Wachumi walivyopendekeza maeneo muhimu kukuza uchumi

Akimwakikisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako (katikati) akiwa pamoja na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari katika ufunguzi wa Mkutano wa 27 wa utafiti jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Kulia ni Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mary O'Neill.

Baadhi ya wachumi wamependekeza maeneo kadhaa kukuza uchumi wa Tanzania ambayo ni; kuendeleza rasilimali watu, kubadilisha muundo wa uzalishaji, kuirasimisha sekta isisyo rasmi, pamoja na kuboresha nguvu kazi kupitia uvumbuzi na teknolojia ili kufikia masoko makubwa zaidi.

Maeneo mengine ni pamoja na kuboresha imani kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuchochea ukuaji na kutumia akiba iliyopo kufadhili uwekezaji.

Hayo yalielezwa katika warsha ya 27 ya mwaka ya utafiti iliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 8 mpaka 9 mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ya “Kuimarisha ukuaji wa uchumi endelevu na shirikishi kupitia mabadiliko ya kimuundo.”

Warsha hiyo pia ilishuhudia uzinduzi wa Programu ya Utafiti ya Miaka mitano ya REPOA juu ya Kubadilisha Muundo na Mwelekeo wa Maendeleo nchini. Warsha hiyo iliandaliwa na REPOA kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji na Gatsby Africa.

Akitoa mada katika siku ya kwanza ya mkutano huo, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB) wa Kanda ya Afrika, Andrew Debalen alisisitiza nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika rasilimali watu.

“Ili kufikia mabadiliko halisi barani Afrika, muundo wa uzalishaji lazima ubadilike. Uchumi wa ujuzi unakosekana. Makampuni makubwa lazima yaboreshe nguvu kazi zake kupitia uvumbuzi na teknolojia ili kufikia masoko makubwa zaidi,” anasema.

Pia anasema sekta ya miundombinu, inayohusisha umeme, barabara, reli, kuimarisha shoroba za kiuchumi na kupunguza gharama za uunganishwaji - ni muhimu.

“Katika uchumi wa kidigitali, kunapaswa kuongezwa kwa miundombinu ya kidijitali na ujuzi husika. Kuongeza thamani ni muhimu pamoja na lengo la kuanzisha eneo la biashara huru hasa katika soko la madini,” anasema Debalen.

Katika eneo la masoko, Debalen anaendelea kusisitiza haja ya uwepo mfumo wa kitaasisi utakaolifanya soko kuwa shindani kuliko lilivyo sasa.

“Mamlaka zinapaswa kufanya mabadiliko ya mfumo na kuondoa vikwazo vyote kwa sekta binafsi ili kuwezesha utoaji wa bidhaa na huduma kwa urahisi,” anasema Debalen.

“Kunatakiwa kuwe na ushirikiano wa kikanda ili kuchochea fursa za Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), kuondoa vikwazo vya ushuru na kutekeleza makubaliano ya kufanikisha biashara,” anasema.

Debalen pia aliipongeza akiba ya ndani ya Tanzania (ikiwa ni kubwa kuliko nchi nyingine za Kiafrika Kusini mwa Jangwa la Sahara) kama fursa nzuri ya kufadhili uwekezaji.

Mzungumzaji wa pili Profesa Jakkie Ciliers kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria cha Afrika Kusini anasisitiza kuwekeza katika nguvu kazi na kushauri kurasimishwa kwa sekta isiyo rasmi ili itoe mchango mkubwa katika pato la Taifa.

“Tanzania inapaswa kupata njia ya kurasimisha sekta isiyo rasmi. Kuwa na sekta kubwa isiyo rasmi ni kikwazo kikubwa kwa ukuaji. Kutumia teknolojia kunaweza kusaidia kushughulikia hilo,” anasema Profesa Ciliers.

“Sekta isiyo rasmi inatakiwa irasimishwe ili ichangie katika mapato ya Serikali na hili litawezekana kwa kutumia njia za kidijitali,” anasema.

Washiriki wa Warsha ya 27 ya mwaka ya utafiti iliyoandaliwa na REPOA wakifuatilia mada. Warsha hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.


Nafasi ya Serikali

Wakati akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako alisema Serikali imechukua hatua ya kukuza nguvu kazi kwa kuwekeza kwenye elimu kuanzia umri mdogo.

“Serikali imeongeza bajeti ya elimu na kuongeza uandikishaji ili kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya elimu. Tumejenga madarasa zaidi na kuajiri walimu zaidi na tumeongeza fedha zaidi kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kujiunga na elimu ya juu,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliongeza kuwa pia katika sekta ya afya, Serikali imeongeza ujenzi wa zahanati na hositali za wilaya na vifaa tiba ili kuboresha sekta hiyo. Pia imehakikisha kuna upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni kipaumbele cha Serikali.

