Teknolojia ya nyuklia yatua Zanzibar
Muktasari:
- Hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za udhibiti na kuhamasisha matumizi salama ya nyuklia karibu na wananchi wa Zanzibar.
Unguja. Katika kuimarisha huduma, tafiti na ubunifu unaolenga kuongeza wigo wa matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi anatarajia kuzindua jengo jipya la Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Kanda ya Zanzibar.
Akizungumza na waadishi wa habari Zanzibar Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliekeza tume hiyo kupanua wigo wake.
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, jengo hilo lililojengwa Dunga Zuze Mkoa wa Kusini Unguja, litazinduliwa Novemba 11, 2024 ambapo uzinduzi huo utaifanya tume hiyo kufikisha ofisi na maabara katika kanda nne Tanzania na visiwani.
Kanda hizo ni Kaskazini (Arusha), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Zanzibar (Unguja).
“Sambamba na hilo, hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za udhibiti na kuhamasisha matumizi salama ya nyuklia karibu na wananchi wa Zanzibar,” amesema.
Amesema teknolojia ya nyuklia ikitumika vizuri inaweza kuongeza tija katika sekta mbalimbali kwani teknolojia hiyo inatumika kuchunguza na kutibu ugonjwa wa saratani, kuboresha mbegu za mazao hasa yale ambayo yanaugumu kustawi na yanatoa mazao kidogo, kuua vimelea vinavyosabisha chakula kuharibika kudhibiti kuzaliana kwa wadudu wanaoeneza magonjwa kama vile mbung’o.
Pia, inahakikisha uimara na ubora wa maungio ya matenki na mabomba makubwa ya mafuta au maji, kuhakiki ubora katika ujenzi wa barabara na reli na kusafisha maji taka kwa ajili ya shughuli ngingine na utafiti wa mafuta na gesi.
“Pamoja na manufaa yaliyoainishwa, katika nchi yetu, kumekuwa na ongezeko kubwa la fursa za kutumia sayansi na teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, afya, viwanda, mifugo, na maji,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, matumizi ya teknolojia hii yatachangia maendeleo katika nyanja hizo kwa kuboresha uzalishaji, kuongeza ubora wa bidhaa, na kuhakikisha usalama na ufanisi wa huduma zinazotolewa.
Hata hivyo, amesema ili fursa hizi zitumike kikamilifu na kwa ufanisi, kuna haja ya kuwa na miundombinu ya kisasa na madhubuti ambayo itawawezesha wataalamu na wanasayansi kufanya kazi katika mazingira yanayowezesha ubunifu na ugunduzi mpya.
Amesema maabara hizi zitakuwa msingi mzuri wa shughuli za utafiti na mafunzo, zikiwawezesha wataalamu kufanikisha tafiti na miradi mbalimbali inayolenga kuboresha huduma na bidhaa katika sekta hizo muhimu.
Matumizi ya maabara hizi pia yatasaidia kuongeza fursa za kufanya biashara na nchi nyingine kwa kuhakikisha usalama wa bidhaa zinazoingia na kutoka nje ya nchi.
Kadhalika, Waziri Mkenda amesema uwepo wa maabara hii utaongeza uwezo wa kitaaluma wa wataalamu, kuwezesha uhamishaji wa teknolojia na kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa katika utafiti wa kisayansi na maendeleo ya teknolojia.
Kutokana na manufaa makubwa ya teknolojia ya nyuklia, Serikali ilizindua ufadhili kupitia Ufadhili wa Samia Extended inayolenga kusomesha vijana wa Kitanzania nje ya nchi katika ngazi ya umahiri kwenye masuala ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, kuanzia mwaka huu, vijana watano wa Kitanzania watapata ufadhili wa shahada hizo za umahiri.
“Pia, Serikali, kwa kushirikiana na wadau, itaendelea kuongeza kiwango cha ufadhili kulingana na uwezo wa kibajeti, ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na wataalamu wa kutosha kati nyanja husika,” amesema.
Hivi karibuni alipotembelea jengo hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, Profesa Joseph Msambichaka alisema zamani ilibidi kubeba sampuli kutoka Zanzibar kupeleka Arusha au Dar es Salaam kwa ajili upimaji wa mionzi jambo ambalo liligharimu fedha nyingi pamoja na muda ili kupata majibu.