Kamati ya Bajeti yaikataa ripoti mradi wa HEET
Muktasari:
- Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali akiri udhaifu, kamati yaagiza iandaliwe ripoti mpya
Unguja. Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi imeikataa ripoti ya utekelezaji mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), ikiagiza iandaliwe upya.
Wajumbe wa kamati hiyo pia wameonyesha wasiwasi iwapo chuo hicho kitakamilisha mradi huo kwa wakati, wakieleza umebaki muda mchache wa ukamilishaji wa mradi lakini utekelezaji bado upo nyuma.
Serikali ya Tanzania ilipokea mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 425 (sawa na Sh972 bilioni), kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mei, 2021 hadi Juni, 2026.
Zanzibar ni miongoni mwa wanufaika kupitia Suza ambacho kilitengewa Dola za Marekani milioni 20 (sawa na Sh45.9 bilioni) katika utekelezaji wa maeneo makuu manne: Ujenzi au ukarabati wa miundombinu, uimarishaji wa mitalaa na kuanzisha mbinu bora za ufundishaji.
Maeneo mengine ni kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kufundisha na kujifunza na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa kitaaluma na uongozi wa chuo.
Hata hivyo, mradi huo umetekelezwa eneo jingine ambalo halikuwa na bajeti awali, ambalo wajumbe hao wamesema ni kosa.
Akiwasilisha taarifa kwa wajumbe hao chuoni hapo leo Novemba 9, 2024, Mratibu wa Mradi Suza, Dk Hashim Hamza Chande amesema wapo nyuma kwa takribani mwaka mmoja katika utekelezaji wa mradi waliouanza Septemba, mwaka 2022.
Wakati mradi ukiwa umebakiza miezi 20 tu kukamilika, katika kipengele cha ujenzi na ukarabati ambacho kinachukua asilimia ya 70 fedha ya mradi mzima, chuo ndiyo kimeingia mkataba wa ujenzi wa maabara ya sayansi na shule ya kilimo.
Mjumbe wa kamati hiyo, Suleiman Masoud Makame licha ya kupongeza hatua zilizofikiwa, amehoji sababu za kuchelewa kuanza ujenzi huo na mbinu gani watakazotumia kuhakikisha wanaukamilisha kwa wakati.
Katika majibu yake, Dk Chande ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, amesema wamechelewa kwa sababu chuo hakina uwezo wa kuthibitisha mkandarasi kwa mujibu wa masharti ya mradi, wanaohusika kuthibitisha hilo ni WB.
Amesema sababu nyingine ni mradi kuwa na mahitaji makubwa ya muda, rasilimali watu na fedha ambavyo havikupangiwa bajeti.
“Changamoto nyingine ni taratibu za manunuzi zinazosababisha kuchelewa upatikanaji wa bidhaa za huduma na vifaa, ujuzi mdogo wa watendaji, mfumo wa bei na kupanda na kushuka kwa Dola ya Marekani,” amesema Dk Chande
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Suza imesaini mkataba wa majengo mawili ya shule ya kilimo na maabara ya sayansi Novemba 4, 2024 na Kampuni ya Mohammed Builders ya jijini Dar es Salaam ambaye anatakiwa kukamilisha ujenzi huo ndani ya miezi 18.
Eneo hilo ndilo linalochukua sehemu kubwa ya mradi kwani unatumia Dola za Marekani milioni 14.574 (sawa na Sh37.520 bilioni) huku tayari zimeshatumika asilimia 21.94 ya bajeti mpaka Oktoba, mwaka huu.
Katika uboreshaji wa nyenzo na vifaa vya kujifunzia, ripoti imesema tayari kompyuta 180 zimenunuliwa na kufungwa katika maabara, jumla ya Dola 221,000 (Sh568.9 milioni) zimetengwa na kutumika sawa na silimia 100 ya bajeti.
Katika eneo la uimarishaji wa mitalaa, tayari minane kati ya tisa imetayarishwa na mingine minane inatakiwa kufanyiwa marekebisho. Dola za Marekani milioni 291,225 (sawa na Sh749.74 milioni) zimetumika ikiwa ni wastani wa asilimia 68 ya bajeti ya Dola 430,000 (sawa na Sh1.107 bilioni) ya bajeti nzima iliyotengwa katika eneo hilo.
