Pemba kuwa kitovu cha utalii

Pemba. Kamisheni ya Utalii Zanzibar imefungua rasmi Bonanza la Utalii, Utamaduni na Michezo kisiwani pemba ambalo linatajwa kuwa mwanga wa kukifanya kisiwa hicho kuwa kitovu cha utalii.

Bonanza hilo limefunguliwa leo Jumatano Novemba 29, 2023 na Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahim Bhaloo, ambapo amesema lengo ni kutangaza utalii adimu wa pemba ikiwemo wa michezo.

“Bonanza hili tumelifanya Pemba kwa ajili ya kukuza utalii wa michezo, urithi na utajiri wa utamaduni wa Pemba lakini pia historia ya kisiwa hiki kinatoa mandhari nzuri kwaajili ya michezo, utalii na utamaduni,”amesema.

Bonanza hilo linalojulikana kwa jina la ‘Pemba Tourisport and Cultural Bonanza’ (PTCB) lililofunguliwa leo linatajiwa kufika tamati Desemba 3, 2023 ambalo linafanyika visiwani humo kwa awamu ya tano.

Mbali na kukuza utalii wa michezo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii, Hafsa Mbamba amesema bonanza hilo pia lina lengo la kukuza uchumi wa Pemba ambao kwa nkiasi kikubwa unategemea utalii.

“PTCB ina lengo la kuboresha kisiwa cha Pemba kwa kuunganisha tamaduni zake, michezo, urithi na vivutio vya asili na kwa kuwa utalii unachangia zaidi ya asilimia 29.2 ya Pato la Taifa la Zanzibar (GDP), PTCB inawakilisha njia ya kusisimua, kuimarisha na kukuza nafasi ya Pemba kiuchumi,”amesema.

Aidha, Hafsa amesema PTCB itasaidia kuongeza idadi ya watalii watakaotembelea kisiwa hicho maarufu kwa kuwa fukwe nzuri na safi.

Hafsa amesema michezo itakayoshindaniwa katika bonanza hilo ni pamoja na: Mashindano ya ngalawa, kuonyesha uhalisia wa vyakula vya asili na shunguli za kupakasa ukili, mashindano ya Duffu, Gwaride la Punda (Donkey Parade), mchezo wa Ngombe.

Michezo mingine ni; Kuendesha baiskeli na kukimbia na mashindano ya Kuogelea