World Vision Tanzania na miaka zaidi ya 40 ya huduma bora za afya za watoto

 Ili kuhakikisha watoto, wanabaki na afya njema shuleni; World Vision Tanzania iliwezesha wanafunzi 37,714 kupata huduma za msingi za maji. Shule 32 zilipata huduma ya maji kupitia vituo 64 vya usambazaji, matanki 8 ya kuvuna maji ya mvua yalijengwa shuleni katika maeneo ambayo hayana mifumo ya usambazaji wa maji ya bomba.


Muktasari:

Siku ya Afya Duniani (WHD), inayoadhimishwa kila mwaka Aprili 7, inaadhimisha kum­bukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 1948 na kila mwaka huangazia masuala mahususi ya afya ya umma.

Siku ya Afya Duniani (WHD), inayoadhimishwa kila mwaka Aprili 7, inaadhimisha kum­bukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 1948 na kila mwaka huangazia masuala mahususi ya afya ya umma.

Mbali na kuangazia jitihada za kufikia ajenda ya “Afya kwa wote,” ambayo ndiyo kaulimbiu ya mwaka huu, WHO itaadhimi­sha miaka 75 ya kuboresha afya ya umma chini ya kaulimbiu hiyo.

Si WHO pekee huiadhimi­sha siku hii muhimu, World Vision Tanzania (WVT) ambayo ni asasi isiyo ya kiserikali ya maendeleo, misaada na utetezi ya Kikristo (NGO) yenye lengo la kuchochea maendeleo kamili na endelevu kwa ustawi wa watoto ndani ya familia na jamii hususan walio hatarini zaidi, inaisherehekea pia kwa kujikita katika kuboresha ustawi wa watoto kupitia jitihada mbali­mali za kimageuzi zinazolenga masuala ya kiroho, kifikra, kisaikolojia na kiuhusiano.

Kwa mwaka huu 2023, tumekabidhi majengo mawili ya wodi ya wazazi katika zahanati mbili, nyumba moja ya watumishi na vifaa tiba vya zahanati saba, mashimo ya kondo na vichomeo kwa vituo viwili vya Afya vya Korogwe.Kwa zaidi ya miaka 40, World Vision imekuwa ikisaidia vituo vinavyotoa huduma za afya za msingi (ikiwa ni pamoja na IMCI - Usimamizi Jumuishi wa Magonjwa ya Utotoni, Pro­gramu Iliyoboreshwa ya Chanjo (EPI); na huduma za afya ya uzazi, afya ya uzazi kwa akina mama na lishe kwa watoto wachanga.

Inafanya kazi pamoja na wiz­ara ya afya kuboresha upati­kanaji wa huduma za afya na lishe zinazojumuisha ujenzi, ukarabati na usimamizi wa vituo vya afya vya umma, kuwa­jengea uwezo watumishi wa afya miongoni mwa mambo mengine katika programu 42 za maeneo zinazoendeshwa katika mikoa 16 ya Tanzania Bara.

Kuelekea katika maadhi­misho ya Siku ya Afya Duniani, gazeti la Mwananchi limefanya mahojiano na Kiongozi wa Timu ya Ufundi wa World Vision Tanzania, Elizabethproscovia Ndaba kuhusiana na shughuli za taasisi, mafanikio yake pamoja mwelekeo wao wa siku za usoni.

Swali: Je, WVT inatekelezaje kwa vitendo kauli mbiu ya Siku ya Afya duniani: Afya kwa Wote?

Kwa kuwa shirika la kijamii, WVT inatumia mbinu mbalim­bali za utekelezaji wa programu ambazo sio tu za gharama nafuu lakini pia zinaupa jamii umiliki wa programu, hivyo, kuhakiki­sha uendelevu wa programu. Mbinu ya Upazaji Sauti na Vitendo ni mbinu ya uwajibikaji kwa jamii na utetezi wa ngazi ya mashina ambayo inalenga kushughulikia huduma muhimu zisizotosheleza kwa kubore­sha uhusiano kati ya jamii na Serikali, na kuwezesha jamii kuiwajibisha Serikali inapobidi.

Katika mwaka wa fedha 2022, chini ya jalada la afya na lishe, World Vision ilipanga kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ya jamii 1200, kusaidia programu ya uongezaji vitamini A kufikia watoto 138,310 wenye umri wa miezi 6-59. Tuliweza kutoa mafunzo kwa wafan­yakazi wa afya ya jamii 1044 na kufikia watoto 134,147 katika maeneo ya mradi huo.

WVT pia ilisaidia watoto 2,587 kupatiwa vyeti vya kuza­liwa na watoto 3,290 walio­sajiliwa kupata bima ya afya kusaidia matibabu yap dhidi ya magonjwa. Miradi kama hiyo huongeza mahitaji ya huduma za afya ya uzazi, afya ya uza­zi wa akina mama na watoto wachanga na pia huchangia katika kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto chini ya umri wa miaka 5 kupitia chanjo.

SwalI: WVT inachangiaje kati­ka maendeleo ya sekta ya afya nchini?

