WWF: Tutafute maendeleo na tuhifadhi mazingira ili yatuhifadhi

Muktasari:

Mazingira bora ni muhimu kwa afya na ustawi wa binadamu. Binadamu na mazingira wana uhusiano wa moja kwa moja ambao kila mmoja ili aweze kustawi anamtegemea mwenzake.

Mazingira bora ni muhimu kwa afya na ustawi wa binadamu. Binadamu na mazingira wana uhusiano wa moja kwa moja ambao kila mmoja ili aweze kustawi anamtegemea mwenzake.

Kwa bahati mbaya, binadamu aidha katika kutafuta maendeleo au shughuli nyingine ameharibu mazingira kwa kiasi kikubwa sana. Amekata miti, amechafua na kuharibu vyanzo vya maji na kuua wanyama pori kwa idadi isiyo kithirika.

Katika ripoti ya WWF ya The Living Planet Report ya mwaka 2018 wataalmu wameeleza kuwa kizazi cha sasa cha binadamu ndio kimeshuhudia uharibifu wa hali ya juu kabisa wa mazingira, lakini pia ndio kizazi ambacho jukumu kubwa la kubadilisha hali hii ya uharibifu linakiangalia.

Kwa maana kwamba, kama kizazi hiki hakitachukua hatua kuboresha hali ya mazingira basi tutakuwa tunaelekea katika kuzama kabisa kwa dunia. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kwa kipindi cha miaka 40 tu zaidi ya asilimia 60 ya wanyamapori wametoweka. Na pia zaidi ya theluthi mbili za maji baridi zimepotea.

Maendeleo ni kitu cha muhimu na ilimradi binadamu anaendelea kuwepo basi na maendeleo yatakuwepo. Swali mtambuka kwa wakati huu ni je, tufanye nini sasa kuhakikisha tunapata maendeleo na tunahifadhi mazingira ili yatuhifadhi?.

Kwa miongo kadhaa sasa WWF imekuwa ikijihusisha na uhifadhi wa mazingira katika nchi zaidi ya 100 duniani kote, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo WWF imekuwa ikifanya kazi kwa miaka zaidi ya ishirini sasa. Dhima ya WWF ni kuwa na dunia ambayo binadamu na viumbe wengine wanaishi na kustawi pamoja.

Ili kuifikia dunia hiyo, WWF imekuwa ikifanya kazi katika maeneo mbalimbali ya misitu huku kukiwa na mchango mkubwa wa kuhifadhi misitu kama ya Udzungwa, Usambara hata misitu ya hifadhi ya Pugu, Kazimzumbwi na Vikindu kilomita chache tu kutoka jijini Dar es Salaam.

Uhifadhi wa bahari, mabonde ya maji baridi, wanyamapori na hata uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala. Haya yote yamekuwa yakitekelezwa kwa ushirikiano mkubwa na Serikali na taasisi zake husika, asasi za kiraia na jamii zinazoishi pembezoni kwa maeneo husika.

WWF imewekeza sana katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira. Elimu hii imekuwa ikitolewa kwa misingi kdhaa waliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa vijana na “Earth Hour” ambayo kwa lugha rahisi ya Kiswahili tunaweza kusema ni “Wasaa wa Mazingira au saa ya dunia”.

Earth Hour ni nini?

Hili ni vuguvugu kubwa kabisa la kimazingira la kijamii linalolenga kupaza sauti za wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kila mmoja kufanya kitu kama sehemu ya kuonyesha kwake kuyajali mazingira.

Ikianzia mjini Sydney nchini Australia miaka kumi na tatu iliyopita, Earth Hour wakati huo ililenga kutumia dakika sitini kuzima umeme ili kusaidia kupunguza matumizi ya maji yanayozalisha umeme huo. Zoezi hili linafanyika kila Jumamosi ya mwisho ya mwezi Machi. Kampeni kubwa ilifanyika na siku hiyo karibu mji wote wa Sydney saa mbili na nusu mpaka saa tatu na nusu ulikuwa giza kabisa. Nchi nyingi zenye ofisi za WWF zilipokea wazo hili na mwaka uliofuta miji mingi zaidi ikashiriki. Mpaka hivi leo, miji zaidi ya 190 hata katika nchi kusiko na ofisi za WWF wanaadhimisha Earth Hour kila Jumamosi ya mwisho wa Mwezi Machi.

