Bukene yapata ofisi mpya ya mbunge
Mwonekano wa ofisi ya Jimbo la Bukene, wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.
Muktasari:
- Ofisi ya Jimbo la Bukene imezinduliwa rasmi ambapo imetakiwa kuwa kiungo kati ya mbunge na wananchi.
Nzega. Wananchi wa Jimbo la Bukene wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora, sasa watanufaika na huduma za karibu zaidi za uwakilishi baada ya kuzinduliwa rasmi kwa ofisi ya jimbo hilo, hatua inayolenga kurahisisha utoaji wa maoni, usikilizaji na utatuzi wa kero zinazowakabili.
Ofisi hiyo imezinduliwa leo Juni 9, 2026 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega, Winifrida Funto, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Funto amesema ofisi hiyo inapaswa kuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na mbunge wao, ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa hata pale mbunge anapokuwa nje ya jimbo.
Amesema ni muhimu ofisi hiyo kufunguliwa kila siku za kazi na wananchi wanaoifika wapate majibu ya changamoto zinazowakabili.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega, Winifrida Funto, akizindua rasmi ofisi ya Jimbo la Bukene wilayani humo.
"Mwananchi akifika ofisini ajisikie kweli amefika mahali sahihi na apate majibu ya shida iliyomleta. Jengo ni zuri, lakini huduma zinazotolewa zinapaswa kuwa bora zaidi," amesema.
Funto amesema msingi wa utendaji bora ni kuwasikiliza wananchi na kuyafanyia kazi maoni yao kwa kuwa si wakati wote huwasilisha changamoto pekee, bali pia mawazo yanayoweza kuchangia maendeleo ya jimbo.
"Wasikilize wananchi kila wakati. Ushauri na maoni yao yafanyiwe kazi kwa manufaa ya jimbo zima kwani wakati mwingine huleta mawazo yenye tija kwa maendeleo," amesema.
Awali, Mbunge wa Bukene, John Luhende, amesema kukamilika kwa ofisi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa wananchi ya kuhakikisha wanakuwa na eneo rasmi la kufikisha changamoto na maoni yao.
"Ofisi hii ni mwanzo wa utekelezaji wa ahadi zangu. Kazi sasa ni yetu sote. Tuleteeni maoni, mapendekezo na kero ili tushirikiane kujenga Bukene yetu," amesema.
Luhende amesema Serikali imekubali kujenga kwa kiwango cha lami barabara za Itobo–Bukene–Mambali pamoja na Nzega–Itobo–Kagongwa, hatua itakayorahisisha usafiri, kupunguza gharama za usafirishaji na kuchochea biashara.
Mbunge wa Jimbo la Bukene, John Stephano Luhende, akizungumza na wananchi wa jimbo hilo baada ya uzinduzi wa ofisi ya jimbo.
"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekubali kutujengea barabara hizi kwa kiwango cha lami. Hii itapunguza gharama za usafiri, kuharakisha usafirishaji wa mazao na kuimarisha shughuli za biashara," amesema.
Mbunge huyo pia amesema ameshughulikia deni la zaidi ya Sh2 bilioni ambalo Halmashauri ya Bukene ilikuwa inaidai kampuni ya ujenzi wa reli ya kisasa ya Yapi Merkezi, kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Amesema kampuni hiyo tayari imeanza kulipa deni hilo ambapo zaidi ya Sh60 milioni zimelipwa na imekubaliana kulipa zaidi ya Sh130 milioni kila mwezi hadi deni lote litakapomalizika.
Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na uzinduzi wa ofisi hiyo wakisema utarahisisha upatikanaji wa huduma na mawasiliano na mbunge wao.
Mkazi wa Bukene, Shilaja Masunga, amesema kwa muda mrefu jimbo hilo halikuwa na ofisi bora ya mbunge jambo lililokuwa likikwamisha utoaji wa huduma.
"Ofisi ya zamani ilikuwa chakavu na hata watumishi hawakukaa kwa muda mrefu. Sasa tuna uhakika wa kupata huduma wakati wote wa kazi," amesema.
Naye Hilda Kapambala amesema uwepo wa ofisi hiyo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Bukene, huku akiitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ili kuongeza fursa za biashara.
"Barabara zikiwa nzuri tutafika sokoni kwa haraka zaidi na kufanya biashara kwa ufanisi. Pia magari yataongezeka na kurahisisha shughuli zetu za kila siku," amesema.