Serikali yatoa Sh1.5 bilioni kwa ujenzi wa matundu ya vyoo shule 22 Mbeya Vijijini
Muonekano wa vyoo viliyojengwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, katika Shule ya Sekondari Malama, Kata ya Nsalala wilayani Mbeya. Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
- Hatua hiyo ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa mwaka 2024 baada ya kufanya ziara na kuelezwa changamoto za miundombinu katika sekta ya elimu, ikiwemo uhaba wa walimu.
Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh1.5 bilioni kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya matundu mapya ya vyoo kwenye shule za sekondari 22 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa mwaka 2024 alipofanya ziara wilayani humo na kuelezwa changamoto mbalimbali, hususan uhaba wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa na walimu.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Aprili 22, 2026 na Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Mbeya, Stanley Mwasi, baada ya kupokea matundu 12 ya vyoo vya wavulana katika Shule ya Sekondari Malama, yaliyojengwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) CCM Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela.
Imeelezwa kuwa miezi miwili iliyopita, Mwaselela alifanya ziara na kukagua miundombinu katika Shule ya Sekondari Malama, Kata ya Nsalala, na kukabidhi madawati 200.
Katika ziara hiyo, alibaini changamoto ya uhaba na ubovu wa miundombinu ya matundu ya vyoo vya wavulana na kuahidi kujenga matundu 12.
“Awali, miezi miwili iliyopita, MNEC alifanya ziara na kukabidhi madawati 200 katika shule hii, lakini alishtushwa kuona hali hafifu ya miundombinu ya vyoo vya wanafunzi wa kiume na kuahidi kujenga, jambo ambalo kimsingi ameliteketeza kwa vitendo,” amesema.
Siku 100 za Rais
Amesema katika kutatua changamoto ya uhaba wa walimu, ndani ya siku 100 kupitia Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, wamepokea walimu 106 wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari 40.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela (katikati), akizungumza na viongozi mbalimbali wakati wa hafla ya kukabidhi matundu 12 ya vyoo aliyojenga katika Shule ya Sekondari Malama. Picha na Hawa Mathias
Mwasi amesema hatua hiyo imeongeza morali kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, jambo ambalo litaleta matokeo makubwa ya kuzalisha wataalamu katika nyanja mbalimbali.
“Lakini tunamshukuru MNEC kwa kusitisha michango kwa wazazi wa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani na kubeba jukumu la kugharamia mwenyewe, jambo ambalo limeleta tija,” amesema.
Kauli ya CCM
Naye MNEC Mwaselela ametaja sababu ya kujenga miundombinu hiyo kuwa ni baada ya kubaini kuwepo kwa uhaba na hali mbaya ya matundu ya vyoo yaliyokuwa yakitumiwa na wanafunzi zaidi ya 400.
“Rais amewekeza fedha nyingi sana kwenye miradi ya sekta ya elimu, lakini sisi wasaidizi wake tusipokuja kuwatia moyo walimu na wanafunzi, hatutakuwa na shukrani kati yetu na wananchi,” amesema.
Ametaja kazi ya MNEC ni kumwakilisha Mwenyekiti wa CCM Taifa katika mkoa husika, kuhakikisha siasa zinaenda sambamba na kugusa maisha ya watu, hususan katika sekta ya elimu.
“Nilipofanya ziara na kukabidhi madawati 200, nilibaini hali hafifu ya matundu ya vyoo vya wanafunzi wa kiume na kuahidi kujenga vingine vipya 12, ambavyo leo nimevikabidhi,” amesema.
Maagizo
Mwaselela ameagiza viongozi wa wilaya na mashina kufanya ziara za kusikiliza na kuibua kero za wananchi, na si kujifungia maofisini, ikiwa ni kutekeleza maagizo ya Mwenyekiti wa Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Acheni kujifungia, tokeni mkaifanye ziara za kuibua changamoto za wananchi ili tuweze kuzibaini na kuzielekeza halmashauri izitekeleze kwa kubana posho za vikao,” amesema.
Kuhusu utekelezaji wa ilani
Mwaselela amesema katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, Halmashauri ya Mbeya Vijijini imeelekezwa kujenga vyumba vya madarasa 724 na matundu ya vyoo 640.
Nyingine ni ujenzi wa nyumba za walimu 27, shule moja ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, sambamba na kukamilisha maboma 112 yaliyopo ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi.
Kwa upande wa shule za msingi, imeelekezwa ujenzi wa matundu ya vyoo 312 na nyumba za walimu, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi, kifungu cha 198, cha kufikisha maendeleo kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Aprili 21, 2026, Mwaselela alichangia matofali 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa bweni na bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Mwaselela, sambamba na kutoa motisha ya Sh3.4 milioni kwa walimu kufuatia matokeo mazuri ya wanafunzi wa kidato cha pili.
Kauli ya uongozi wa shule
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Malama, Neema Mwakimenya, ameshukuru kukamilishwa kwa ujenzi wa miundombinu ya matundu ya vyoo na kusema kuwa itasaidia utulivu wa masomo kwa wanafunzi wa kiume shuleni hapo.
“Kimsingi tunashukuru sana kwani awali hali ilikuwa mbaya kulikuwa na matundu 10 yaliyokuwa yakitumiwa na wanafunzi wa kiume 429, lakini ongezeko la matundu 12 linafanya kufikia idadi ya vyoo 22,” amesema.
Mwakimenya ameishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya kujifunzia mashuleni, jambo ambalo limeongeza morali kwa walimu na wanafunzi kufanya vyema kwenye masomo.
Kauli za wananchi
Amina Ally, mkazi wa Tarafa ya Mbalizi, amesema wana kila sababu ya kupongeza jitihada za MNEC katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kugusa jamii kwa kuchangia miradi ya maendeleo.
“Tunaona jitihada zake za kujitoa kwa hali na mali, ikiwemo kutuondolea mzigo wa kuchangia fedha za masomo ya ziada kwa watoto wetu wanaojiandaa kufanya mitihani. Jambo hili linaonyesha kujali, na tutamuombea kwa Mungu amlinde,” amesema.