Lengo nyuma ya Earth Hour limeendelea kuboreshwa na sasa siku hii mbali ya watu kuzima taa saa mbili na nusu mpaka saa tatu na nusu usiku pia hutumika kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mazingira, kuchukua hatua kwa vitendo na kufanya shughuli za uhifadhi wa mazingira lakini pia kupaza sauti kwa Serikali za nchi na viongozi wa kidunia wasaidie katika kufanya maamuzi yatakayowezesha uhifadhi wa mazingira ili hatimaye tuwe na dunia rafiki kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine.

Dunia imeshuhudia maamuzi muhimu yakifanywa kutokana na tukio hili la Earth Hour kwa mfano nchini Uganda wamefanikiwa kuanzisha msitu wa ekari 2,700 ujulikanao kama msitu wa Earth Hour.

Nchini Tanzania chini ya Earth Hour WWF imekusudia kurejesha misitu ya Hifadhi ya Pugu, Kazimzumbwi na Vikindu katika hali yake asili kwa kupanda miti na kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mazingira lakini pia kuwezesha vikundi vidogo vya wajasiriamali kwa elimu ya kutengeneza majiko sanifu na mitaji ya kuwezesha biashara zao.

Mpaka hivi leo miti zaidi ya 45,000 imepandwa msituni Kazimzumbwi na mingine zaidi ya 1000 katika msitu wa Pugu. Shule na taasisi za kijamii kama hospitali zimewekewa huduma za umeme wa nishati ya jua na zaidi elimu imeendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo shule, halmashauri za Wilaya Kisarawe, Mkuranga na Kilwa pamoja na Kanda ya Ziwa, WWF imeendelea kuadhimisha siku hii ya Earth Hour kwa ukamilifu hapa nchini.

Ikianza kwa kuangazia mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha kuchukua hatua miaka 13 iliyopita, mtazamo wa dhima nzima ya Earth Hour umeendelea kubadilika na kuanzia mwaka 2018 lengo limekuwa kuchochea mazungumzo juu ya mabadiliko ya tabianchi lakini pia kuhamashisha hatua muhimu kuchukuliwa hasa na viongozi wa nchi na wa dunia kwa ujumla ili kuiokoa dunia na hatari ya kuelekea kwenye uharibifu mkubwa usiomithirika wa dunia ambao bila kuchukua hatua miaka michache tu ijayo utapelekea dunia na viumbe vilivyomo kupotea kabisa.

Lengo hili ni kusaidia lengo namba 1 la Aichi ambalo linataka watu wengi kadri iwezekanavyo kufahamu madhara ya uharibifu wa mazingira lakini pia kufahamu nini wanatakiwa kufanya na kuchukua hatua na WWF imekusudia kufikia watu bilioni moja duniani ifikapo mwisho wa mwaka huu na ujumbe huo.

Kwa nini 2020?

Mwaka 2020 ni mwaka muhimu sana kwa mazingira dunia kwa sababu muda si rafiki sana haswa linapokuja suala la kubadilisha mwelekeo wa ustawi wa jamii na mazingira.

Dunia inapoteza uasili wake kwa kasi kubwa huku uchafuzi wa hewa ukiongezeka kwa asilimia 90 katika miaka michache tu. Huu ni mwaka wa kufanya maamuzi na mabadiliko muhimu. Ni nia ya wanamazingira kubadilisha hali ya dunia ifikapo mwaka 2030, hivyo ni lazima hatua zianze kuchukuliwa sasa. Mwaka 2020 ni mwaka ambao kuna matukio mengi muhimu ya kimazingira. Matukio hayo ni kama yafuatayo:-

1.      Umoja wa Mataifa unafikisha miaka 75 na kutakuwa na mkutano mkubwa utakaowakutanisha viongozi wote wa juu dunia mwezi Septemba. Hii ni nafasi muhimu kwa viongozi hao kujadili hatma ya dunia na kukubaliana kwa mkakati endelevu wa kubadilisha hali ya uharibifu wa mazingira dunia.

2.     Umoja kwa mataifa kupitia mkutano wake wa Convention on Biological Diversity (COP-15) huko Beijing mwezi Oktoba watakuwa wakitengeneza na kukubaliana juu ya mkakati wa miaka kumi wa kimazingira. Watajadili hali halisi ilivyo sasa na kuweka malengo muhimu ya kurekebisha hali ya dunia kwenye suala la mazingira.

