Mmoja afariki mvua kubwa iliyonyesha Zanzibar
Muktasari:
- Amesema mvua hiyo kubwa ilionyesha kwa takribani siku tano imesababisha kifo cha mtu mmoja na kupelekea familia 1440 kuathirika na wengine kuhama makaazi yao kwa muda.
Unguja. Mvua kubwa ilionyesha kwa siku tano Zanzibar imesababisha mtu mmoja alietambulika kwa jina la Abuubakar Abdalla (25) kufariki Dunia huku familia zipatazo 1440 zikiathiriwa vibaya na mvua hiyo na baadhi kuhama makaazi yao.
Akizungumza na Mwananchi Digital Mkurugenzi mtendaji wa idara ya maafa Zanzibar Makame Khatib Makame amesema mtu huyo alifariki baada ya kuzama katika moja ya mtaro wa maji maeneo ya Sebleni mjini hapa na maiti yake kuonekana siku ya pili kufuatia jitihada za wananchi waliokua wakimtafuta.
Amesema kufariki kwa kijana huyo kulitokana na kuzidiwa na kina kirefu cha maji na kukosa msaada kutoka kwa watu wa karibu kwani wakati tukio hilo linatokea siku ya jumapili oktoba 5 kulikua na mvua kubwa ambayo ilipelekea watu wengi kubaki majumbani mwao.
‘’Kwa sababu ya mazingira haya kijana huyu alishindwa kupata msaada katika muda muafaka na kupelekea kufariki Dunia lakini wananchi walifanikiwa kupata maiti yake siku ya pili ambayo ilikua jumatatu ya oktoba 6.
Akizungumzia kuhusu kadhia ya kuingiliwa na maji kwenye makaazi yao familia zipatazo 1440 amesema Serikali wanaendelea kufanya tasmini ya kina kuona ni kwa namna gani ambayo wataweza kuwasaidia wananchi waliokumba na hali hiyo.
Said Abdalla mkaazi wa tomondo ziwamaboga alisema uwepo wa mvua hizo kubwa ilimlazimu yeye na familia yake kuhama kabisa nyumbani kwao na hadi sasa bado wameshindwa kurudi.
Amesema wamelazimika kubaki kwa ndugu zao maeneo ya Mombasa wakisubiri maji kupungua ama kutoka kabisa kwenye nyumba wanayoishi ili waweze kurudi.
Asma Awadhi mama wa watoto wawili na mkaazi wa fuoni chunga alisema yeye na watoto wake walilazimika kuhama usiku mkubwa kufuatia mvua hizo.