Kwa upande wa kuwajengea uwezo wafanyakazi, hadi Oktoba mwaka huu, wanataaluma 72 kati ya hao 33 kwa ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) na 39 Shahada ya Uzamili wamepata masomo kupitia mradi, huku wafanyakazi 127 wakipata mafunzo ya muda mfupi kwa fani tofauti.
Eneo hilo limetengewa Dola milioni 2.39 (sawa na Sh6.152 bilioni) na hadi Oktoba mwaka huu Dola milioni 1.082 (Sh2.787 bilioni) zimetumika ikiwa ni wastani wa asilimia 43.3 ya bajeti ya eneo hilo.
Mpangilio wa ripoti
Akizungumza baada ya kuwasilishwa ripoti hiyo, mjumbe wa kamati, Suleiman Masoud Makame amesema jinsi ilivyo inaibua maswali mengi kwani haijaeleza kitaalamu.
Mjumbe mwingine, Profesa Omar Fakih Hamad amesema hatua ya mradi iliyofikiwa na kipindi kilichobaki, bado inasikitisha.
“Imebaki miezi 20 pekee kukamilika kwa mradi, lakini ukiangalia hatua tulizopo tena kwenye ujenzi wa majengo ndiyo kwanza juzi umesainiwa mkataba, hapa tunaona kweli ukamilishaji wa mradi, tunapaswa kupewa maelezo mbinu gani zitatumika kuhakikisha malengo yanafikiwa,” amesema.
“Tunataka tupate maelezo ya jitihada mpya mtakazotumia au kama hazipo tujue tunakwendaje,” amesema.
Profesa Omar amesema katika miradi hiyo wametaja kiwango cha fedha kilichopatikana na kutoka lakini taarifa haijataja kipindi gani zimetolewa, akisema bado nayo hiyo ni kasoro kwa taratibu za kiuhasibu.
Kuhusu mkataba walioingia na mkadarasi, amesema kwenye taarifa ilipaswa kuonyesha muda muafaka walipoingia mkataba na tarehe ambayo anapaswa kumaliza mkataba huo, lakini nalo halijaonyeshwa.
Kuhusu mradi wa kununua kompyuta amesema katika ripoti haijachanganua lakini kwa mtazamo wa kawaida kiasi kinachotajwa kununua kinaonekana kikubwa, hivyo bila kuweka mchanganuo wake haieleweki.
“Mimi nimefanya hesabu zangu kwa wastani inaonyesha kompyuta moja imenunuliwa kwa Sh3.160 milioni, sasa mtu anaweza kujiuliza kwa nini kompyuta moja inunuliwe fedha zote hizi, sasa hapa panahitaji maelezo aina gani kwanza ya kompyuta zilizonunuliwa na kwa nini lazima ziwe hizo,” amesema Profesa Omar ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya kompyuta.
Mjumbe mwingine, Asha Abdalla Mussa amesema viwango vya fedha kwenye maeneo husika vinatofautiana na ripoti waliyopewa mwaka jana, huku taarifa ikionyesha fedha zilizotengwa na kutolewa lakini haionyeshi kilichobaki.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, awali amesema kuna ufafanuzi wa kimazingira na kitakwimu, hata hivyo naye amekiri kutoridhishwa na ufafanuzi wa wataalamu, hivyo kuiomba kamati kuwapa muda ili wairekebishe na kuiwasilisha kwao wakati mwingine.
“Waheshimiwa naomba nikiri kuwa mimi mwenyewe sijaridhishwa na majibu ya ripoti, tunaomba tupewe muda iandaliwe upya ripoti hii ili kuweka katika utaratibu unaotakiwa,” amesema.
Amesema kwa kawaida kamati inatakiwa kwenda mara moja kwenye taasisi husika, hivyo watahakikisha wanagharamia tena iwapo itabidi kamati irejee kusomewa ripoti nyingine.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwanaasha Khamis Juma amesema Kamati ya Bajeti ni tofauti na ya kisekta kwani wao wanaangalia fedha zinavyoingizwa na jinsi zinavyotumika.
Amesema kama kwenye ripoti haionyeshi jambo hilo linawawia vigumu wao kuandaa ripoti yao ambayo wanatakiwa kuiwasilisha barazani.
“Mmejitahidi katika utekelezaji wenu ila mmetutengenezea maswali mengi, inawezekana hamfahamu tunachokitaka, tukipata tunachotaka hatuna tatizo kwa hiyo ripoti hii ikaandaliwe upya kisha tupate ripoti safi,” ameagiza.