Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM, ACT- Wazalendo waliamsha Pemba

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar Dk Mohamed Said Dimwa akizungumza na wanachama wa chama hicho baada ya kukagua ujenzi wa tawi la Kengeja Mtambile Pemba

Muktasari:

  • CCM na ACT-Wazalendo vinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ikilenga kuleta utulivu wa kisiasa Zanzibar.

Unguja. Siku moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kudai mwanachama wake mpya kuvamiwa na mali zake kuchomwa moto, ACT-Wazalendo kimeibuka kikieleza madai hayo ni mbinu chafu za kutengenezwa.

Septemba 11, 2024 CCM  ilidai mwanachama wake Salum Mohamed Juma, aliyedaiwa kujiunga nacho akitokea ACT-Wazalendo, mali zake zilichomwa moto usiku wa kuamkia Septemba 10, 2024 katika Shehia ya Wingwi wilaya ya  Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa alidai usiku wa Septemba 10, watu wasiojulikana walivamia makazi ya mwanachama huyo na kuchoma moto godoro, vitambulisho, nguo na bendera ya CCM kisha kukimbia baada ya wananchi kujitokeza kuzima moto huo.

Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Timothy Mwampagale jana Septemba 11 alisema yupo safarini, lakini hakuwa amepokea taarifa hizo, akiahidi akizipata atazifanyia kazi.

Kutokana na madai hayo, Dk Dimwa aliagiza Polisi kuhakikisha watu wote waliohusika kwenye tukio hilo wanashughulikiwa. Kwa upande wake, ACT-Wazalendo limetaka jeshi hilo na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mgeni Khatib Yahya kuacha kile ilichodai kutumika kisiasa.

Dk Dimwa akizungumza akiwa ziarani alisema, "Chama cha Mapinduzi tuna dhamana ya kulinda amani na utulivu wa nchi kwa gharama yoyote, hatuwezi kukubali Zanzibar irudi katika siasa za chuki na machafuko kwa wananchi wasiokuwa na hatia.”

“Wito wangu kwa vyama vyote vya upinzani tutafakari na kujisahihisha kwa kuacha mara moja siasa za uchochezi zinazoweza kuibua machafuko, hivyo tuwe viongozi wa kuelekeza mema na kudhibiti wafuasi wetu wasifanye vurugu," alisema Dk Dimwa.

Alisema CCM kinatarajia vyombo vya ulinzi na usalama nchini vitachukua hatua za haraka kwa kuhakikisha watu wote waliohusika na uhalifu huo bila kujali cheo, chama cha siasa au umaarufu wanafikishwa katika vyombo vya kisheria.


Ilichosema ACT-Wazalendo

Katika taarifa kwa umma iliyosainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), Omar Ali Shehe leo Septemba 12, imewalalamikia CCM ikidai inashirikiana na Polisi na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, kuwakamata na kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria viongozi wa chama hicho na baadhi ya wafuasi wake.

Miongoni mwa wanaodaiwa kukamatwa ni kiongozi wa chama hicho Micheweni, Rashid Khalid Salim.

Wengine ni wanachama Bakar Mbarouk Ali, Is-haka Rashid Salim na Khamis Rashid Salim.

ACT-Wazalendo inadai chanzo cha sintofahamu ni baada ya viongozi wa CCM kujaribu kupandisha bendera ya ACT kisha kuishusha kwa madai ya kuaminisha umma kuwa wanachama wa chama hicho wamejiunga na CCM.

“Kwa sababu viongozi na wanachama wetu wanajua wajibu wao na haki ya kulinda chama chao, walihakikisha wanazuia upandishwaji wa bendera ya chama chetu na kisha kushushwa, jambo lililozua hasira kwa viongozi wa CCM na ndipo waliandaa mbinu mbovu ya kufukiza nyumba ya mwanachama wao ili kupata sababu ya kuwaweka kizuizini viongozi na wanachama wetu,” inadai ACT-Wazalando.

Kiongozi huyo amesema wanaamini vitendo vinavyoanza kujitokea akidai vinasaidiwa na vyombo vya dola kuwatisha viongozi wao, vinatia wasiwasi ukiwa ni wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“ACT-Wazalendo tunatoa wito kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya Micheweni kutojihusisha na masuala ya kisiasa badala yake wajikite katika masuala muhimu ya kusimamia haki za wananchi. Pia tunalitaka Jeshi la Polisi kukataa kutumika kisiasa watumie weledi na taaluma,” amesema.


DC Micheweni

Akizungumzia tuhuma dhidi yake, Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mgeni Khatib Yahya amesema hawaangalii chama bali usalama wa wananchi na mali zao.

Licha ya kukiri kuwashikilia kwa muda watu wanne akiwemo aliyedai ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, Mgeni amesema walifanya hivyo kulinda usalama baada ya kuibuka vurugu kati ya pande zote mbili.

“Zile kauli zilizokuwa zikitolewa pale zilikuwa za kuhatarisha amani kama vyombo vya ulizi na usalama tulilazimika kuwashikilia watu wanne ili kutuliza ghasia kisha waliachiwa,” amesema.

Amefafanua, “baada ya hapo tumekaa na viongozi wa pande zote mbili, CCM na ACT-Wazalendo kuwaeleza namna ambavyo wanatakiwa kulinda usalama wa raia na kuepuka migongano isiyokuwa ya lazima.”