Miaka 13 ya EnDev: Mapinduzi ya nishati safi yanavyobadili maisha ya mamilioni ya Watanzania
Mzalishaji bingwa wa majiko kutoka Misungwi, Mwanza, Elizabeth Mussa akionyesha Jiko Matawi. Kupitia mkakati wa “5I’s” wa EnDev, zaidi ya mafundi 120 wamegeuzwa kuwa wajasiriamali wa kitaalamu, wakisaidia kuuza karibu majiko milioni moja nchini.
Kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja sasa, mapinduzi ya kimyakimya lakini yenye nguvu kubwa yamekuwa yakishika kasi katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji nchini.
Kuanzia kando ya Ziwa Victoria hadi nyanda za juu za Mvomero, namna familia zinavyopika na kuangaza nyumba zao imebadilika kwa kiasi kikubwa, shukrani kwa programu ya Energising Development (EnDev).
Programu hii inayofadhiliwana wadau mbalimbali imethibitisha kuwa nishati safi si kwa ajili ya watu wa mjini pekee, bali ni msingi wa maendeleo ya Taifa zima.
Tangu ilipozinduliwa mwaka 2013 ikitekelezwa na SNV Tanzania kwa uratibu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Shirika la Biashara la Uholanzi (RVO), EnDev ililenga kutatua changamoto mbili kuu: utegemezi wa mbinu duni za kupikia na ukosefu wa umeme maeneo ya vijijini.
Wanufaika wa nishati safi wakijadili jambo kuhusu Jiko la Umeme (EPC). Jiko hili wamelipata kupitia mfumo wa mikopo wa programu ya EnDev inayotekelezwa na SNV Tanzania kwa kushirikiana na SACCOS.
Wakati ikitimiza miaka 13 ya utekelezaji wake ifikapo Juni 2026, programu hii imeacha alama isiyofutika kwa karibu Watanzania milioni mbili ambao sasa wanavuta hewa safi na kufurahia faida za nishati safi ya kupikia.
Kuondoa matumizi ya nishati zisizo safi katika kaya
Kwa vizazi vingi, “mafiga matatu” ndiyo yalikuwa kimbilio la jikoni nchini, lakini yalikuwa na athari kubwa za kiafya na mazingira. Mamilioni ya kaya zilitegemea kuni na mkaa, hali iliyowaweka wanawake na watoto kwenye hatari ya kuvuta hewa yenye sumu, huku wakipoteza saa nyingi kutafuta nishati hizo.
Suluhisho la EnDev lilikuwa ni Jiko Matawi, jiko sanifu la bei nafuu linalozalishwa nchini ambalo hupunguza matumizi ya nishati kwa asilimia 40.
Likiuzwa kati ya Sh 5,000 hadi Sh 25,000, jiko hili limebuniwa kumudu mfuko wa familia zenye kipato cha chini huku likiokoa fedha nyingi zinazotumika kwa ajili ya kununulia mkaa na kuni.
Tofauti na kutoa majiko bure, EnDev ilitumia mkakati wa “5I’s” (Utambuzi, Uanzishaji, Ulezi, Uwekezaji, na Kujitegemea). Programu hiyo iliwatambua mafundi wa ndani na kuwageuza kuwa wajasiriamali wa kitaalamu, ikiwapa mafunzo ya biashara navitendea kazi.
Mmoja wa wanufaika ni Fatma Ramadhani, mbunifu wa majiko mwenye umri wa miaka 70 kutoka Mvomero, ambaye kupitia kipato na motisha ya EnDev, amefanikiwa kujenga nyumba imara inayotumika pia kama karakana na stoo.
Leo hii, Fatma ni mmoja wa wazalishaji zaidi ya 120 katika mikoa 20 ambao kwa pamoja wameuza karibu majiko milioni moja.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme
Kadiri soko la majiko sanifu lilivyokua, EnDev ilielekeza nguvu kwenye upishi wa kutumia umeme (e-cooking) tangu mwaka 2022. Kwa kushirikiana na SACCOS na kutumia mifuko ya mikopo (Revolving Loan Funds), programu imefanya majiko ya umeme (EPCs) kupatikana kwa urahisi zaidi.
