Wataalamu wanawake wa Yara wachangia usalama wa chakula, kipato kwa wakulima

Kutana na Mwajuma Mwangu na Veronica Rusagira, wataalamu wa kilimo ambao wanajinasibu kutoogopa na kujifunga kibwebwe kushiriki katika kukuza kilimo nchini.
Wanawake hawa wanafanya kazi katika kampuni ya Norway inayotengeneza na kusambaza mbolea na kemikali nyingine za kilimo, Yara, tawi la Tanzania. Ni wanawake pekee katika nyadhifa zao katika kampuni hiyo.
Wakiongea na Mwananchi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani (Machi 8, 2023), Mwajuma na Voronica wanasema wana shauku kubwa ya kusonga mbele katika shughuli waliyoichagua.
Wataalamu hao wanatumaini kuwa mfano kwa wanawake wengi vijana wajiunge na shughuli za kilimo. Wanaamini kuwa mchango wa wanawake katika kuleta utoshelevu wa chakula na kupunguza umaskini ni wa muhimu. Wanataka kuona wanawake wengi wakiwa mstari wa mbele katika mnyororo wa thamani wa kilimo.
Veronica Rusagira
Akiwa mhitimu wa Chuo cha Kikuu cha Kilimo cha Sokonine (SUA), Veronika alijiunga na Yara Tanzania mwaka 2019 baada ya kufanya kazi katika kampuni nyingine kwa muda mfupi. Wakati huo alikuwa akisimamia miradi ya kilimo cha bustani katika Mkoa wa Iringa, lakini sasa anasimamia shughuli za Yara Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani na Zanzibar.
Kazi yake ni kuhakikisha wakulima wanapata mavuno ya kutosha ili wajipatie kipato kizuri kwa mauzo ya mazao kupitia mipango mizuri ya kilimo cha kitaalamu kama vile matumizi sahihi ya mbolea na virutubisho vingine.

Veronica amekulia shamba na tangu akiwa na umri mdogo alijifunza thamani ya kufanya kazi kwa bidii na umuhimu wa kilimo katika kuendesha maisha.
“Kazi yangu inasukumwa na dhamira ya kutaka kuona wakulima wanafanikiwa. Ni kazi nzuri. Fikiria inasisimua kiasi gani kuwasaidia wakulima na nchi yako kuwa na chakula cha kutosha,” anasema.
Anasema ni muhimu kukuza usawa wa kijinsia katika sekta ya kilimo na uelewa wa fursa mbali mbali zinazopatikana kwa wote.
“Ni ukweli usiofurahisha kwamba wasichana wengi wanakwepa kuingia kwenye kilimo kwa sababu wanaona kilimo ni taaluma ya wanaume,” anasema.
Anatoa wito wa kuanzishwa kwa programu zinazowalenga wasichana shuleni na wanawake vijana, kukuza ushiriki wa wanawake katika kilimo na kupinga upofu wa kijinsia na mila zinazowakatisha tamaa wanawake.
Veronica anashukuru kwamba akiwa Yara anapata msaada na ushirikiano unaohitajika kuvuka malengo yake ya kazi na kitaaluma. Uvumilivu wa wazazi wake ndio uliomsukuma kutumia utaalamu wake kusaidia kuleta matokeo chanya kwenye maisha ya wakulima na kuchangia katika maendeleo endelevu.
Kwa mfano, anazungumzia furaha aliyoipata kushuhudia mafanikio makubwa ya mkulima aliyekuwa akimsimamia kupata Sh200 milioni kutoka kwenye mavuno yake ya nyanya. “Nilishawishika sana na fursa zilizoko kwenye kilimo katika kubadili maisha ya mamilioni ya wakulima na jamii zao,” anasema.
Mwajuma Mwangu
Mwajuma ambaye pia ni mhitimu wa SUA alikuwa siku zote na udadisi mkubwa kuhusu kilimo.
“Mshawishi wangu mkubwa alikuwa mjomba wangu. Alikuwa anapata fedha nyingi kupitia kilimo na alinishawishi nikasomee sayansi ya uchumi wa kilimo baada ya kuona udadisi wangu katika masuala ya kilimo,” anasema.

Baada ya kufanya kazi na kampuni mbili za kahawa kwa miaka minane, alijiunga na Yara mwaka 2021 na tangu wakati huo amekuwa akisimamia shughuli za Yara katika mkoa wa Songwe.
“Yara nimepata mazingira yanayofaa kuchangia kwa ubora wote utaalamu wa kilimo yanayogusa maelfu ya wakulima kwa kufanya kazi karibu na Serikali, wakulima na washirika wengine.”
Mwajuma alikulia katika kijiji kidogo ambapo kahawa ilikuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha ya jamii yake. Hilo lilimfanya hata aamue kusomea Shahada ya Uzamili katika Uchumi na Sayansi ya Kahawa.
“Ndoto yangu ni kuona vijana wanafanikiwa kupitia kilimo. Nafasi ya kufanikiwa Tanzania ni kubwa, na kufanya kazi na watoa huduma kama Yara kunaweza kufanikisha zaidi.”
Anasema kilimo ni muhimu kwa maendeleo endelevu. Anatumia muda mashambani, akifanya kazi sambamba na wakulima, na kuwapa mipango mizuri ya kilimo na ufumbuzi kutoka Yara ambao hutolewa kulingana na mahitaji pekee ya kila mkulima.
“Wanawake wengi zaidi watiwe moyo ili kujihusisha na kilimo na kushinda ubaguzi wowote wa kijinsia, hata kwa wanataaluma kama mimi. Kama wanawake, ni lazima tuwe na imani na uwezo wetu na tuwe tayari kutoa mawazo yetu. Unapopewa fursa lazima uoneshe unaweza kufanya, hakuna tusichoweza kufanya kama tunaiweka akili yetu katika hilo,” anasema huku akiishukuru kampuni ya Yara Tanzania kwa kumruhusu kujaribu na kuwa mbunifu katika kutoa huduma za kitaalam. Mkurugenzi Mkuu wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo, anasema kampuni ya Yara inashirikiana na serekali na wadau mbalimbali kuwafikishia wakulima bidhaa na huduma mbalimbali ili kuwanyanyua kimaisha kupitia kilimo.
“Hapa Yara tuna furaha kwamba wataalam wetu wanaishi kivitendo mpango wetu wa kuilisha na kuilinda dunia, huku tukitoa ufumbuzi wenye tija kwa kilimo na mazingira,” alisema Mr Odhiambo.