NCCR Mageuzi bado haijazindua kampeni, yajifungia kupanga ratiba
Muktasari:
- Wiki moja baada ya kampeni za urais kuanza rasmi, chama cha NCCR-Mageuzi hakijaingia rasmi kwenye ulingo wa kampeni. Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Ameir Ali, amesema chama kiko katika vikao vya ndani kuandaa ratiba ya uzinduzi na mikakati ya kitaifa.
Dar es Salaam. Wiki moja imepita tangu pazia la kampeni za urais na ubunge kufunguliwa rasmi Agosti 28, 2025, lakini chama cha NCCR-Mageuzi hakijaonekana kuanza mikutano yake ya kampeni.
Katika ratiba ya kampeni za wagombea urais iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), chama hicho licha ya kuorodheshwa miongoni mwa vyama vilivyo tayari kuanza mbio za Ikulu, ratiba ya INEC haioneshi siku ya uzinduzi wa chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Septemba 6, 2025, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Zanzibar, Ameir Ali, ameeleza kuwa chama hicho kipo katika vikao vya ndani kupanga ratiba hiyo.
Amesema chama hakijachelewa kwa sababu ya matatizo bali kipo katika maamuzi ya ndani na kitaweka wazi mipango yake baada ya kukamilika.
"Chama kipo katika hatua za mwisho za kupanga ratiba ya uzinduzi na mikutano ya kampeni, tutakapokamilisha maandalizi hayo tutatoa taarifa rasmi kuhusu Uzinduzi huo," amesema.
Kuchelewa kwa NCCR-Mageuzi kuanza mbio zake kusaka Ikulu, kumekuja wakati vyama vingi vikiwamo CCM, CUF, Chaumma, Makini, NLD na UPDP tayari vimeanza kuzunguka mikoni kufanya kampeni zake baada ya kuzindua rasmi kwa nyakati tofauti.
Historia na changamoto za ndani
NCCR Mageuzi ni miongoni mwa vyama vya upinzani vilivyokuwa na ushawishi mkubwa katika miaka ya 1990, hasa wakati wa mwanzo wa demokrasia ya vyama vingi viliporejea tena nchini.
Hata hivyo, chama hicho kimekumbwa mara kwa mara na migogoro ya kiuongozi iliyoathiri uimara wake na kutikisa nguvu yake kisiasa.
Miongoni mwa migogoro iliyowahi kutikisa chama hicho ni ule wa kugombea uenyekiti na usajili wa viongozi, hali iliyosababisha kuondoka kwa baadhi ya makada wake akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa, James Mbatia na viongozi wenzake waandamizi kukaa kando.
Tofauti hizo ziliwahi kufikishwa mahakamani na Tume ya Uchaguzi mara kadhaa, hata hivyo maamuzi yake bado yaliathiri mshikamano na kuaminiana ndani ya chama hicho.
Kuhusu hofu kuwa kuchelewa kuanza kampeni kutachochea changamoto katika kujenga ushawishi na kufikia wapiga kura wengi, hasa ikizingatiwa kwamba muda wa kampeni ni mfupi kuzungumza na wananchi wa nchi nzima kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Ameir ameonesha kutokuwa na wasiwasi.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa chama hicho kipo imara na kitaingia rasmi kwenye uwanja wa kampeni mara baada ya kumaliza maandalizi yake.
"Chama kipo imara na kilishathibitishwa na ofisi ya Msajiri wa vyama vya siasa nchini kuwa kinashiriki uchaguzi huu, tukimaliza kupanga ratiba tunazindua na kuanza rasmi kampeni," amesema.