Maboresho ya daftari la wapiga kura kuanza kesho

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbetto akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inaanza zoezi la kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu la mpiga kura, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikihamasisha wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi.

Unguja. Wakati zoezi la maboresho kwenye daftari la kudumu la kupiga kura likianza, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewaomba wananchi waliotimiza sifa za kupiga kura kujiandikisha kwenye daftari hilo ili waweze kushiriki katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025.

Novemba 8, 2023, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi alitangaza kuwa uboreshaji huo utaanza kesho Jumamosi Desemba 2, 2023 na unatarajia kufanyika kwa siku 45 na utahitimishwa Januari 15, 2024.

Leo Ijumaa, Desemba Mosi, 2023 katika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Zanzibar, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa chama hicho Zanzibar, Khamis Mbeto amezungumza na waandishi wa habari ambapo amewahamasisha wananchi wajitokeza kwa wingi kujiandikisha.

“Nawasihi wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la mpigakura kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba na itawasaidia kuchagua viongozi bora ifikapo mwaka 2025,” amesema na kuongeza;

“Ikiwa atatokea mwananchi yeyote amezuiwa na Sheha kujiandikisha, basi hana budi kulumbana naye kwa kuwa  kutakuwa na fomu maalumu ya kuandika malalamiko na mtu atapata haki yake.” amesema

Mbeto, amewataka watendaji wa Serikali kutumia kauli nzuri wanapowahudumia wananchi katika kuwatatulia shida zao, huku wakikumbuka kuwa wapo kwenye nafasi hizo kuwatumikia wananchi.

"Serikali imeteua viongozi kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, nao wana haki ya kujua kinachoendelea katika maeneo yao wakihoji wanatakiwa kupewa majibu mazuri na sio kauli chafu kwani ni haki yao," amesema Mbeto

Amesema kutokana na kauli zisizo na afya, wananchi wamekuwa wakiogopa kupeleka malalamiko kwa viongozi hao, na kujikuta wakikimbilia kwa viongozi wa chama hicho.

“Kuna wakurugenzi, makatibu wakuu na baadhi ya mawaziri wamekuwa wakilalamikiwa mara nyingi kwa kauli zisizofaa, nawaomba waachane na tabia hiyo badala yake wawajibike kwa mujibu wa matakwa ya utumishi wa umma,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mbeto amesema Serikali imetenga Sh12 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia wananchi watakaopisha ujenzi wa uwanja wa ndege kisiwani Pemba.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mbeto, Serikali haina nia ya kuwaumiza wananchi wake na ikitokea mtu hajaridhika na fidia hiyo ana fursa ya kupeleka malalamiko yake.

Amesema kuwa chama hicho kimefanikiwa kupata kampuni 25 za uwekezaji kutoka Saudi Arabia ambazo zitakuja mwezi ujao na watawekeza katika kilimo, nishati na gesi, madini na utalii.