Vyoo bora, maji safi na usafi wa mazingira ni msingi wa ustawi wa afya ya jamii
Upatikanaji wa vyoo bora na maji safi na salama kunatajwa kama moja ya huduma bora ambazo binadamu anazihitaji katika mazingira yake ili kuweza kujikinga na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.
Hii ni kutokana kwamba huduma hizo zina mchango mkubwa katika kujenga uchumi imara kwani kuzikosa katika maeneo ya kazi, taasisi za elimu, majumbani kuna madhara makubwa katika kupunguza uzalishaji.
Kutokana na jambo hilo, Novemba 19 kila mwaka ni Siku ya Choo Duniani ambapo dunia hukumbushwa kuwa choo na huduma za maji safi ambazo hazipewi umuhimu zinaweza kuchangia ukuaji wa uchumi.
Hii ni siku rasmi ya Umoja wa Mataifa ambayo inaadhimishwa ili kuhamasisha hatua za kukabiliana na tatizo la usafi wa mazingira duniani. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu bilioni 3.5 ulimwenguni bado wanaishi bila vyoo safi na salama ikijumuisha na watu milioni 419 wanajisaidia haja kubwa maporini au sehemu nyingine tofauti na chooni.
Nchini Tanzania kulingana na Utafiti wa Demografia na Afya pamoja na Utafiti wa Viashiria vya Malaria (TDHS-MIS) wa mwaka 2022, asilimia 18.1 ya kaya zina miundombinu duni ya usafi wa mazingira, huku asilimia 9.7 ya watu wakijihusisha na kujisaidia sehemu za wazi.
Hali hii ina maana kwamba wanajisaidia katika maeneo ambayo hayana vyoo kabisa, kama vichakani, mashambani, au maeneo mengine yasiyo rasmi. Ukosefu huu wa huduma bora za usafi una athari kubwa kwa afya ya jamii, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa magonjwa yanayohusiana na maji na usafi kama vile kuhara, minyoo, na magonjwa ya ngozi.
Kwa Tanzania siku hii huadhimishwa na Serikali na wadau mbalimbali kwa kutoa elimu kupitia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari, makongamano na mitandao ya kijamii kuelezea umuhimu wa huduma hizo kwa jamii.
Wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la WaterAid wamekuwa wakishirikiana na Serikali kuhakikisha upatikanaji wa vyoo bora pamoja na huduma za maji safi za salama kwa jamii.
Moja ya malengo makuu ya WaterAid ni kuhakikisha jamii zinapata huduma endelevu za vyoo bora, usafi wa mazingira na binafsi kupitia utoaji elimu na kusisitiza mwenendo wa tabia za usafi pamoja na maji safi kwa ajili ya matumizi ya kila siku kama vile kunawa mikono kwa wahuduma wa afya kila mara baada ya kutuo huduma kwa wagonjwa kama kina mama wakati wa kujifungua, wanafunzi mashuleni katika kupata maji ya kunywa salama na kunawa lakini pia kwenye jamii kupika na kunywa.
Aidha, WaterAid inawekeza katika ujenzi wa vyoo bora kwa kufahamu kwamba upatikanaji wa vyoo bora ni sehemu muhimu ya afya na ustawi wa jamii yenye kuleta amani na maendeleo kutokana na kuepeuka magonjwa yanayozuiwa.
Haya yanajidhihirisha kupitia mradi wa “kubadili tabia siha shuleni na katika vituo vya kutolea huduma za afya’ ambao unatekelezwa na shirika hilo katika wilaya za Kisarawe mkoani Pwani na Hanang mkoani Manyara.
Mradi huo ambao unahusisha ujenzi na ukarabati wa vyoo mashuleni pamoja na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ujenzi wa miundombinu ya kuvunia maji ya mvua pamoja na mifumo ya maji ya kunywa na kunawa mikono umesaidia kwa kiasi kikubwa kubadili tabia za wanajamii wa maeneo hayo.
Katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani mradi mwingine kama huo umeleta mapinduzi makubwa katika kubadili tabia za wananchi huku ukipunguza changamoto za magonjwa kama kipindupindu, kuhara yanayotokana na ukosefu wa vyoo bora na maji safi na salama.
Ofisa Afya wa Wilaya ya Kisarawe ambaye pia ni mratibu wa mradi wilayani humo, Kalist Bushui anasema mradi huo unahusisha mbinu za kubadili tabia za wanajamii pamoja na ujenzi na ukarabati wa vyoo mashuleni na vituo vya kutolea huduma za afya.
“Katika Wilaya ya Kisarawe mradi huu unatekelezwa katika shule za msingi 30 pamoja na vituo 15 vya kutolea huduma za afya zikiwemo hospitali na zahanati,” anasema Bushui.