Wakina mama wakiwa wameshika bidhaa za sola walizozipata kupitia program ya EnDev inayotekelezwa na SNV Tanzania kwa kushirikiana na kampuni za sola wakati wa program ya sola ya RBF.
Hadi sasa, zaidi ya majiko 9,000 ya umeme yameuzwa, hatua inayoelezwa kuwa muhimu katika kulinda misitu ya Tanzania na kuondoa kabisa uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba.
Kuleta mwanga maeneo ya vijijini
Wakati EnDev inazindua mkakati wake wa matumizi ya nishati ya jua (solar) mwaka 2014, upatikanaji wa umeme vijijini ulikuwa asilimia 21 pekee, huku familia nyingi zikitumia vibatari vyenye hatari na gharama.
EnDev ilianzisha mfumo wa ufadhili wa kutoa motisha baada ya matokeo (RBF), ambapo kampuni binafsi zililipwa baada ya kuthibitika kuwa zimefunga mifumo ya sola katika nyumba za wananchi wa vijijini.
Mfumo huu ulichochea ushindani na kuyafikia maeneo yaliyodhaniwa kuwa hayana faida kibiashara. Mkurugenzi Mtendaji wa Zola Electric, Xavier Helgesen, anasema motisha hiyo ilisaidia kampuni yake kuwafikia wateja zaidi ya 150,000 nchini. Kwa ujumla, miradi ya sola imewafikia mamia ya maelfu ya watu na kutengeneza ajira zaidi ya 780.
Uwezeshaji wa wanawake na mazingira
Usawa wa kijinsia umekuwa mhimili wa EnDev. Katika sekta ya upishi, asilimia 54 ya wazalishaji wa Jiko Matawi ni wanawake. Katika sekta ya sola, mpango huo umetengeneza ajira za kudumu 271 kwa wanawake, nyingi zikiwa katika nafasi za kitaalamu.
Vilevile, kupunguza mahitaji ya mkaa na kuni kumesaidia kuhifadhi bioanuwai ya Tanzania, kulinda vyanzo vya maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Mustakabali wa baada ya 2026
Wakati programu hii ikiadhimisha miaka 13 ya mafanikio mwezi Juni 2026, inatoa taswira ya matumaini kwa maendeleo endelevu ya baadaye. Mradi huu umeonyesha kuwa mbinu zinazotegemea soko, ambapo sekta binafsi na wajasiriamali wazawa wanawezeshwa ni endelevu zaidi kuliko misaada ya kawaida.
Hata hivyo, kazi bado haijaisha. Mamilioni ya Watanzania bado hawana huduma ya nishati safi na soko la vifaa vya kupikia vinavyotumia nishati ya umeme bado liko katika hatua za awali za maendeleo.
Kutokana na hilo, mwelekeo sasa ni kuendeleza mifumo hii ambayo mafanikio yake yameanza kuonekana, kusistiza matumizi ya nishati yenye tija kama pampu za maji zinazotumia sola kwa wakulima, pamoja na kuunganisha taarifa za kidijitali ili kujiandaa na soko la kimataifa la kaboni.
EnDev ambao unatekelezwa kwa ushirikiano na wafadhili mbalimbali umeweka msingi imara, sasa ni jukumu la Serikali, sekta binafsi na washirika wengine kuendeleza safari hii ya mageuzi ili kuhakikisha hakuna mtanzania anayeachwa nyuma.
Kwa wanawake kama Fatma Ramadhani na karibu watu milioni mbili walioguswa na EnDev, mustakabali wao sasa haukumbani tena na changamoto ya moshi bali ni wenye mwanga, safi na uliojaa fursa.
Programu ya EnDev inafadhiliwa kwa ushirikiano wa wafadhili mbalimbali wakiwemo; Shirika la Maendeleo la Ujerumani, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, Norad na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), UKAid, Shirika la Misaada la Australia na Sweden.