa ajili ya kulinda wanyamapori wanaotokana katika hifadhi ya Mkomazi ikiwemo Tembo kuvamia mashamba na makazi ya watu.

Meneja Mradi Mwandamizi wa Shirika la CARE Tanzania, Alfei Maseke ambaye ni Meneja wa mradi wa NATURE anasema lengo la mradi huo ni kuwezesha mifumo ya ikolojia kutoa huduma stahiki zinazoboresha usalama wa chakula, kuruhusu jamii kutumia rasilimali, kuongeza kipato, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.

Anafafanua kuwa mradi huo unashirikiana na wizara mbalimbali, zikiwemo Wizara ya Kilimo, Maji, Mifugo, Uvuvi, Mazingira, Serikali za Mitaa, Idara ya Maafa, Mamlaka za Serikali za Mitaa (Mufindi, Same, Kiteto Chemba na Simanjiro), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Mamlaka za Mabonde ya Maji (Wami Ruvu, Pangani).

Mkulima wa Kata ya Maore, kijiji cha Maore wilayani Same, Paulo Mtango akiwa katika shamba lake la mbogamboga anazolima kupitia kilimo cha oganiki.

Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mashirika ya Kijamii (CBO), Asasi za Kiraia zinazofanya kazi katika wilaya ambazo mradi unatekelezwa na wadau mbalimbali kama vile watafiti, wataalamu wa sera kwa ajili ya kusaidia kutengeneza sera zinazohusu EbA kama vile kilimo, mifugo, usimamizi wa maliasili na utalii na jamii katika wilaya zinazonufaika.

“Kwa pamoja, tunalenga kuweka mazingira mazuri kupitia sera na kanuni ili kuziwezesha jamii kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kujihusisha na shughuli za kuzalisha vipato huku zikihifadhi na kulinda mifumo ya ikolojia,” anasema Maseke.

Mbinu ya ulinzi wa mifumo ya ikolojia kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile upandaji miti karibu na vyanzo vya maji, mashamba na taasisi za umma, ufugaji nyuki katika maeneo ya vyanzo vya maji, kilimo hifadhi, umwagiliaji kwa njia ya matone, uvunaji wa maji, kilimo cha vitalu, ufugaji wa kuku, maeneo maalum ya malisho, hifadhi ya misitu, urutubishaji wa miti katika maeneo yaliyoharibiwa, mipango ya uvunaji wa kaboni, utalii wa mazingira, matumizi endelevu ya ardhi na utatuzi wa migogoro ya ardhi ni chachu ya mabadiliko katika jamii.

Kuwepo kwa mipango bora ya matumizi ya ardhi ya kijiji kunatoa nafasi kubwa ya kukuza matumizi endelevu ya ardhi na kusaidia urejeshwaji wa mifumo ya ikolojia.

Lakini mradi umeonyesha kuwa, gharama za utekelezaji ni ndogo, kwa mfano Sh milioni 27 zilitumika kujenga vituo vitatu vya maji wilayani Simanjiro kwa ajili ya ufugaji wa samaki, miradi ya ufugaji nyuki ni kuanzia Sh 50,000- 100,000, kufuga ng’ombe kuanzia Sh milioni 2, ufugaji wa mbuzi kuanzia Sh 150,000.

Ushiriki wa jamii katika kupanga na kufanya maamuzi, hatua za kuelekea kupunguza migogoro ya wanyamapori na binadamu imeongeza ustahimilivu kwa jamii na kuhimiza wafugaji wanaohamaham kuwa na malisho ya kudumu, hii itapunguza shinikizo katika mifumo ya ikolojia.