Ushahidi unaonyesha kuwa mifumo ya afya inayoendeshwa na mbinu ya huduma ya afya ya msingi (PHC) ndiyo njia bora na ya gharama nafuu ya kusoge­za huduma za afya na ustawi karibu na watu. World Vision Tanzania inaamini katika ush­irikiano na upigiaji chapuo matokeo mapana kama mkakati wa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya na hatimaye kuhakikisha ustawi wa watu.

Katika utekelezaji wa mka­kati wa mwaka wa fedha 21/22, kongano la Kagera lilitenga fedha kwa ajili ya kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika mkoa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa afya. Kituo cha afya cha Rubale amba­cho kilikuwa kikitoa huduma za afya ya uzazi na watoto katika chumba kimoja hata baada ya kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya tangu 2013 hadi sasa, kimeweza kuongeza idadi ya akina mama wanaojifungua kutoka 20 kwa mwezi mwaka 2019 hadi zaidi ya 54 kwa mwezi mwaka 2022.

Tulisaidia ujenzi wa vyum­ba vitatu vya kulaza wagon­jwa vyenye vitanda nane kila kimoja, vyumba vya kujifun­gulia vyenye vitanda viwili, kituo cha kulelea wazee, na chumba cha kuhifadhia vifaa na cha kusafisha uchafu. Maz­ingira mazuri ya kujifungulia katika kituo hicho yalichangia kuongezeka kwa idadi ya akina mama wajawazito wanaohud­huria kituo hicho. Fedha za ziada kupitia DHFF kutoka kwa Serikali ziliwezesha ujenzi wa ziada wa jengo la upasuaji.

Katika mwaka huo wa fedha, Shirika la World Vision kupitia Programu ya Eneo la Kwam­sisi lililopo Korogwe, lilisaidia ununuzi wa vifaa tiba mbalim­bali vitakavyotumika katika zahanati zote za Kwamsisi.

Vifaa hivyo vya matibabu viligharimu Sh37 Milioni na vitahudumia watu wazima wapatao 14,946 wakiwemo watoto 7,578.

Juhudi hizi zote zinalenga kusaidia juhudi za serikali kuboresha afya na ustawi wa wananchi. Vilevile, jitihada kama hizo zimefanyika mkoani Kigoma ambapo tulikamilisha ujenzi wa wodi ya wazazi ya Nyamtukuza na kitengo cha wagonjwa wa kutwa cha Chura­zo (wanaokuja na kuondoka) katika eneo la Nyaronga.

Pia, katika kuchangia juhu­di za Serikali za kupambana na kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na hali duni ya usafi na maz­ingira, na kuhakikisha kuwa taasisi kama shule na hospi­tali zinakuwa na miundombinu mizuri ya kujikinga na magon­jwa ya kuambukiza kama vile Uviko-19 na magonjwa mengine ya milipuko. , tulijenga vituo viwili vya kunawia mikono kati­ka zahanati ya Mkalamo, kijiji cha Kwamsisi, iliyogharimu Sh30 Milioni zinazotarajiwa kunufaisha jumla ya wakazi 1778 wakiwemo watoto 830.

Kwa mwaka wa fedha wa 21/22, vituo 14 vya huduma za afya vilipata maji safi, vituo 17 vya kutolea huduma za afya vilipata huduma za usafi wa mikono baada ya ujenzi wa vituo vya kudumu vya kunawia mikono kukamilika.

Matundu 24 ya vyoo vya matofali vilivyotenganishwa kwa uzio kwa kuzingatia jinsia vilijengwa katika vituo 11 vya afya. Haya yote yameboresha utoaji huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Swali: Je, WVT inaionaje sekta ya afya?

Kumekuwa na uboreshaji mkubwa katika sekta ya afya ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita, na hii inajumuisha upatikanaji wa huduma maalu­mu katika vituo vya ngazi ya chini vya afya, vifaa tiba na bidhaa, kuongezeka kwa rasili­mali watu katika sekta ya afya, kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za afya kupitia bima na miundombinu.

Swali: Changamoto na njia ya mbele ni zipi?

Suala muhimu zaidi katika huduma za afya kwa sasa ni gharama kubwa ya huduma. Zaidi ya asilimia 40 ya Watan­zania wetu hawana uwezo wa kumudu huduma za afya. Gharama za huduma za afya hubadilisha tabia ya watu, huku wengi wakiacha kuonana na daktari wanapohisi wagonjwa au kutokuhudhuria hospitali moja kwa moja kutokana na mzigo mkubwa wa magonjwa unaoikabili sekta ya afya.

Tabia kama hizo zinaweza kusababisha matatizo makub­wa ya kiafya, kuongeza ghara­ma za huduma na hatimaye kuibebesha mzigo mzito sekta ya afya.

Suluhisho la hili linaweza kuwa kupunguza gharama za huduma za afya, kupunguza viwango vya malipo ya bima na kuweka gharama elekezi kwa huduma za bima zitolewazo na taasisi binafsi na muhimu zaidi kuungana kusaidia mpango wa sasa wa Serikali katika kuhakik­isha huduma ya afya kwa wote ambayo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa matibabu kwa jamii.