Askari aliyedaiwa kupotea akutwa amefariki msituni
Muktasari:
- Polisi yasema uchunguzi wa vinasaba (DNA) unafanyika kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Unguja. Askari wa Kikosi cha Valantia (KVZ), Haji Machano Mohamed ambaye alidaiwa kupotea akiwa katika mafunzo ya uongozi, mwili wake umepatikana ukiwa umeharibika msituni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Septemba 28, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Daniel Shillah askari huyo alipotea tangu Agosti 8, 2024 na taarifa zilitolewa Kituo cha Polisi Dunga, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja Agosti 9, 2024.
Kamanda huyo amesema askari huyo alikuwa akihudhuria mafunzo ya uongozi katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Dunda.
Katika taarifa hiyo, amesema siku hiyo saa nane mchana katika msitu uliopo jirani na chuo hicho, askari huyo akiwa na wenzake alipotea katika mazingira ambayo hayakueleweka.
“Baada ya wenzake kurejea kambini ndipo ilipobainika askari huyo haonekani, hivyo taarifa zilipelekwa Polisi kituo cha Dunga na uchunguzi kuendelea,” imeeleza taarifa.
Kamanda Shillah amesema Septemba 26, 2024 saa 10.00 jioni kwenye msitu huo ulionekana mwili wa binadamu ukiwa umeharibika.
Amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ulibaini mwili huo ukiwa na nguo na viatu ambavyo vinafanana na alivyokuwa amevaa askari huyo siku alipopotea.
Katika mfuko wa suruali ilipatikana simu ambayo imetambuliwa kuwa ni ya askari huyo.
“Uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea ukiwepo wa ulinganisho wa vinasaba (DNA) kwa lengo la kubaini ni kitu gani kilichomkuta mwenzetu kupoteza uhai ili hatua nyingine za kisheria zifuate,” amesema.