Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SMZ yakiri changamoto ya kurundikwa vifusi mbele ya nyumba za watu

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar Bakar akijibu maswali katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar

Muktasari:

  • Serikali imesema inaelewa changamoto hiyo na imekuwa ikimuelekeza mkandarasi kuondoa vifusi visivyotumika ili kupunguza adha.

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri wananchi kuathirika na vifusi vinavyowekwa mbele ya nyumba zao kutokana na ujenzi unaoendelea katika barabara za ndani.

Hayo yamebainishwa leo Juni 9, 2026 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar Bakari, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Magomeni, Mahfoudh Abdalla Mohammed, katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Unguja.

Mwakilishi huyo amesema licha ya wananchi kushukuru kwa ujenzi wa miradi ya BIG-Z hasa barabara za ndani, lakini miradi hiyo imekuja na changamoto kubwa za wasimamizi kurundika vifusi katika majumba ya watu, kutokamilisha uzibaji wa mitaro na kuchelewa kuwalipa fidia wananchi waliopata matatizo ya nyumba na mengineyo.

Kutokana na hali hiyo, mwakilishi huyo aliuliza iwapo Serikali inazitambua changamoto wanazopitia na kauli yake katika kuzitatua.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Dk Hamad amesema Serikali inaelewa kwamba kuwepo kwa suala la vifusi katika maeneo ya ujenzi imekuwa ni changamoto kwa wakazi wa maeneo hayo.

“Katika juhudi za kuondokana na kadhia hiyo, imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya ujenzi wa mradi na kumuelekeza mkandarasi kuondoa vifusi visivyotumika tena ili kupunguza adha kwa wananchi,” amesema.

Amesema licha ya mkandarasi kuondoa kifusi kisichotumika pale anapokamilisha ujenzi katika eneo husika, lakini baadhi ya vifusi kwa kiasi fulani hubakishwa kwa ajili ya kurudishiwa pembezoni mwa mitaro inapokamilika ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuifanya mitaro hiyo kuwa imara zaidi.

Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, mkandarasi yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha mitaro, na vifusi vilivyobakia vinatumika kurudishiwa pembezoni mwa mitaro.

“Hivyo, tunawaomba wananchi waendelee kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki cha kumalizia ujenzi wa mitaro na barabara zilizobakia katika maeneo yao,” amesema.

Kuhusu ulipaji wa fidia, amesema mradi wa BIG-Z umetumia zaidi ya Sh4.3 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia katika miradi ya ujenzi wa barabara za ndani na mitaro ya maji ya mvua iliyojengwa katika shehia za Magomeni, Meya, Nyerere, Muungano, Kwa Wazee, Amani, Kilimahewa Juu, Kilimahewa Bondeni na Shaurimoyo.

Hata hivyo, amesema kuna wananchi wachache waliobaki ambao nyumba zao zimepata madhara au sehemu ya ardhi zao kuchukuliwa wakati ujenzi unaendelea.

Wananchi hao ni wale ambao hawakuwemo katika tathmini ya awali, jambo linalolazimu tathmini nyingine kufanyika ili kuwatambua waathirika hao na kujua gharama halisi.

Amesema kwa sasa taratibu zote zimekamilika na wananchi wote waliobakia watalipwa fidia zao kwa mujibu wa taratibu zilizopo hivi karibuni.

“Hivyo, naomba niwahakikishie na kuwatoa wasiwasi wananchi wote walioathirika na ujenzi wa mradi huu kwamba mradi utamlipa kila mwananchi anayestahiki kulipwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo,” amesema.

Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba kwa maslahi mapana ya taifa lao.

Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zinaratibu na kusimamia utekelezaji wa mradi wa kuimarisha uchumi Zanzibar (BIG-Z). Miongoni mwa kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa barabara za ndani na mitaro ya maji ya mvua.

Ujenzi wa miradi hiyo unatekelezwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi chini ya mkandarasi kutoka kampuni ya CRJE na mshauri msimamizi wa ujenzi kutoka kampuni ya Dar Al-Handash.