Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manispaa ya Iringa yajipanga kukarabati shule chakavu

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakisikiliza Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26 . Picha na Christina Thobias

Muktasari:

  • Manispaa ya Iringa imesema imeanza mipango ya kukarabati shule chakavu hatua kwa hatua, huku madiwani wakisisitiza utekelezaji wa haraka ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Iringa. Manispaa ya Iringa imesema imejipanga kukarabati shule zote chakavu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, kufuatia madiwani kuibua hoja ya urekebishaji wa miundombinu katika shule kongwe zenye uhitaji mkubwa.

Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Ibrahim Ngwada, amesema Februari 10, 2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26 kuwa elimu ni kipaumbele cha halmashauri, hivyo ukarabati wa shule utafanyika kulingana na upatikanaji wa rasilimali.

“Lengo letu ni kuhakikisha shule zote zinaboreshwa hatua kwa hatua kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia,” amesema Ngwada.

Hoja ya ukarabati iliibuliwa na Diwani wa Kata ya Mkimbizi, Eliud Mvela, aliyehoji ni lini Shule ya Msingi Igeleke itajengewa madarasa mapya na matundu ya vyoo kutokana na uchakavu uliopo.

Akijibu hoja hiyo, Ngwada amesema manispaa imeanza kupanga vipaumbele vya ukarabati, huku shule zenye uhitaji mkubwa zikipewa nafasi ya kwanza.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema ukarabati wa miundombinu ya elimu ni jukumu la serikali kwa kushirikiana na wadau na jamii, akibainisha kuwa mipango ya maboresho inaendelea.

“Shule zenye uhitaji mkubwa zitapewa kipaumbele, lakini ushiriki wa wananchi katika michango na ufuatiliaji utasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi,” amesema Mlawa.

Ngwada ameongeza kuwa manispaa inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza mapato ya ndani, ikiwamo kupanga vizuri wafanyabiashara na kudhibiti biashara holela, ili kuongeza uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo ukarabati wa shule.

Amesema uongozi utaendelea kufuatilia miradi yote iliyoahidiwa kwa wananchi ili ihakikishe inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Wakizungumza na Mwananchi Digital Februari 11, 2026, baadhi ya wananchi wamesema wanatarajia kuona ukarabati wa shule za zamani ukifanyika haraka kutokana na uchakavu mkubwa uliopo katika madarasa.

Wameeleza kuwa baadhi ya majengo yana nyufa, paa zinazovuja na sakafu zilizoharibika, hali inayowaweka wanafunzi katika hatari hasa wakati wa mvua.

Mkazi wa Igeleke, Judith Audinie, amesema mazingira ya shule nyingi hayaridhishi na yanahitaji maboresho ya haraka ili kulinda usalama na kuboresha ufaulu wa wanafunzi.

“Madarasa mengi ni ya zamani na hayajawahi kufanyiwa ukarabati wa maana kwa muda mrefu,” amesema mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.