Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yazindua mkakati na mpango wa uwekezaji wa kuendeleza sekta ya mbegu

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde (wa nne kushoto), pamoja na wageni wa ngazi za juu, wakizindua kwa pamoja Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Mbegu na Mpango wa Uwekezaji, ramani ya mwelekeo iliyobuniwa kuleta mageuzi katika sekta ya mbegu hadi mwaka 2030.




Dodoma. Serikali ya Tanzania imezindua rasmi Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Mbegu Tanzania pamoja na Mpango wa Uwekezaji, hatua inayoweka dira ya kitaifa ya kuimarisha sekta ya mbegu nchini hadi mwaka 2030.

Uzinduzi huo ulifanyika wakati wa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu Tanzania uliofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 500 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Washiriki hao walijumuisha wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Wabunge, Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Chama cha Wafanyabiashara wa Mbegu Tanzania (TASTA), AGRA, Washirika wa Maendeleo, taasisi za kifedha, Wakulima, Sekta binafsi na taasisi za utafiti.

Mkakati huo uliandaliwa chini ya uongozi wa Wizara ya Kilimo kupitia mashauriano mapana na wadau mbalimbali, na unatoa mfumo wa pamoja wa kuimarisha upatikanaji, usambazaji, udhibiti wa ubora pamoja na kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji, ubunifu na ushiriki wa sekta binafsi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde alisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha mifumo ya uzalishaji, usambazaji na udhibiti wa ubora wa mbegu nchini.

Wadau wa sekta ya mbegu walishiriki katika uzinduzi wa nyaraka hizo mbili za kimkakati—Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Mbegu na Mpango wa Uwekezajizenye lengo la kuimarisha sekta ya mbegu nchini hadi mwaka 2030.

“Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya uzalishaji, usambazaji na udhibiti wa ubora wa mbegu kupitia TOSCI na TARI ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na salama,”alisema Mhe. Silinde.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuendeleza sekta ya mbegu.

“Mkutano huu unatoa jukwaa muhimu kwa wadau kujadili fursa na changamoto zinazoikabili sekta ya mbegu na kubaini mikakati ya vitendo ya kuboresha uzalishaji, uthibitishaji na usambazaji wa mbegu bora nchini Tanzania,” alisema Chimagu.

Mchakato wa kuandaa mkakati huu uliungwa mkono na Taasisi ya Kimataifa ya Usimamizi wa Maji (IWMI) kupitia programu za CGIAR Ukama Ustawi Initiative na Scaling for Impact, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya nchini New Zealand, na kutekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la ASPIRES Tanzania.

Akiwasilisha mkakati huo, Mkurugenzi wa shirika la ASPIRES Tanzania, Profesa David Nyange alieleza malengo makubwa yaliyowekwa kwa ajili ya maendeleo ya sekta hiyo.

“Mkakati huu unaweka malengo ya kitaifa yenye dira kubwa, ikiwemo kuongeza mara mbili eneo linalotumia mbegu bora kutoka takribani hekta milioni tatu hadi hekta milioni sita ifikapo mwaka 2030, pamoja na kuongeza mtandao wa wauzaji wa pembejeo za kilimo kutoka takribani 3,000 hadi 12,000 nchini,” alisema Prof. Nyange.

Naye Dkt. Idil Ires wa IWMI alibainisha kuwa utekelezaji wenye mafanikio wa mkakati huo utahitaji uwekezaji na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

“Kutoka kwenye mkakati hadi kufikia matokeo halisi kutahitaji uwekezaji wa pamoja, ushiriki madhubuti wa sekta binafsi na ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za utafiti, sekta ya fedha na washirika wa maendeleo,” alisema Dkt. Ires.

“Vilevile, ni muhimu kutambua kuwa matumizi ya mbegu bora pekee hayawezi kujenga ustahimilivu wa kilimo kwa kiwango kikubwa bila upatikanaji wa uhakika wa maji na uwekezaji katika umwagiliaji,” aliongeza Dkt. Ires.

Uzinduzi wa Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Mbegu Tanzania unaashiria mwanzo wa hatua mpya katika maendeleo ya kilimo nchini.

Kupitia kuimarisha mifumo ya mbegu bora, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuboresha uratibu katika mnyororo wa thamani wa mbegu, Tanzania inaweka msingi imara wa kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ushindani wa sekta ya kilimo, kuzalisha ajira na kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mamilioni ya wakulima nchini.