Othman: Kutofuatwa sheria kumechangia dhulma ya ardhi Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud akizungumza na wananchi wa Makaani Vitongoji Kusini Pemba baada ya kupokea malalamiko ya wananchi eneo hilo wakidai kudhulmiwa eneo lao.

Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud ameziagiza Mamlaka pamoja na Jamii, kuzingatia utambuzi wa ardhi kuepusha dhulma na migogoro isiyomalizika.

Othman ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 29, 2023 alipokutana na watendaji na wananchi Makaani Vitongoji wakati akiwasikiliza malalamiko yao.

Amesema eneo hilo  linakabiliwa na changamoto nyingi za muda mrefu ambazo chimbuko lake ni kukosekana utaratibu wa mzuri wa kutambua ardhi hivyo kunahitajika juhudi za utatuzi wa pamoja.

"Tatizo na mahitajio makubwa ni kuwepo chombo cha kusimamia matumizi ya ardhi kama inavyohitajika katika miongozo ya kisheria bila hivyo dhulma ya raslimali hii itaendelea katika maisha yote," amesema

Ametaja mapendekezo ya Sheria saba zilizopitishwa Mwaka 1989, ikiwemo ya utambuzi wa ardhi ambazo amedai hazifuatwi.

Hata hivyo, ametaja njia bora ya kumaliza migogoro hiyo kwanza ni kuwahalalishia wananchi ardhi zao kabla ya kuanza kutambua ardhi hizo.

"Ukweli ni kwamba kwa kuzingatia maslahi binafsi hata kwa baadhi ya viongozi na watu wengine wenye mamlaka, kinachodhihiri ni kudhulumu na wengi kudhulumiwa haki ya ardhi, na hata baadhi yawakati kwamadai ya kukosa karatasi za nyaraka ambazo wengine wamezipata ili kutenda dhulma".

Akisisitiza juu ya mkanganyiko katika upatikanaji na utoaji wa nyaraka za ardhi Othman amesema: "Tatizo la Nchi yetu ni kwamba kila mmoja ni bosi wa ardhi, haijulikani ni Sheha, Mkurugenzi au yeyote yule maana kila mtu ana mamlaka na anatoa maamuzi ya ardhi,"

Hata hivyo, amewahakikishia wananchi kwamba Serikali itakabiliana na changamoto hiyo kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria na utaratibu unaostahiki kwakuhusisha sekta zote.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud, amesema wanajitajidi kukabiliana na malalamiko ya wananchi, zikiwemo changamoto za watu wa Kijiji hicho licha ya kwa kiasi kikubwa kwa sasa ndiyo kwanza zimeibuka na zinahitaji busara ya namna ya kukabiliana nazo.

"Dhamira yetu na dhamira ya Serikali hii ya Awamu ya Nane siyo kudhulumu wala kuwakosesha wananchi haki zao, bali la msingi ni kukaa na kushirikiana pamoja na kufuata taratibu," amesema Mattar

Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Ofisi yake zikijitokeza changamoto, ili kila mtu aweze kuendelea na maisha kwa kuzingatia haki.

Akitolea ufafanuzi baadhi ya Malalamiko ya Wananchi, juu ya madai ya ardhi yanayozunguka pia maeneo ya Vitongoji Kwareni, Liko la Vumba na Kimbu-Sadi, Ofisa wa Mazingira Wilaya ya Chake-Chake, Mwalim Khamis amesema uamuzi ya kuipima, kuitumia na kuihaulisha ardhi kwa watumiaji wakiwemo wawekezaji kunahitaji maamuzi ya sekta jumuishi.

"Wananchi na wamiliki wa maeneo hayo walistahiki kushauriwa, kufidiwa na pia kuongozwa juu ya utaratibu wa kulitumia tena kwaajili ya uzalishaji eneo ambalo sasa linatumika kuchimba mawe, kokoto na raslimali za namna hiyo," amesema Mwalim

Baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho, akiwemo Saleh Nassor Juma alisema wanachokishuhudia kwasasa ni madhila yanayotokana na ugumu wa maisha wakilazimishwa kuondoka kwenye ardhi yao.

"Ardhi yetu imevamiwa, inachukuliwa na tunalazimishwa kuondoka kama mnavyoona, tunahisi hii ni kusaliti hata ile Sera na miongozo ya Mzee (Abeid Amani) Karume ya kwamba wananchi wapate ahueni ya kumiliki pahala pa maisha yao," amesema Saleh.