“Tumewezesha Mpango wa Kuondoa Umasikini (TASAF) ambao umefikia kaya milioni moja katika vijijini 10,000 tangu ulipoanzishwa mwaka 2000 jambo lililosaidia kuzinyanyua kaya hizo na kuzindoa kwenye umasikini,” alisema.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru alieleza kwamba lengo ni kuzingatia sekta zinazoajiri watu wengi, hasa kilimo, ili kufikia matokeo endelevu na kuhakikisha kutosheleza masoko ya mazao.

“Tunapaswa kuwa makini kuhusu mabadiliko ya tabianchi, hasa kuhusiana na sekta ya kilimo. Tunapopanga maendeleo, tumekumbushwa pia kupanga kwa ajili ya mazingira,” anasema Mafuru.

Dk. Donald Mmari, Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, katika hotuba yake ya ufunguzi, alisema: “Ili kuharakisha mabadiliko ya kimuundo, tunaamini kuwa utafiti lengwa, mazungumzo na hatua za sera zitahitajika ili kuondoa vikwazo vinavyopunguza ukuaji wa uwezo wa uzalishaji na uzalishaji wa kazi nchini.”

“Kama taasisi ya kitafiti, sisi REPOA tuko tayari kufanya kazi ya uchambuzi zaidi katika maeneo yaliyobainishwa ili kutoa taarifa kwa Serikali na wadau wengine kama sehemu ya jitihada za pamoja za kuharakisha ukuaji na mabadiliko ya muundo nchini na kukuza ushirikiano wa kikanda wenye ufanisi,” anasema Dk Mmari.


Ubia sekta binafsi, umma

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Nguo na Mavazi Tanzania (TEGAMAT), Adam Zuku alishauri kufanyiwa maboresho ya ubia huo ili kuwalazimisha wawekezaji wa nje kuingia ubia/ kushirikiana na wazawa.

“Kwa sasa sheria haimpi ulazima mwekezaji kuwa na ubia na Serikali, matokeo yake ujuzi wake akiondoka anaondoka nao, anapofanya ajira anahakikisha sehemu muhimu anakuja na watu wake. Wawekezaji wengi wa kigeni wanaweka watu wao katika nafasi muhimu, lakini sio kwa kiasi kikubwa na wazawa. Lakini kwa ushirikiano, inamaanisha Serikali pia itakuwa sehemu ya kampuni hizo,” anasema Zuku.

Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa wazawa wanashirikishwa katika sekta muhimu kama vile uchimbaji madini, makaa ya mawe, gesi, au uvuvi wa bahari kuu.

“Kwa mfano, Bahrain inawataka wawekezaji wote wa kigeni wanaotaka kuwekeza nchini kuungana na wawekezaji wa ndani ili kuhakikisha ubadilishanaji wa teknolojia. Pia inadhibiti utoroshaji wa faida,” anasema.

Zuku pia alipendekeza haja ya mfumo unaowezesha wakulima kuwekeza katika kuongeza thamani ya mazao ili kuzuia kutetereka wakati wa mabadiliko ya bei.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue alisema licha ya Tanzania kuingia kwenye uchumi wa soko, bado baadhi ya Watanzania wana fikra za zamani na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

“Ingawa tumeingia katika uchumi wa soko, bado tunatumia mfumo wa uchumi wa zamani. Tunasahau kuwa uchumi huu unaweza kukua kupitia ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma. Hapo ndipo tunapopaswa kuelekea,” anasema Balozi Sefue.

Alielezea kuhusu kutoaminiana kati ya sekta ya umma na binafsi. “Kama Serikali haiamini sekta binafsi na sekta binafsi haiamini Serikali hakutakuwa na mfumo mzuri wa kujenga ushirikiano. Tumekuwa tukisema kwamba kila upande unapaswa kuwa na njia ya kusikiliza mwingine,” alisisitiza Balozi Sefue.

“Imani hiyo tumesema kwamba lazima kuwe na mifumo na taratibu za majadiliano ya kila mmoja kumsikiliza mwenzake, sio kila mmoja kuja kwenye mazungumzo kutetea msimamo wake na masilahi yake,” alisema.

Balozi Sefue pia alishauri mfumo unaotumika kwenye uzalishaji wa sukari katika viwanda vya sukari, utumike na kwenye uzalishaji wa pamba.

“Kwa nini kwa mfano tumeweza kwenye sukari lakini bado tuna changamoto kwenye pamba? ninachojua ni kwamba mfumo unaotumika Kilombero ni ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi na sekta ya umma,” alihitimisha.