Chakula kisicho salama kinavyoweza kupoteza nguvu kazi ya Taifa

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Habiba Hassan Omar akizungumza wakati wa kongamano la kuadhimisha Siku ya Usalama wa Chakula Duniani Zanzibar leo Juni 8, 2024.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa watu milioni 600 wanaugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama, kati ya hao 420,000 wanapoteza maisha. 

Unguja. Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Habiba Hassan Omar amewataka wadau wa chakula nchini kuzingatia usalama ili kulinda afya ya mtumiaji.

 Akifungua kongamano la kuadhimisha siku ya usalama wa chakula duniani Juni 8, 2024 katika Mkoa wa Mjini Magharibi, amesema kuna madhara mengi yanayosababishwa na mpangilio mbovu wa chakula. Amesema jambo hilo ni tishio kwa afya za binadamu na pia linapoteza nguvu kazi ya Taifa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa watu milioni 600 wanaugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama, kati ya hao 420,000 wanapoteza maisha. 

Dk Habiba amesema jamii inaathirika kwa kutumia vyakula visivyo salama, hivyo amewataka Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), kutumia maadhimisho hayo kutoa elimu kwa jamii kuhusu usalama wa chakula na kulinda afya ya mtumiaji.

“Usalama wa chakula ni mnyororo unaoanzia kwa mkulima hadi kufika kwa mtumiaji, mfano mkulima anaweza kuzalisha chakula salama na kusafirisha salama, lakini tatizo likaanzia kwa muuzaji kushindwa kukihifadhi na kikamfikia mtumiaji hakina tena kiwango cha usalama kinachohitajika,” amesema.

Amewataka wananchi kutumia mlo kamili na kufanya mazoezi ili kulinda afya na kupunguza madhara yanayotokana na chakula kisicho salama.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA, Dk Burhan Othman Simai amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutoa elimu kwa jamii ili kujilinda kutokana na uchafuzi wa chakula unaosababisha matatizo, yakiwemo magonjwa yasioambukiza, ambayo husababisha kifo na ulemavu wa kudumu.

Akitoa maelezo kuhusu usalama wa chakula, ofisa kutoka ZFDA, Aisha Suleiman Bundakazi amesema chakula salama ni kile ambacho hakitamletea madhara ya kiafya mtumiaji baada ya kukitumia.

Amesema chakula salama ni ambacho kimeepukana na vihatarishi vya kifizikia na kibiolojia, hivyo usalama wa chakula ni muhimu kwani kisicho salama kinaweza kuleta madhara kwa mtumiaji.

Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Bernard Chove amesema wanaoangaliwa zaidi katika usalama wa chakula ni wakulima, wauzaji na walaji lakini kundi la wasafirishaji limesahauliwa jambo ambalo linaweza kusabaisha uchafuzi kwa kiasi kikubwa.

“Elimu duni ya uhifadhi wa chakula na vifungashio vyetu vinaweza kuchangia uchafuzi wa chakula wakati wa usafirishaji, inabidi tuwapatie elimu wenzetu wasafirishaji,” amesema Chove.

Mtaalamu wa uhakika wa chakula na lishe kutoka Shirika la Chakula Duniani (FAO), Stella Kinambo amesema ni vyema kufanya utafiti na uchambuzi sahihi ili kufikia malengo ya kimataifa ya usalama wa chakula na kutoa mwongozo kwa watumiaji.

Kinambo amesema elimu ya usalama wa chakula kwa watumiaji bado ni ndogo, Watanzania wengi wanazingatia uwepo wa chakula bila kujali ubora na usalama wake.

Ofisa miradi Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar, Haji Abdulla amewasihi wazalishaji kuzalisha bidhaa bora ili kukidhi vigezo vya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaingiza bidhaa zenye usalama kumlinda mtumiaji.

Aliipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wananchi wanapata chakula salama, ikiwemo ujenzi wa maabara ya kisasa ya ZFDA.

Maadhimisho ya siku ya chakula duniani hufanyika Juni 7 kila mwaka, kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa ‘usalama wa chakula, jiandae kwa usiyoyatarajia.’