3.     Mkutamo mwingine muhimu wa Desemba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mfumo wa mabadiliko ya tabianchi (United Nations Framework Convention on Climate Change, UNFCCC) pia utawakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira na viongozi kujadili na kila nchi itapata nafasi ya kuwakilisha mpango mkakati wao wa kufikia makubaliano ya mkutano wa Paris.

4.     Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) yanafikia ukomo wake mwaka 2030 huku baadhi ya mikakati midogo midogo 21 ikifikia ukomo mwaka huu wa 2020. Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2019 inaonyesha mengi ya malengo haya hayatafikiwa kwa ukamilifu ifikapo mwaka 2030 na ndio maana ipo haja ya kuyatazama upya na kupanga mikakati madhubuti ya kufika kwenye dunia tuitakayo. Ukiyaangalia malengo haya mengi ni kimazingira kama maji safi (6), nishati safi na nafuu (7), mabadiliko ya tabianchi (SDG 13), matumizi na uzalishaji endelevu (12), maisha chini ya maji (14), maisha juu ya ardhi (15).

 

Earth Hour 2020

Earth Hour kwa miaka yote imekuwa ni shughuli inayowajumuisha watu wengi kwa pamoja kusherehekea zawadi nzuri tunazozipata kutoka kwa mazingira kama maji, hewa, nishati, dawa na hata uhai wenyewe na kuhimizana kuchukua hatua za kuendelea kuilinda dunia.

Kufuatia hali ya taharuki duniani kote ya maambukizi ya virusi vya COVID-19 mtazamo wa maadhimisho ya Earth Hour umebadilika kabisa, badala ya shamrashamra ambazo huambatana na siku hii tutakuwa na shughuli mbalimbali za mtu mmoja mmoja na shughuli za kimtandao zaidi.

Tunawahamisisha Watanzania kila mmoja alipo kufanya kitu japo kimoja katika kusaidia kuilinda dunia na mazingira yake. Hii yaweza kuwa kupanda miti, kusafisha mazingira au kutoa elimu kwa familia na ndugu juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kuchukua hatua muhimu katika kuhifadhi mazingira.

Waweza pia kuzima taa kwa saa moja kuanzia saa mbili na nusu usiku mpaka saa tatu na nusu. Kwa wale wataalam wa mitandao huu ndio wakati wa kuitumia vyema na kuleta matokeo chanya katika dunia yetu, ongea na marafiki zako kwa Instagram au Face book live na waweza kututag wwftanzania.

Huu ndio muda wa kuchukua hatua na kila mmoja wetu analo jukumu kwani kama alivyowahi kusema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa zamani, Ban Ki Moon hakuna Plan B na wala hakuna sayari B ambayo tutaweza kuhamia tukiharibu hii.

Ujumbe wetu mwaka huu unasema “Nature Matters” kwa maana kuwa uasili na kila kilichomo ni muhimu kwa kila mmoja wetu. #Connect2Earth.

“Earth Hour inatakiwa kuwa kila siku, hasa mwaka huu kwani hitaji la kuilinda dunia yetu ni kubwa kuliko wakati wowote katika historia.  Tunahitaji kupaza sauti zetu kwa ushirikiano kwa ajili ya dunia. Wakati tunapambama na maambukizi ya Corona tukumbuke pia kuungana kuihifadhi dunia yetu. Ninawahamasisha kila mmoja mahali alipo kuchukua hatua na huenda kujiwekea mkakati binafsi wa kuhifadhi mazingira. Tulindane na kwa pamoja tuyalinde makazi yetu duniani kwa usalama na uwajibikaji,” anasema Amani Ngusaru Mkurugenzi Mkazi WWF Tanzania.

Anasema tumekuwa na wadau kadhaa katika kuadhimisha Earth Hour na mwaka huu kwa mara ya kwanza tumeungana na Vodacom Foundation Tanzania ambapo huko Dodoma tumepanda miti elfu thelatini na tano mpaka sasa na lengo letu ni kupanda miti elfu sabini.

 “Watu wanapoamua wenyewe kuchukua jukumu duniani kote kama Earth Hour hapo ndipo hupatikana mafanikio ya dhati. Tunafurahi kuwa sehemu ya Earth Hour mwaka 2020 nchini Tanzania, tunawatia moyo Watanzania hasa katika kipindi hiki kigumu kuwa tutafanikiwa tu tukiungana na kushirikiana kila mmoja kwa nafasi yake ili tupate matokeo tunayoyataka kimazingira. Tunawahamasisha wafanya maamuzi, biashara na kila mmoja kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko,” wanasema Vodacom.