Anasema kwa upande wa shule mradi umefanikiwa kujenga na kukarabati vyoo na kuvifanya kuwa bora na vya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya kuvunia maji ya mvua, ununuzi wa matenki ya kuhifadhia maji, mifumo ya maji safi kwa ajili ya kunywa na kunawa mikono, kutoa vifaa vya kufanyia usafi, sabuni za kunawia mikono, vifaa vya kuchomea taka, ujenzi wa vyumba maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujistiri wakati wa hedhi pamoja na kuanzisha klabu za afya mashuleni.
Anasema katika vituo vya kutolea huduma za afya mradi umefanikiwa kujenga na kukarabati vyoo, ujenzi wa miundombinu ya kuvunia maji ya mvua, ununuzi wa matenki ya kuhifadhia maji, mifumo ya maji safi kwa ajili ya kunywa na kunawa mikono, kutoa vifaa vya kufanyia usafi, sabuni za kunawia mikono na vifaa vya kuchomea taka.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kazimzumbwi iliyopo Kata ya Kazimzumbwi wilayani Kisarawe, Christian Sinkonde anasema mradi huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya magonjwa, utoro kwa wanafunzi pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo.
“Kabla ya mradi huu hali ya usafi hususani vyoo hapa shule ilikuwa mbaya lakini baada ya kuletewa mradi huu mambo yamebadilika hivi sasa tuna vyoo bora, tuna maji ya kutosha na mifumo ya kisasa ya kunawia mikono na miundombinu inayowawezesha wanafunzi wa kike kuweza kujistiri wanapokuwa katika kipindi cha hedhi ikiwemo chumba maalumu, taulo za kike na maji safi na sabuni,” anasema Sinkonde.
Anasema mambo yaliyofanywa na mradi huo yamesaidia kupunguza magonjwa na kuwafanya wanafunzi kuhudhuiria masomo yao vizuri jambo ambalo limeongeza ufaulu na kuifanya shule hiyo kuongoza katika kata hiyo na kuwa shule bora ya 20 kiwilaya.
Ofisa Afya Wilaya ya Hanang, Reuben Mangare anasema mradi huo umekuja katika muda muafaka ambapo wilaya hiyo inatoka katika changamoto kubwa ya janga la mafuriko ya matope lililotokea mwaka jana.
“Mradi huu umetusaidia kuboresha mazingira na miundombinu ya vyoo na maji katika zahanati mbili za Laganga na Bashang kwa kujenga na vyoo kwa ajili ya wagonjwa na wafanyakazi, kuweka matanki ya maji, kichomea taka shimo maalumu la kuwekea ‘kondo la nyuma’ baada ya mama mjamzito kujifungua ukarabati wa chumba cha kujifungulia kina mama na shimo la kuweka majivu baada ya taka kuchomwa,” anasema Mangare.
Anasema kabla ya ujio wa mradi huo zahanati hizo zilikuwa na changamoto kubwa ya maji safi, wagonjwa na wafanyakazi walikuwa wanatumia choo kimoja, hakukuwa na miundombinu ya kuhifadhia taka jambo ambalo lilikuwa linahatarisha afya za wagonjwa, ndugu na wafanyakazi.
Ukarabati wa chumba cha kujifungulia kina mama Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bashang iliyopo Kata ya Wareta wilayani Hanang, Jabai Qamara anasema wanashukuru sana kwa ujio wa mradi huo kwani umewasaidia kwa kiasi kikubwa katika zahanati hiyo.
“Mradi huu umetusaidia kutujengea vyoo bora ambavyo vinahusisha vyoo vya watu wenye mahitaji maalumu (walemavu), kutuwekea mitambo ya kutibu maji na sasa tunapata maji safi ya kunywa, mifumo ya kuvunia maji ya mvua, tanki la lita 60,000 pamoja na muiundombinu ya maji ya kunawia mikono na sabuni,” anasema Qamara.
Katika Siku hii ya Choo Duniani 2024, kuna haja Serikali na wafadhili kuweka kipaumbele katika uwekezaji katika miundombinu endelevu ya maji safi, vyoo bora na usafi binafsi (WASH), hasa katika jamii ambazo hazijafikiwa na miundombinu hiuo, ili kuhakikisha kuwa huduma za usafi wa mazingira na maji zinakuwa endelevu, zinalindwa na zinapatikana kwa wote.
Upatikanaji wa usafi, usafi wa mazingira salama ni haki ya msingi ambayo lazima ihakikishwe ili kuboresha afya ya jamii, kukuza utu na kuendeleza usawa wa kijinsia kwa wote.